ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 18, 2017

RC MTAKA: MFUKO WA BIMA YA AFYA NDIO MTINDO WA KISASA WA HUDUMA KATIKA NCHI ZOTE DUNIANI

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka akihutubia katika Mkutano wa wadau wa Mfuko wa Bima ya afya NHIF/CHF

Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Bima ya afya Taifa (NHIF) Bi Anne Semamba Makinda akizungumza katika Mkutano wa wadau wa Mfuko wa Bima ya afya NHIF/CHF Mkoani Simiyu

Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Bima ya afya Taifa (NHIF) Bi Anne Semamba Makinda (kushoto) akizungumza jambo na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka (kulia) katika Mkutano wa wadau wa Mfuko wa Bima ya afya NHIF/CHF
Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Bima ya afya Taifa Ndg Leonard Konga akitoa taarifa ya Maboresho ya huduma kwa wanachama na wadau wa mfuko wa Bima ya afya
Rc Mtaka akisisitiza jambo wakati wa mkutano huo
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Bima ya afya Taifa (NHIF) Bi Anne Semamba Makinda akisisitiza jambo katika Mkutano wa wadau wa Mfuko wa Bima ya afya NHIF/CHF Mkoani Simiyu
Kaimu Meneja wa Bima ya afya Mkoa wa Simiyu ambaye pia ni Meneja wa Mfuko wa Bima ya afya Mkoa wa Shinyanga Ndg Immanuely Imani akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za NHIF Mkoa wa Simiyu
Rc Mtaka akielezea ruksa ya uwekezaji katika mkoa wa Simiyu ikiwa ni pamoja na ruhusa ya kutoa eneo la ardhi bure kwa yeyeote anayetaka kuwekeza katika ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza dawa za binadamu
Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe Tano Mwera akishauri uongozi wa Bima ya afya Taifa kuweka wazi magonjwa yasiyotibiwa kwa kutumia Bima ya afya huku akitilia mkazo kadhia ya unyanyapaa wanayokumbana nayo watumiaji wa Bima ya afya
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Bima ya afya Taifa (NHIF) Bi Anne Semamba Makinda (kushoto) akizungumza jambo na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka katika Mkutano wa wadau wa Mfuko wa Bima ya afya NHIF/CHF alipozuru katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
Wadau wa Mfuko wa Bima ya afya NHIF/CHF wakisikiliza kwa makini huku wengine wakipata nafasi ya kuuliza maswali kwenye mjadala katika Mkutano huo

Na Mathias Canal, Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka amesema kuwa ushirikiano baina ya Ofisi yake,Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na wananchi kwa ujumla utaufanya mkoa huo kuwa mabalozi wazuri kwa wananchi kujiunga kwenye mfuko wa Bima ya Afya kama ambavyo lengo la Bodi na wizara ya afya limekusudiwa Kwani wananchi kujiunga na Mfuko wa Bima ya afya ndio mbinu pekee rahisi na kisasa katika matibabu duniani kote.

RC Mtaka ameyasema hayo wakati akihutubia katika Mkutano wa wadau wa Mfuko wa Bima ya afya NHIF/CHF, Mkutano uliokuwa na madhumuni ya kubaini changamoto zinazowakabili wananchi wanaotumia Mfuko wa Bima ya afya sawia na kutoa elimu ya umuhimu wa kujiunga na Mfuko wa Bima ya afya.

Ameeleza kuwa kujiunga na mfuko huo ni muhimu kwa wananchi kwani watapunguza gharama kubwa wakati wa matibabu kwa wale ambao hawajajiunga kwani wanapaswa kutambua kuwa ugonjwa hauna Siku rasmi ya kuingia mwilini unawakumba watu wakati wowote pasina kubisha hodi.

Katika kufikia dhamira ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli ili kuwa na Tanzania ya viwanda Mkuu Huyo wa Mkoa wa Simiyu ameiomba Bodi ya Mfuko huo wa Bima ya afya kuanzisha ofisi za Mkoa kwani watapatiwa eneo la ujenzi pasina kulipia.

Hata hivyo amesema kuwa kwa yeyote anayetaka kuwekeza kwa kujenga kiwanda cha kutengeneza Dawa na vifaa tiba atapatiwa eneo Bure kwa ajili ya kuanzisha kiwanda hicho.

Awali akitoa taarifa ya Maboresho ya huduma kwa wanachama na wadau wa mfuko wa Bima ya afya Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Bima ya afya Taifa Ndg Leonard Konga amesema kuwa Mfuko wa Bima ya Afya ni Taaisi ya umma iliyoundwa kwa mujibu wa sheria sura Na 395 TL 2002 ambapo ni matokeo ya utekelezaji wa Sera ya mabadiliko katika sekta ya afya iliyoanza kutekelezwa kuanzia miaka ya 1990.

Mfuko huo umeanzishwa kwa dhamira ya kutoa Bima ya afya kwa makundi mbalimbali ya wananchi, Kujenga uwezo wa kifedha kwa vituo, Kushirikisha sekta binafsi katika kuharakisha maendeleo ya sekta ya afya.

Konga amesema kuwa mafanikio ya utekelezaji wa shughuli za Bima ya afya yanategemea kila mdau kutimiza wajibu wake kwani mazingira ya kiutendaji ni kusimamia na kutekeleza miongozo na maagizo ya serikali kupitia wizara yenye dhamana ya kusimamia upatikanaji wa huduma za afya.

Amebainisha kuwa lengo mahususi katika utekelezaji wa mpango wa Mfuko wa Bima ya afya ni kuwawezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma za afya kuanzia ngazi ya Zahanati hadi ngazi ya hospitali ya Mkoa, Kuongeza wigo mpana zaidi kwa watanzania wanaopata huduma za matibabu kupitia Bima ya Afya.

Naye Kaimu Meneja wa wa Bima ya afya Mkoa wa Simiyu ambaye pia ni Meneja wa Mfuko wa Bima ya afya Mkoa wa Shinyanga Ndg Immanuely Imani akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za NHIF Mkoa wa Simiyu amezitaja changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na Upungufu wa dawa katika baadhi ya vituo, Ukosefu wa vifaa tiba na ubovu wa majengo, Baadhi ya waajiri kuchelewesha madai, Watoa huduma wachache kuwasilisha madai yenye kutiliwa shaka na mwitikio mdogo wa wananchi kujiunga na NHIF/CHF.

Sambamba na hayo pia ameelezea matarajio ya Mfuko wa Bima ya afya katika Mkoa wa Simiyu kuwa ni pamoja na kuelimisha watoa huduma kutumia fedha za uchangiaji kwa ajili ya kununulia dawa, kuhimiza watoa huduma kuomba mikopo ya vifaa tiba, ukarabati, dawa na vitendanishi.

Matarajio mengine ni pamoja na kuendelea kuimarisha ukaguzi wa waajiri ili kutoa michango sahihi kwa wakati, Kuimarisha mifumo ya ulipaji madai ili kuzuia malipo ya madai yasiyo halali na kuendelea kushirikiana na Halmashauri katika kuhamasisha jamii kujiunga na Mfuko wa Bima ya afya.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Bima ya afya Taifa (NHIF) Bi Anne Semamba Makinda Amesema kuwa Bodi yake imekusudia kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi sawia na kupinga vikali lugha mbovu zitolewazo na baadhi ya watoa huduma katika sekta ya afya dhidi ya wananchi wanaoenda kupata matibabu katika Zahanati, Vituo vya afya, Hospitali za Wilaya, Mikoa na Rufaa.

Amesema katika maeneo mengi waliyopita wamebaini kuwa wananchi wengi wametumia fedha zao kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya lakini wanapoenda kuhudumiwa wanakumbana na matusi pasina huduma bora.
Bi Makinda amesema kuwa wanaendelea na utaratibu wa kubaini zahabati, kituo cha afya ama Hospitali zinazokiuka utaratibu Na baada ya kubainika tu watachukuliwa hatua Kali za kisheria.

Hata hivyo ameeleza jinsi ambavyo mtandao wa matibabu wa serikali ulivyo mzuri kwani unaanzia ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya, Mkoa hadi Taifa.

Bodi hiyo imeahidi kufungua Ofisi za mikoa mipya ya Njombe, Katavi, Geita huku wakiahidi pia kuanza ujenzi na kufungua ofiai katika Mkoa wa Simiyu baada ya kupewa eneo la ujenzi Bure na Mkuu wa Mkoa huo Mhe Antony Mtaka.

No comments: