ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 22, 2017

Wabunge wa CUF wafikishana polisi

Waliofikishwa polisi ni Hamidu Bobali (Mchinga)
By Habel Chidawali na Haji Mtumwa, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dodoma/Z’bar. Wabunge wa CUF jana walifikishana polisi mjini hapa wakidaiwa kutishiana kwa maneno.

Waliofikishwa polisi ni Hamidu Bobali (Mchinga) na Abdallah Mtolea (Temeke) ambao walihojiwa wakidaiwa walimtishia maisha Magdalena Sakaya wa Kaliua.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema wabunge hao ambao wako mjini hapa kuhudhuria vikao vya kamati za Bunge, baada ya kutoa maelezo waliondoka.

“Tatizo lenyewe ni la Agosti mwaka jana, kwamba walimtishia maisha mbunge mwenzao Sakaya, lakini tulipowataka kituoni walikuwa nje ya mkoa ndiyo maana leo wameitwa,” alisema Mambosasa.

Katibu wa wabunge wa CUF, Juma Kombo Hamad (Wingwi) alisema hayo ni mambo ya kisiasa tu.

Kugombana kwa wabunge hao kunaelezwa kuwa ni kutokana na misimamo yao ndani ya CUF ambayo imegawanyika kambi mbili, za mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba na ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.

Mtatiro apongeza matawi ya CUF kuwatimua vigogo

Wakati wabunge hao wakipelekana polisi, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro amepongeza hatua ya matawi ya chama hicho yaliyowavua uanachama baadhi ya vigogo wake.

Mtatiro alisema hayo jana walipokuwa akizungumza na wanahabari kutoa maazimio ya Baraza Kuu la Uongozi liliofanyika juzi katika ofisi za chama hicho Vuga mjini hapa.

Alisema chama hakiangalii cheo cha mtu au ukaribu wake na watu, bali masilahi ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Alisema kikao hicho kilikubaliana na matawi hayo yaliyoamua kuwafukuza wanachama ambao walionekana kwenda kinyume na taratibu.

Alisema kitendo hicho ni cha kupongezwa kwani baada ya kuona kasoro ziliopo, walizifanyia kazi kwa masilahi ya wengi.

“Nalisema hili kwa uwazi, hatuwezi kumvumilia mwanachama akifanya anavyotaka..., hata awe katibu mkuu Maalim Seif Sharif Hamad, tutamchukulia hatua kali ikiwamo kumvua uanachama kama walivyofanyiwa baadhi ya wanachama.”

Aliwataja baadhi ya wanachama waliovuliwa uanachama na baraza na kukubaliana na uamuzi huo kuwa ni Mohamed Habib Mnyaa kutoka (Mkanyageni), Haroub Shamis (Chachechake), Mussa Haji Kombo (Miembeni Chakechake), Khalifa Suleiman Khalifa (Gando), Nassor Seif Amour (Mtambile) pamoja na Rukia Kassim Ahmed (Wawi) yote yakiwa majimbo ya Pemba na Thiney Juma Mohamed wa Kidato – Unguja.

Maalim Seif

Akizungumza katika mkutano huo, Maalim Seif aliwaambia Wazanzibari kuwa hivi karibuni watasherekea matunda ya kura zao walizopiga katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 hivyo wasikubali kuchokozwa au kujiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa amani, badala yake wawe wastaarabu na kusubiri sherehe ya kupatikana kwa haki yao.

Maalim Seif amekuwa akitoa kauli hiyo mara kwa mara na ambayo imekuwa ikijibiwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwamba uchaguzi umepita na hakuna nchi wala taasisi yoyote inayoweza kuyabadili.

No comments: