ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 22, 2017

MASAUNI AWATAKA WANANCHI KUSHIRIKIANA NA POLISI KUWAFICHUA WAHALIFU KIBITI, MKURANGA NA RUFIJI MKOANI PWANI

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto) akizungumza na mamia ya Wananchi wa Kijiji cha Bungu, Wilaya ya Kibiti, mkoani Pwani. Masauni alifanya ziara katika Wilaya hiyo kwa lengo kuangalia hali ya usalama wa Wilaya ya Rufiji, Kibiti na Mkuranga ambapo alizungumza na askari polisi wanaolinda usalama katika maeneo hayo na baadaye alizungumza na wananchi na kuwaomba kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi bila woga ili waweze kuwasambaratisha wahalifu katika maeneo hayo. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (wapili kulia) akimsikiliza Mkazi wa Kijiji cha Bungu, Wilaya ya Kibiti, mkoani Pwani, Ayubu Mketo alipokuwa anamuuliza swali kuhusiana na hali ya usalama katika eneo lao la Bungu. Hata hivyo, Masauni aliwahakikishia usalama wananchi wa Wilaya hiyo pamoja na ya Rufiji na Mkuranga, kuwa askari wake wameweka kambi kwa ajili ya kupambana na wahalifu pamoja na kuwalinda wananchi wa maeneo hayo. Masauni alifanya ziara katika maeneo hayo ambapo alizungumza na polisi pamoja na wananchi kuhusu kushirikiana na Jeshi la Polisi bila woga ili Jeshi hilo liweze kupambana na wahalifu kikamilifu.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na askari Polisi wanaolinda usalama katika Wilaya ya Kibiti, Rufiji na Mkuranga ambao wameweka Kambi katika Wilaya ya Kibiti kwa lengo la kupambana na wahalifu katika Wilaya hizo. Masauni pia alizungumza na mamia ya wananchi wa Kijiji cha Bungu na kuwahakikishia usalama wao na pia aliwataka kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili waweze kuwasambaratisha wahalifu hao kwa uharaka zaidi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto), Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani (RPC), Onesmo Lyanga wakiwasili Kituo cha Polisi Bungu, Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani. Masauni alifanya ziara katika Kituo hicho na alizungumza na askari Polisi wanaolinda amani katika eneo hilo na pia alizungumza na wananchi ambapo aliwataka watoe ushirikiano kwa Jeshi hilo katika mapambano ya kuwasambaratisha wahalifu mbalimbali waliopo Wilaya ya Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani humo.

Na Felix Mwagara/MOHA
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amewataka wananchi wa Wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani kuwapa taarifa za matukio ya uhalifu Jeshi la Polisi bila woga wowote ili Jeshi hilo liweze kuwasambaratisha wahalifu katika maeneo hayo.

Masauni alisema Jeshi hilo ili liweze kufanikiwa katika mapambano yake na wahalifu katika maeneo hilo, nguvu ya wananchi inahitajika sana katika utoaji wa taarifa ya matukio hayo.


Akizungumza na mamia ya wananchi wa Kijiji cha Bungu wilayani Kibiti, Masauni alisema Jeshi lake limejipanga kikamilifu kwa kupambana na wahalifu na litahakikisha wahalifu hao wanakamatwa wote ili wakazi wa maeneo hayo kuendelea kufanya shughuli zao za kuijenga nchi kama kawaida bila wasiwasi wowote.

Aliongeza kuwa, ili jeshi hilo lifanikiwe zaidi katika mapambano hayo linahitaji msaada wa kupata taarifa ya wahalifu hao kwa kuwa baadhi ya wananchi wanawajua wahalifu hao lakini wanaogopa kutoa taarifa kwa polisi wakiwa na wasiwasi wa kuja kuvamiwa endapo ikijulikana.

Masauni aliwahakikishia usalama endapo watatoa ushirikiano kwa Jeshi hilo kwani umakini utakuwepo na hakuna mwalifu atakaye jua kuwa Jeshi hilo limepewa taarifa zozote, kwani kitendo cha kuto kuripoti taarifa ya wahusika hao ni hatari kwa usalama wa wananchi hao kwani huwezi kujua majambazi hayo yanaweza yakaja siku yoyote kuwavamia wananchi hata kama hawakuhusika kutoa taarifa zozote hivyo njia ya busara kushirikiana na polisi ili Jeshi hilo liweze kufanya kazi yake ya kupambana nao na kuleta usalama zaidi.

“Nchi yetu ni ya amani, na Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kuleta maendeleo kwa wananchi wake, kama mnavyoona viwanda vinajengwa, na pia mnaendelea kufanya shughuli zenu kwa amani kabisa, sasa ili amani hii iweze kudumu, mnatakiwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi pale ambapo mnakuwa na taarifa na wasiwasi na mtu yeyote katika maeneo yenu ambaye hana nia nzuri na usalama wenu,” alisema Masauni.

Alisema Jeshi la Polisi halipaswi kuogopwa na raia mwema, Jeshi hilo ni rafiki kwa kila Mtanzania mwema ambaye ana uzalendo wa dhati na nchi yake, Jeshi ni rafiki ya wananchi, hivyo wananchi wanapaswa kuwa karibu na Jeshi kwa kuwa hao ndio walinzi wa wananchi pamoja na mali zao.

Aidha, Masauni aliwataka wananchi wa maeneo hayo kufuata sheria ili waweze kuishi kwa amani na ushirikiano na endapo watafanya makosa basi jeshi hilo litawakamata wale wote watakaovunja utaratibu mzuri wa kuishi ikiwemo wale wanaoendesha bodaboda bila kofia ngumu.

“Jeshi halionei mtu, na endapo mtaonewa tafadhali nipeni taarifa kwa njia ya simu au mpigieni msaidizi wangu, na pia mnaweza mkawasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ili shida zenu, kero, malalamiko yote ambayo yapo kinyume na sheria wanayoyafanya baadhi ya polisi wetu wasiokuwa waaminifu tuyajue na kuyafanyia kazi kwa dakika chache,” alisema Masauni.

Kabla ya kufunga mkutano huo na kuendelea na ziara yake katika mikoa ya Lindi na Mtwara, Masauni alitoa namba zake za simu ya mkononi kwa wananchi hao pamoja na ya msaidizi wake, pia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani pamoja na wa Wilaya nao walitoa namba zao kwa ajili ya mawasiliano na wananchi hao.

Mwisho/-

No comments: