AMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU MKUTANO WA KAMATI NDOGO YA MAWAZIRI WA SIASA NA DIPLOMASIA WA JUMUIYA YA MAENDELEO YA KUSINI MWA AFRIKA (SADC)
Mkutano wa Kamati Ndogo ya Mawaziri wa Siasa na Diplomasia wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC Inter State Politics and Diplomacy Sub Committee-ISPDC) utafanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 21 hadi 24 Februari 2017.
Mkutano huo ambao utahudhuriwa na zaidi ya wajumbe 100 kutoka nchi wanachama wa SADC utatanguliwa na kikao cha Makatibu Wakuu na Maafisa Waandamizi utakaofanyika tarehe 21 na 22 Februari, 2017. Kikao hicho kitafuatiwa na kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje tarehe 24 Februari, 2017.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga ataongoza majadiliano katika kikao cha Mawaziri. Aidha, Balozi Dkt. Aziz P. Mlima, Katibu Mkuu wa Wizara ataongoza majadiliano ya kikao cha Makatibu Wakuu na Maafisa Waandamizi.
Ikumbukwe kuwa, Mkutano wa ISPDC unafanyikia hapa nchini kwa kuwa Tanzania ndio Mwenyekiti wa sasa wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Organ on Politics, Defense and Security Cooperation). Aidha, Ibara ya 6 (5) ya Itifaki ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama inamuelekeza Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Mawaziri kuitisha Mkutano wa ISPDC angalau mara moja katika mwaka wa uongozi ndani ya SADC Organ.
Kamati Ndogo ya ISPDC inajumuisha Mawaziri wote kutoka nchi wanachama wa SADC wenye dhamana ya kusimamia masuala ya Siasa na Diplomasia. Hivyo, tunatarajia Mawaziri 15 wa Mambo ya Nje pamoja na Makatibu Wakuu wao kushiriki katika Mkutano huu. Agenda zitakazojadiliwa zitajikita katika maeneo ya kisiasa, kiulinzi na kiusalama katika kanda.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 20 Februari, 2017
No comments:
Post a Comment