Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi wa wilaya za Mkuranga na Temeke, Ofisini kwake jijini Dar es salaam Februari 7, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Wilaya za Temeke na Mkuranga kuangalia namna ya kupunguza msongamano uliopo katika eneo la Mbagala.
Moja ya hatua alizowashauri kuchukua ni pamoja na kuhamisha kituo cha mabasi ya mikoa ya kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kutoka Temeke hadi Mkuranga.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Februari 7, 2017) alipokutana na viongozi wa wilaya hizo Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutafua njia za kuondoa msongamano huo.
Amesema kwa sasa hakuna namna ambayo wataweza kuondoa msongamano huo zaidi ya kuhamishia kituo cha mabasi ya mikoa ya kusini wilayani Mkuranga.
Waziri Mkuu amesema eneo la Mbagala kwa sasa lina msongamano mkubwa ambao ni lazima Serikali ichukue hatua za haraka za kuuondoa.
“Ikiwezekana mabasi ya mikoa ya kusini yaishie Mkuranga, hivyo kirikianeni kutafuta eneo la kujenga kituo kikubwa cha kisasa cha mabasi,” amesema.
Amesema kituo hicho watakachokijenga kiwe na uwezo wa kuhudumia mabasi yote yatokayo mikoa ya kusini na kituo cha Mbagala kiwe cha daladala za kawaida.
Pia Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa kituo hicho kutawezesha kuongeza mapato ya Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga.
Aidha Waziri Mkuu amewataka viongozi hao kwenda kujadiliana katika vikao vya mabaraza ya Madiwani juu ya mkakati huo na kisha kumpelekea taarifa ifikapo Februari 15 mwaka huu.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Bw. Filberto Sanga amesema wazo hilo ni zuri na wilaya yake ina maeneo ya kutosha kujenga miundombinu hiyo.
“Ni kweli wilaya ya Temeke imeelemewa kwa maana ya maeneo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maendeleo na haina pa kupumulia zaidi ya Mkuranga , hivyo tupo tayari kushirikiana nao,” amesema.
Wakati huo huo, Bw. Sanga ameiomba Serikali itakapoanza awamu ya tatu ya ujenzi wa mradi wa mabasi ya mwendo kasi ufike hadi Mkuranga mjini badala ya kuishia Vikindu.
Amesema kwa sasa wilaya yake ina viwanda 67 ambavyo kati yake vipo vinavyofanya kazi na vingine vikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi, hivyo mabasi hayo yatarahisisha usafiri kwa wafanyakazi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bw. Felix Lyaniva amesema amefurahishwa sana na mawazo hayo ya kuhamisha kituo cha mabasi cha Mbagala kwani katika vitu vilivyokuwa vinamnyima usingizi ni pamoja na msoingamano wa mabasi na wafanyabiashara wadogo wadogo katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment