ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 12, 2017

BALOZI SEIF AKUTANA NA MABALOZI WANAOIWAKILISHA TANZANIA NCHI ZA NJE

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Mabalozi wapya walioteuliwa hivi karibuni kuiwakilisha Tanzania katika Mataifa mbali mbali Duniani hapo Ofisini kwa Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif wa kwanza kutoka Kushoto akibadilishana mawazo na Mabalozi hao ambao wa kwanza kushoto mwa Balozi Seif  ni Balozi Dr. Abdulla Possi anayekwenda Shirikisho la Ujerumani na Balozi Sylvester Ambukile anayeelekea Nchini Afrka Kusini.

Balozi Seif wa Tatu kutoka Kulia akiwa katika Picha ya pamoja na Mabalozi Wapya wa Tanzania walioteuliwa hivi karibuni kuiwakilisha Tanzania katika Mataifa mbali mbali Duniani mara baada ya kufanya nao mazungumzo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Kulia ya Balozi Seif ni Balozi Sylvester Mabumba Comoro, Balozi Sylvester Ambukile Afrika Kusini na Balozi Omar Yussuf Mzee Algeria, na kushoto ya Balozi Seif ni Balozi Baraka Luvanda India na Balozi Dr. Abdulla Possi Shirikisho la Ujerumani. Picha na – OMPR – ZNZ.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Mabalozi wanayoiwakilisha Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mataifa rafiki Duniani wana kazi ngumu na nzito ya kuinadi Tanzania katika Nchi hizo ili ipate kuungwa mkono katika harakati za kuimarisha Uchumi wake.


Alisema yapo maeneo na sekta kadhaa ambazo zimeshajengewa miundombinu imara kama Utalii, Mawasiliano, Kilimo, Biashara na Afya zinazohitajika kupata msukumo kwa mataifa rafiki na washirika wa maendeleo katika njia ya kustawisha maisha ya Wananchi na kuongeza pato la Taifa.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Mabalozi Wapya wa Tanzania walioteuliwa hivi karibu na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kuliwakilisha Taifa kwenye Mataifa mbali mbali Duniani walipofika kuaga rasmi wakijiandaa kuelekea kwenye vituo vyao vya Kazi.

Mabalozi hao aliokutana nao Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar ni Balozi Sylvester Mabumba anayekwenda Visiwa vya Comoro, Balozi Baraka Luvanda anaelekea Nchini India, Balozi Omar Yussuf Mzee anakwenda kuanzisha Ubalozi Mpya waTanzania Nchini Algeria, Balozi Dr. Abdulla Posi anakwenda Shirikisho la Ujerumani na Balozi Sylvester Ambukile anayekwenda Nchini Afrika Kusini.

Balozi Seif Ali Iddi alisema kumalizika kwa vita Baridi Vikuu vya Pili vya Dunia ndani ya Karne ya 20 vilivyokumbwa na wimbi la Mataifa Makubwa kutaka kuendelea kutawala dhidi ya yale yaliyokuwa yakipigania Kujitawala kumeipeperusha Dunia hiyo kuelekea kwenye uchumi zaidi.

Alisema nafasi yao ya Kidiplomasia ni vyema wakaitumia katika ushiriki wao kwenye vikundi mbali mbali vya ushirikiano vinavyowapa fursa Wanadiplomasia hao kubadilishana mawazo na Taaluma ya jinsi ya kustawisha Uchumi na Maendeleo ya Mataifa yao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Mabalozi hao Wapya wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nafasi waliyoipata ambapo Rais wa Tanzania hakufanya makosa kutokana na vigezo tofauti alivyovitumia katika kuwapata kushika wadhifa huo.

Balozi Seif alitaja Nchi wanazokwenda Mabalozi hao za Shirikisho la Ujerumani, Comoro, Algeria, India, Afrika Kusini na Israel kwamba zimekuwa na uhusiano mzuri wa Kihistoria na Tanzania kiasi kwamba jukumu lao linapaswa kuzingatia udumishaji wa ushirikiano huo.

Alisema zipo nafasi za mafunzo ya Elimu ya Juu, Taaluma katika Sekta za Kilimo, Afya, Biashara na Utalii zinazopatikana katika Mataifa hayo kiasi kwamba Mabalozi hao watapaswa kuzifuatilia ili zilete tija kwa Vijana watakaopata Taaluma ya Kujenga Taifa lao.

Akitoa Shukrani kwa niaba ya Mabalozi wenzake Balozi Sylvester Luvanda anayeiwakilisha Tanzania Nchini India alisema wamethamini fursa ya uteuzi waliyopewa na Taifa na kuahidi kwamba watawajibika kwa nguvu zao zote.

Balozi Sylvester alifahamisha wazi kuwa inatia moyo na faraja kuona kwamba Nchi wanazokwenda kufanya kazi bado zina mafungamano mazuri ya ushirikiano wa Kidiplomasia na Tanzania.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

12/4/2017.


No comments: