Na Mussa Mbeho Katavi
WAZEE wanaonufaika na fedha zinazotolewa na serikali katika mpango
wake wa kunusuru kaya maskini kupitia mradi wa TASAF III Mkoani Katavi wameanza kufunguka juu ya manufaa wanayopata
kupitia mpango huo.
Wakizungumza na mwandishi wa gazeti hili hivi karibuni wakati wa zoezi la kugawiwa fedha hizo ikiwa ni mgao wa 15 tangu kuanza kwa mradi huo, wazee hao walisema wazi kuwa mpango huo umeanza kuboresha maisha yao sambamba na afya zao.
Walisema fedha hizo zimewawezesha kuwa na uhakika wa maisha sambamba na kupata milo 3 ya chakula na sasa wana afya
njema sana.
Mzee Paschal Daniel (75) mkazi wa kijiji cha misunkumilo
katika kata ya misunkumilo alisema mwanzoni alipewa sh 30,000 akazitumia kwa chakula tu lakini mgao uliofuata alinunua kuku 2 baadae 3.
Aliongeza kuwa fedha hizo japo ni kidogo lakini zinawasaidia sana kimaisha kwani zamani alikuwa anaishi maisha ya taabu sana ikiwemo kuomba omba lakini sasa haombi tena kwa watu.
‘Sasa siombi tena chakula kwa watu, naomba serikali
iache mradi huu uendelee, wasiuondoe,' aliongeza.
Mzee Magubika Andrea (80) mkazi wa kijiji cha Mitwigu anaeleza kuwa
tangu aanze kupata hela za TASAF III maisha yake yamebadilika sana
kwani ana uhakika wa kupata chakula kila siku na tayari amefuga kuku
10 na amepanga kununua bati moja moja ili kuezeka nyumba yake, anataka
kuondoa nyasi.
Mzee VITARIS PETRO (74) wa kijiji cha Ilembo alieleza bayana kuwa
alikuwa anaumwa sana na chakula kilikuwa hamna, lakini baada ya kupata
hela hizo akanunua dawa na chakula, sasa ameshapona na afya yake
imerudi vizuri hana wasiwasi tena ameanza kunawili.
‘Kama sio hizi hela za serikali ningekufa mapema, nilikuwa
naumwa sana, ndani chakula hamna, watoto hawaendi shule hata nguo
walikuwa hawana, baada ya kupewa hela sasa watoto wanasoma, na mimi
nimepona kabisa na nina kuku 6’, aliongeza.
Bi.Mery Paulo (74) mkazi wa kitongoji cha kawajense anasema hali yake ilikuwa duni sana lakini baada ya kuwezeshwa 40,000 za awali watoto wake 3 na wajukuu 2 waliokuwa wameacha shule sasa wanaenda wote na mmoja amekuwa wa kwanza darasani kati ya watoto 60.
‘Nyumba yangu ilikuwa ya nyasi sasa nimebadilisha nimeweka bati upande
mmoja nitamalizia upande mwingine kidogo kidogo nikipata hela
nyingine’, alisema Salome.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa TASAF Mkoa wa katavi Iginas Kikwala alisema kuwa mradi huu umewasaidia sana wananchi wengi kwani wengi wao walikuwa wanakula mlo mmoja tu kwa siku kutokana na kuishi maisha ya umaskini.
Alisema kuwa changamoto kubwa anayokumbana nayo kuwa ni baadhi ya
wananchi kuomba kuongezewa hela kwa msingi kwamba hela wanayopewa ni kidogo na kwamba wanashindwa kuigawa kwa chakula na kuanzisha miradi.
No comments:
Post a Comment