ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, April 1, 2017

KUTOKA MEZA YA MHARIRI WA JAMII: Ney kafanikisha, ujumbe umefika

By Ndimara Tegambwage, Mwananchi

Nimekuwa nikifuatilia taarifa za msanii Emmanuel Elibariki au kwa jina la kisanii, Ney wa Mitego katika magazeti ya kila siku, redio, televisheni na kwenye mtandao

Ney alifukuliwa kitandani saa nane usiku. Akadakwa na polisi. Ni Jumapili iliyopita katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Premier Lodge mjini Turiani; mkoani Morogoro.

Ney alimalizia zile saa chache kabla ya asubuhi, katika kituo cha polisi Turiani. Bila shaka akiimba kimoyomoyo. Au akitunga na kupanga na kupangua beti. Beti za mashairi mapya; maombolezo au ukombozi.

Lakini ni woga tu. Angemwaga mtama, polisi wangejitupatupa. Majirani wangeasi usingizi; wangeasi ndoto zao; nyumba zao kubomoa kwa mboni. Mbu, chawa na papasi wangeachwa solemba!

Kwanini? Kisima kingehamia polisi. Chota! Chota sauti. Chota maudhui. Chota madoido. Siyo kitu kilekile “kaletabobo” – kilichozaa mkasa. Kingine kisuzacho. Kidondoshacho chozi la furaha la polisi. Kipozacho katikati ya meko.

Ni woga tu. Bali Ney angeimba, polisi wangetunga macho hadi kweupe: Bila kusutwa na mbu. Bila bigi-Ji kinywani. Wakavuwakavu wakilinda hohehahe na mwanafasihi.

Ni woga tu. Usingizi ungekauka. Gereza la upweke lingebomoka. Kimya cha mauti kingepasuka kwa kishindo cha radi. Mito ya machozi ya furaha ingeleta mafuriko. Na usiku ungekatika – utake usitake na Ney afikishwe Morogoro na Darisalama!

Lakini nani anajua mashtaka? Someni kwa hatua. Hawa wanadai kakosoa Serikali kupindukia. Wale wanadai amekashifu Serikali. Huyu hapa anadai kamkashifu Rais. Yule kule anadai ameandika matusi. Kila mmoja anadai, anadai…

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amenukuliwa akisema Ney “anashikiliwa kwa amri kutoka Dar es Salaam… anakabiliwa na tuhuma za kutoa wimbo unaokashifu Serikali.”

Vyombo vya habari vimenukuu ofisa wa Shirikisho la Muziki Tanzania akikandia mashairi ya Ney. Magazeti yakaandika. Redio na televisheni zikatangaza. Ululululuuu! Mtoto Ney yuko hatarini. Acha akione cha mtema kuni. Labda na cha mtema fimbo.

Kumbe hii ni fasihi tu. Wanaodai ametukana hawasemi ametukana nini, nani na wapi. Wanaodai amekashifu hawaelezi amekashifu nini, nani, wapi na vipi. Wanaomtuhumu kukosea hawataji kosa – kakosa nini, kamkosea nani na kamkosea vipi.

Uko wapi wimbo wenyewe – beti zote, maneno yote – tuyasome. Wanaotusimulia juu ya ubaya, makosa, kashifa na dharau ndani ya wimbo mbona hawatupi fursa ya kuusoma – kuuona wote ili nasi tujiamulie?

Katikati ya mafuriko ya madai na tuhuma, anaingia John Joseph Pombe Magufuli. Huyu ndiye mwenye Serikali inayodaiwa ‘kusemwa’– kusengenywa, kukejeliwa, kubeuliwa, kukashifiwa au kutukanwa. Huyu ndiye Rais wa nchi.

Nani kasema Rais hana pua – hapumui na hanusi? Nani anasema Rais hafikiri, hana ubongo? Nani anasema Rais hana macho; haoni, anasukumwa tu? Nani kasema Rais hana vionjo – hiki kitamu kile kichungu?

Nani kasema Rais hana utambuzi – hiki kizuri kile kibaya? Nani anasema Rais hana utashi; napenda hiki, sipendi kile? Nani kasema Rais hawezi kung’amua – hili lina maana hii na lile lina maana ile?

Sasa Rais kaagiza Serikali yake, ‘mwachieni Ney wa Mitego’ na wimbo wake, ‘Wapo.’ Na Ney hajahonga. Hajapiga magoti na kubembeleza. Hajatungua beti na msamiati wake.

Waziri wa Sanaa, Harrison Mwakyembe anasema Rais amesikiliza wimbo huo na ‘ameona ni njia ya wasanii kuwasilisha mambo yanayotokea katika jamii.’ Ushindi.

Magazeti, redio, televisheni na mitandao ikaanza tena: “Rais ameruhusu wimbo wa Ney.”

Ameruhusu? Kwanini aruhusu? Ni kazi yake kuruhusu? Ni kazi yake kukataza? Hapana! alichofanya kinaeleweka?

Rais amesikiliza wimbo. Ameupenda. Ameamuru Ney aachiwe. Mwakyembe amenukuliwa akisema Ney aongeze wakwepa kodi kwenye orodha ya wimbo ‘Wamo.’

Mwakyembe amenukuliwa akisema msanii aachiwe, kwa amri ya Rais na ikibidi “kesho nionane naye hapa Dodoma ili nimpe marekebisho kidogo ya kuongezea kwenye wimbo huu.”

Hapo ndipo kuna utata mpya. Msanii kafanya kazi. Katekenya jamii na watawala. Katekenya walengwa. Kafaulu kwa kiwango cha watawala kukumbuka wengine ambao wangetajwa kwenye fasihi hii. Wasingetajwa wote.

Sasa Mwakyembe anataka kurekebisha kazi ya fasihi ili aweke vitu vyake? Anataka kuunda ToT ndani ya Ney wa Mitego? Huko ndiko kutafuta kuzima nguvu ya fasihi ambayo hata Rais wake ameitambua.

Mwakyembe anataka waongeze maneno ili kumwimbia nani wakati walioimbiwa wamesikia na wamekumbuka ambao msanii hakuwataja?

Acheni wanafasihi na wenye sanaa waumbe bila kuingiliwa. Kitokacho moyoni tofauti na cha kupewa.

Mwandishi ni Mhariri wa Jamii wa vyombo vya habari vya Mwananchi Communications Limited wachapishaji wa magazeti ya The Citizen, Mwanaspoti na hili. Kwa maswali na hoja j, wasiliana naye kwa: 0713614872 au 0763670229; e-mail: ndimara@yahoo.com au ntegambwage@tz.nationmedia.com   

No comments: