Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Mbeya Upande wa Serikali za Mitaa, Costantine Mushi
MOJA ya matendo ya unyanyasaji wa kijinsia unaoendelezwa na baadhi ya watu mkoani Mbeya ni wanawake na watoto wa kike kuwa wa mwisho kupata chakula wakati wa mlo; Imefahamika.
Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Mbeya Upande wa Serikali za Mitaa, Costantine Mushi alibainisha hayo wakati akifungua Semina ya siku tatu ya Mafunzo ya Haki za Binadamu na Unyanyasaji wa Kijinsia kwa Wasimamizi wa Sheria wakiwemo mahakimu mkoani Mbeya.
Semina hiyo iliandaliwa na Chama cha Majaji Wanawake (TAWJA) kwa ufadhili wa Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa.
Alisema, “Inasikitisha kuona katika dunia ya leo, mama na watoto wake wa kike wanakula mwishoni baada ya baba na watoto wa kiume wote kula chakula,” alisema Mushi.
Akaongeza, “Ni kama vile kundi hili wanakula makombo ya chakula walichokula wanaume kwenye familia zao. Chakula kinapaswa kiwekwe mezani na watu wote wajumuike kula kwa pamoja.”
“Kama Serikali ya Mkoa tutahakikisha aina zote za ukatili zinazofanyika ndani ya jamii tunakabiliana nazo ili kuhakikisha jamii inaishi kwa ushirikiano na bila ubaguzi.”
Katika Semina hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Atuganile Ngwala alisema jamii mkoani Mbeya haina budi kujiuliza kwa nini vitendo vya ukatili na unyanyaaji wa kijinsia hususan ubakaji vinaongezeka licha ya kuwepo adhabu kali ya kifungo cha miaka isiyopungua 30 kwa wanaotiwa hatiani na kwamba, hali hiyo inapaswa kuibua mjadala mpana.
Alitaka jamii kutafakari zaidi namna ya kukomesha vitendo hivyo, badala ya kutegemea sheria pekee kutoa katazo, adhabu na fundisho.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Katarina Revocati alisema mafunzo hayo yataleta mabadiliko katika maamuzi yao kwani baadhi yao hushiriki ukatili huu bila kujua.
Revocati alisema wapo baadhi ya wasimamizi hao ambao kutokana na kulelewa na kukulia katika mifumo iliyohalalisha ukatili huo, hujikuta wakifanya maamuzi kwa kuona jambo alilofanyiwa mhusika kuwa halali na aliyekosa hapaswi kuwajibishwa.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment