ANGALIA LIVE NEWS
Saturday, February 11, 2017
Lema, mkewe wakwama tena
By Filbert Rweyemamu na Zulfa Musa mwananchipapers@mwananchi.co.tz
Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha imetupilia mbali tena maombi ya upande wa utetezi uliotaka kesi inayomkabili Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na mkewe, Neema ihamishiwe Mahakama Kuu.
Akisoma uamuzi huo jana, hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, Nestory Barro alisema pamoja na hoja za kisheria kutolewa na upande wa utetezi, bado hakuona sababu itakayofanya mahakama yake ishindwe kusikiliza kesi hiyo na kutoa uamuzi.
Awali mawakili wa upande wa utetezi, John Malya na Sheck Mfinanga walipinga hati ya mashtaka iliyotolewa na upande wa mashtaka kuwa ilikuwa na makosa, hivyo waliiomba mahakama ihamishie kesi hiyo Mahakama Kuu.
Barro alisema hoja kubwa aliyoiona ilikuwa ni kuhamisha faili la kesi hiyo liende Mahakama Kuu kujibu baadhi ya masuala ya kisheria, lakini pamoja na hayo hata mahakama yake inaweza kujibu masuala hayo hivyo alitaka mashahidi wa Jamhuri waanze kusikilizwa.
“Mahakama hii ina uwezo wa kisheria kusikiliza shauri hili. Ninachokiona hapa wakili Mfinanga unafanya makusudi kuchelewesha usikilizaji wa kesi. Tuache mashahidi watoe ushahidi wao tujue mbivu na mbichi ni zipi,” alisema Barro.
Hakimu Barro alisema hoja juu ya makosa ya hati ya mashtaka ambayo iliwasilishwa na upande wa utetezi ni kwamba kimsingi ni jambo linaloweza kufanyiwa masahihisho kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kifungu cha 234 na kuagiza upande wa Jamhuri kurekebisha mapungufu hayo.
Pamoja na uamuzi huo mdogo kutolewa, wakili Mfinanga aliweka kusudio la kukata rufaa ya kupinga uamuzi uliotolewa kwa kuwa sheria namba 361(1) A inampa nafasi hiyo, huku akiomba mwenendo wa kesi kusubiri uamuzi.
Lema na mkewe wameshtakiwa kwa tuhuma za kutuma ujumbe kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo unasema “karibu Arusha tutakudhibiti kama mashoga wanavyodhibitiwa Arabuni”.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment