Msanii Agnes Waya, maarufu Masogange anatarajiwa kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam leo wakati kesi yake ya tuhuma za kutumia dawa za kulevya inapokuja kwa kutajwa na kuangalia kama upelelezi umekamilika au la.
Masogange anatarajiwa kufikishwa mbele ya Hakimu Mkazi, Wilbard Mashauri wa mahakama hiyo, ambaye ndiye anasikiliza kesi hiyo.
Mara ya mwisho kesi hiyo ilipotajwa mahakamani hapo hakimu huyo alimpa onyo mshtakiwa huyo baada ya kuchelewa kufika katika chumba cha mahakama, hatua iliyofikiwa baada ya Wakili wa Masogange, Nictogen Itege kuieleza mahakama kuwa mteja wake yuko njiani anakuja.
Taarifa hiyo ilisababisha, Hakimu Mashauri kumuhoji kuwa mbona yeye yupo mahakamani? Akadai kuwa walipita njia tofauti ndiyo sababu ikatokea kuwa mmoja kafika mwingine bado.
Hakimu Mashauri alisema mteja wake anatakiwa afuate masharti ya dhamana na mamlaka. Hata hivyo, baada ya muda kidogo Masogange alionekana katika viwanja vya Mahakama wakati kesi yake tayari ilikuwa imeahirishwa.
Awali, akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Constantine Kakula alidai kuwa kati ya Februari 7 na 14, 2017 katika maeneo yasiyojulikana ndani ya Jiji la Dar es Salaam Masogange alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin (Diacety Imophine).
Katika shtaka la pili, Kakula alidai kuwa kati ya Februari 7 na 14, 2017 mtuhumiwa huyo alitumia dawa za kulevya aina ya Oxazepam na kwamba alifanya makosa hayo chini ya kifungu cha 18 (a) cha Sharia ya Kupambana na Dawa za Kulevya namba 5 ya mwaka 2015.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Masogange alikana na yuko nje kwa dhamana ya wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh. milioni 10.
No comments:
Post a Comment