ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, February 12, 2017

VIDEO: Bunge laonya ubabe, kutaja majina


By Sharon Sauwa, Mwananchi ssauwa@mwananchi.co.tz

Dodoma. Sakata la kutangaza hadharani majina ya watu wanaotakiwa kuhojiwa kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya jana lilizidi kushika kasi baada ya vigogo watatu kutoa kauli zinazoonyesha kutokubaliana na utaratibu unaotumiwa katika vita dhidi ya dawa hizo haramu.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai ameonya dhidi ya mwelekeo unaoonyesha kuingiliana kwa mihimili ya nchi na kuagiza kuwa mtu anayemtaka mbunge ni lazima atoe taarifa kwake.

Wakati akisema hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Adadi Rajab ameelekeza makamanda wa polisi wa mikoa na wilaya kukaa na wakuu wao wa mikoa na wilaya na kuwaeleza utaratibu wa kushughulikia watuhumiwa wa makosa ya jinai, akisema suala hilo ni la kitaaluma.

Naye Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema na kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, amekataa wito wa Makonda kuripoti kambini, akisema hana mamlaka hayo na kwamba atafanya hivyo ikiwa tu ataitwa na mtu sahihi kisheria.

Kauli hizo zimetoka wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiendesha operesheni ya kupambana na dawa za kulevya kwa staili ya kutangaza kwanza majina ya watu wanaoshukiwa au anaoamini wana taarifa zinazoweza kusaidia kukamata wahusika wa biashara hiyo haramu.

Makonda ameshatangaza majina ya wanasiasa, wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wasanii na viongozi wa dini, ambao baadhi wamekaa rumande kwa siku kadhaa, kupekuliwa majumbani kwao na kufikishwa mahakamani.

Baada ya wabunge kupaza sauti zao kupinga staili hiyo, jana kwa nyakati tofauti viongozi hao wakuu wa taasisi hizo waliamua kuweka sawa mambo.

Ndugai aonya nchi kuvurugwa


Jana, Spika Ndugai alisema wakati akiahirisha Bunge kuwa, “kwenda kibabe kutaivuruga nchi”.

“Katika Mkutano wa Sita kulijitokeza hoja kuwa hadhi ya Bunge letu imeshuka. Napenda kukuhakikishieni kuwa iko pale pale, kama si kupanda,” alisema Ndugai.

Alisema hawana ugomvi wowote na mahakama wala Serikali na hawafikirii.

Alisema mambo ya ofisa mmoja kusahau mipaka ya kazi zake, ni ya kawaida ambayo mahali panapohusika watachukua hatua za kuyaweka sawasawa tu.

Alisema kama kuna mtu anamuhitaji mbunge, ni lazima amtaarifu.

“Kuna kikao unahitaji koramu (akidi) itimie. Wakati mwingine hata akikosekana mmoja inawezekana jambo hilo la kamati lisitekelezwe. Kwa hiyo kama kuna ofisa yoyote anamuhutaji mbunge, lazima aniambie. Hatuwezi kwenda hivyo. Kwa hakika kwenda hivyo kibabebabe kutaivuruga nchi,” alisema bila ya kutoa mifano.

Kabla ya kusema hayo, wakati mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Balozi Adadi Rajab akihitimisha michango ya wabunge kuhusu ripoti yao, alisema upelelezi wa kesi za jinai hauwezi kufanywa kwa kutaja majina ya watu hadharani.

Upelelezi ni taaluma

Balozi Adadi, ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kabla ya kustaafu, alisema kazi ya kusaka wauzaji wa dawa za kulevya ni ya kitaaluma.

“Investigation (upelelezi) wa kesi hizi kama za dawa za kulevya ni taaluma. Watu wanasomea. Kuna doctorate of investigation (shahada ya uzamivu ya uchunguzi). Sio kutaja watu tu hadharani,” alisema Adadi.

Balozi Adadi aliwashauri makamanda wa polisi wa mikoa na makamanda na wilaya kukaa na wakuu wao wa mikoa na wilaya kuwaeleza namna bora ya kufanya uchunguzi wa kesi za aina hiyo.

“Hao makamanda wamesomea kazi hizo za upelelezi. Upelelezi haufanywi kwa kutaja majina. Hatutaki kesi hizo ziende kufa mahakamani,” alisisitiza.

Kauli ya Balozi Adadi imekuja wakati wabunge wengi wakipinga utaratibu unaotumiwa na Makonda wa kutaja majina ya watu hadharani.

Tayari Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye pia ni kiongozi wa kambi ya upinzani, ameshasema hataenda kituo cha polisi kwa wito wa Makonda, huku Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, akisema kutaja watu kwa ajili ya kwenda kusaidia kutoa taarifa za biashara ya dawa za kulevya ni kuhatarisha maisha ya anayetakiwa kusaidia upelelezi.

Naye Mbowe, ambaye pamoja na wengine 64 alitakiwa waripoti kituo kikuu cha polisi jijini Dar es Salaam jana, alisema hawezi kuitikia wito wa mkuu wa mkoa kwa kuwa hana mamlaka hayo.

Badala yake, Mbowe amesema wiki ijayo atafungua kesi mahakamani kumshtaki Makonda kwa kumchafulia heshima yake aliyoijenga kwa miaka mingi ndani na nje ya nchi.

Lakini kamanda wa polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro amesema endapo Mbowe hataitikia wito huo bila kutoa taarifa yoyote ya dharura, watamfuata kwa kuwa Jeshi la Polisi linamuhitaji.

Mbowe atunisha misuli


Akizungumza na waandishi wa habari bungeni mjini hapa jana, Mbowe alisema wanaunga mkono vita hiyo, lakini wanapinga kuendeshwa kwa hila na kwa kutofuata sheria.

“Ni vyema mkatambua kuwa nchi yetu inaongozwa na Katiba, sheria na kanuni mbalimbali na (lazima zifuatwe) katika kutekeleza jambo lolote. Kama ni jinai kuna taratibu za kisheria,” alisema.

“Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam sio polisi na kwa mujibu wa sheria na hana mamlaka ya summons (wito) kwa watu kwenda polisi.”

Bila ya kuwataja majina, Mbowe alisema viongozi wa kupachikapachika wamejipa mamlaka ya kimungu ya kufikiria kwamba ukishaitwa kiongozi fulani, basi una mamlaka juu ya sheria.

“Tumeona kosa hili linafanywa na Rais na sasa linaigizwa na wakuu wa mikoa na wilaya, kufikiria kwamba ukishakuwa mkuu wa mkoa ama wilaya basi una mamlaka yote kisheria ,”alisema.

Alisema makosa ya jinai yana utaratibu wake na kwamba makosa ya dawa za kulevya yamewekewa sheria zake na yana vyombo rasmi vya kisheria vya kushughulikia.

“Mkuu wa mkoa hana investigative powers (mamlaka ya kiuchunguzi) ya kuchunguza dawa za kulevya. Tena kimsingi tukiangalia taratibu ambazo mkuu wa mkoa ametumia, unaona kabisa anawaepusha wafanyabiashara wa dawa za kulevya na mkono wa sheria kwa kuharibu ushahidi,” alisema.

Mbowe alisema makosa ya dawa ya kulevya hayana dhamana kwa hiyo huwezi kwenda kwenye hadhara na orodha ya majina ya watu wanaotuhumiwa.

“Mengine yameandikwa Philemoni, mengine yana jina moja. Una watuhumu viongozi kwa Watanzania wenzio kwa makosa mazito kama haya? Sisi ni viongozi, hatuongozi tu familia zetu. Hawa ni wabunge mimi ni kiongozi wa wabunge wote, ni mbunge wa jimbo, ni kiongozi wa kijamii, ni baba mwenye watoto, mke na familia,” alisema.

Alisema mkuu wa mkoa hana mamlaka ya kushughulikia jinai.

“Mkuu wa Mkoa anafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria ambayo haimpi mamlaka ya kuita watu kituo cha polisi, lakini (yeye) anawaonea Watanzania ambao hawajui sheria. Wanaona kwa sababu ni kiongozi wa Serikali wanaona ana mamlaka makubwa,” alisema.

“Mimi nitakuwa tayari kutoa ushirikiano wakati wowote kama taratibu za sheria zitafuatwa na vyombo vinavyohusika kisheria.”

Kuhusu tuhuma alizoitiwa polisi, Mbowe alipinga vikali.

“Ninakanusha kwa nguvu zote kuhusika kwa njia yeyote kufanya biashara au kutumia dawa za kulevya wakati wowote katika maisha yangu,” alisema kiongozi huyo.

“Mimi ni mtu mzima na kiongozi wa muda mrefu. Sijawahi kujihusisha kwa njia yeyote au kushirikiana na mtu yeyote anayefanya biashara hiyo haramu.”

Alisema Chadema kama chama kikuu cha upinzani na chama makini, sambamba na viongozi wengine wa vyama vya upinzani, wanakubaliana kwamba dawa za kulevya ni hatari kwa Taifa.

“Biashara hii imeachiwa kushamiri kwa miaka mingi kwa sababu wahusika wakubwa ni washirika ama ni wenza wa CCM. Kwa hiyo vita ya kupiga kelele dhidi ya biashara hii na watumiaji, imechelewa sana,” alisema Mbowe.

Alisema hawezi kukubali mtu mmoja awachafulie heshima yake na atahakikisha anamshtaki mahakamani.

“Hawa (wabunge) wanaongozwa na muuza dawa ya kulevya kweli? Upumbavu huo siwezi kukubali na Makonda atabeba mzigo huo.

“Sina ugomvi na Jamhuri na wala na waziri, Rais wala nani, ila tuna ugomvi na Makonda. Tutapambana kwenye vyombo vya sheria nchini na kimataifa hadi hiyo haki ipatikane. Na sijui kama ana fedha za thamani inayoweza kulipa kusafisha jina langu alilochafua.”

Mbowe, aliyekuwa ameongozana na wabunge wa kambi ya upinzani akiwemo kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema wiki ijayo watamfungulia mashtaka kwa kumchafua na kwamba hahitaji uchunguzi wa kipolisi kwa sababu anajijua hana hatia.

“Kwa hiyo sihitaji polisi waseme sina kosa. Eti waje, tukikuta hawana makosa tutawaachia. Tutawaachia? Unawadhalilisha watu halafu unasema utawaachia? How is Makonda going to clean my name? (atanisafishaje jina langu),” alisema.

“Nimejenga jina langu kwa miaka mingi, si jambo dogo na hii ndo tatizo la kuwapa mamlaka watoto wadogo wasiokuwa na busara. Unajua lazima hivi vyeo vya kupewa vitolewe kwa watu ambao wana busara.”

Alisema urafiki wa Makonda na Rais Dk John Magufuli haumpi mtu mamlaka ya kuwachafua viongozi wengine.

Alisema, “Hata ripoti ya maandishi ni ya kitoto sana mtu unaandika mmliki wa Slipway na Yatch Club ile ni klabu ya members (wanachama) haina mmiliki. Wewe mkuu wa mkoa unaweza kuandika mmiliki wa Yatch Club ambayo ipo kabla ya uhuru?”

“Sasa anaita watu 65 Dar es Salaam wakamuone leo (jana) mimi siwezi kwenda kwenye huo ujinga, ila nitakuwa tayari kuitwa na chombo chochote chenye mamlaka ya kisheria.”

Mbowe pia alilitaka Jeshi la Polisi kufanya kazi zake kwa mujibu wa sheria na si kwa matamko.

“Jeshi la Polisi au mamlaka yoyote ya kidola inafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria. Kanuni za kipolisi zinaelekeza namna ya kufanya kazi, si kila mtu amkamate mwingine. Polisi wamefundishwa namna ya kufanya uchunguzi.”

Alisema haiwezekani kufanya uchunguzi wa watu wanaojihusisha na dawa za kulevya kisha ukawaita polisi kwa siku tatu.

“Makonda anavuruga ushahidi, amekoroga. Kama kuna muuza unga nchi hii, tayari ameshaondoka, akibaki ataonekana mtu wa ajabu,” alisema Mbowe.

“Ukimhusisha mtu na dawa za kulevya, lazima uwe na ushahidi. Mimi nina uhakika, sijihusishi kwa asilimia 100.”

Naye Zitto Kabwe alisema anaungana na wabunge wa Ukawa kuonyesha umoja akiamini hashambuliwi Mbowe pekee bali upinzani wote.

“Mimi nimefanya kazi na Freeman, ameniibua nikiwa mtoto wa chuo kikuu. Angekuwa ni mtu anayehusika na dawa za kulevya, mimi ndo ningekuwa punda wake. Kwa hiyo mtu kuibuka na kutuhumu tuhuma kubwa kama hizo dhidi ya kiongozi wa umma, ni kitu ambacho kinapaswa kulaaniwa,” alisema.

“Nani anajua Makonda ataishia wapi. Tulisema bungeni kuwa ameanza na wasanii, kesho atataja wabunge, nadhani kuna haja na nyie waandishi kusaidia kuonyesha ni mamlaka gani ya sheria inampa mkuu wa mkoa mamlaka ya kutangaza raia kwenda kituo cha polisi,” alisema.

Alisema Makonda anayo mamlaka kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama kuagiza polisi kuchunguza na kuchukua hatua na kwamba hana mamlaka ya kuchunguza na kuagiza watu kwenda kituo cha polisi.

“Mimi ningekushangaa ungeenda kituo cha polisi. Umefanya uamuzi sahihi kutokwenda kama wanakuhitaji wakupe wito wa kisheria. Sio mtu apite barabarani tu na makaratasi yake ya kufungia vitumbua yameandikwa hovyo hovyo hata mwandiko utafikiri mtu hakufika darasa la pili halafu anatuhumu watu kama ambavyo amefanya,” alisema.

Mwisho

No comments: