ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 11, 2017

MAKAMU WA RAIS MHE. SAMIA AZINDUA KIKOSI KAZI CHA UOKOAJI WA MFUMO-IKOLOJIA WA BONDE LA MTO RUAHA MKUU

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiongoza mkutano wa uzinduzi wa kikosi kazi cha kuokoa mfumo-ikolojia wa bonde la mto Ruaha Mkuu uliofayika kwenye ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa. 
Mhe. January Makamba akithutubia juu ya umuhimu wa mto Ruaha ambao unahudumia watu zaidi ya milioni 6 na namna ambavyo umeathirika na shughuli za binadamu kwenye warsha ya uzinduzi wa kikosi kazi cha kuokoa mfumo- ikolojia wa bonde la mto Ruaha Mkuu uliofayika kwenye ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi (MB) Mhe. Wiliam Lukuvi (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe.Amina Masenza wakati wa mkutano wa uzinduzi wa kikosi kazi cha kuokoa mfumo-ikolojia wa bonde la mto Ruaha Mkuu uliofayika kwenye ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa. 
Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa Tanzania Mhandisi Gerson Lwenge akihutubia wakati wa warsha ya uzinduzi wa kikosi kazi cha kokoa mfumo -ikolojia wa bonde la mto Ruaha mkuu. 
Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe akichangia mawazo yake wakati wa warsha ya uzinduzi wa kikosi maalum cha kuokoa mfumo-ikolojia katika bionde la mto Ruaha mkuu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba wakati wa mkutano wa uzinduzi wa kikosi kazi cha kuokoa mfumo- ikolojia wa bonde la mto Ruaha Mkuu uliofayika kwenye ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Richard Kasesela akichangia mtazamo wake wakati wa uzinduzi wa kikosi kazi cha kuokoa mfumo-ikolojia wa bonde la mto Ruaha mkuu.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amezindua Kikosi Kazi Maalum kwa ajili ya kuokoa mfumo wa ikolojia katika bonde la mto Ruaha Mkuu ambalo lipo katika hatari ya kutoweka kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea kwenye bonde hilo kutokana na shughuli za Kibinadamu.

Kikosi kazi hicho ambacho kimezinduliwa mjini Iringa kitafanya kazi chini ya usimamizi wa Makatibu Tawala wa mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe kwa kuchambua kwa kina tafiti na matokeo ya tafiti hizo ili kupendekeza hatua za haraka zitakazochukuliwa katika kudhibiti uharibifu kwenye bonde hilo ambao umechangia kupungua kwa maji kwenye mto Ruaha Mkuu.

Akizindua Kikosi kazi hicho mjini Iringa ambacho ambacho kimehudhuriwa na Mawaziri kutoka Wizara Tano, Makamu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amesema ofisi yake imeamua kuunda kikosi hizo ili kuokoa hali mbaya ya uharibifu wa mazingira unaoendelea kufanyika hivi sasa katika Bonde la Mto Ruaha Mkuu.

Amesema kutokana hali kuwa tete kwenye bonde hilo ndio maana hatua ya haraka na za dharura zimechukuliwa na ofisi yake kwa kuunda kikosi kazi hicho ambacho kinaundwa na wataalamu mbalimbali wa serikali, washirika wa maendeleo ambao wana uwezo wa kufanya maamuzi ya kisera na kiutendaji ili kutoa suluhu ya kudumu ya kuhifadhi bonde hilo.

“Muda wa kusema bila kutenda umeshaisha nataka kikosi kazi hiki kifanye kazi usiku na mchana na kuleta matokeo bora na kwa muda mfupi”. Amesisitiza Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais amewataka wajumbe wa kikosi kazi hicho washirikishe wadau wote katika kufanya kazi hiyo ili kujenga dhana ya uwajibikaji katika uhifadhi wa mazingira ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu.

Amesema anaimani kubwa kuwa wajumbe wa kikosi kazi kilichoundwa na ofisi yake kitakuwa na mchango mkubwa katika kufikia azma ya serikali ya kuokoa mfumo wa ikolojia katika bonde hilo kwa kubuni mikakati kabambe na endelevu ya kukabiliana na uharibifu huo.

Makamu wa Rais alinukuu hotuba ya Papa Mtakatifu Francis Mjini Rome, Italia katika Mkutano wa Pili wa Lishe wa Duniani uliofanyika mwaka 2014 aliyesema kuwa Mungu anasamehe lakini Mazingira hayasamehi akimaanisha kuwa ni muhimu kwa wadau wote wakashiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January makamba amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa Kikosi kazi kilichoundwa kitafanya kazi kwa viwango vinavyotakiwa ili kuhakikisha mfumo wa ikolojia katika bonde la mto Ruaha Mkuu unalindwa na kutunzwa ipasavyo.

Amesema kuwa kikosi kazi hicho pia kitakuwa na jukumu la kukusanya maoni na mapendekezo ya wadau wote ikiwemo wananchi wanaoishi katika bonde hilo kuhusu namna ya kutunza bonde pamoja na kuandaa rasimu ya Mapango wa Kitaifa wa Hifadhi ya Mazingira ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu.

Aidha kikosi kazi hicho kitakuwa na mamlaka ya kuchukua hatua za moja kwa moja kwa kutumia mamlaka ya sheria mbalimbali kwa masuala ya kisekta na kuwakilisha mapendekezo kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais.

Kikao hicho cha uzinduzi wa Kikosi Kazi Maalum kwa ajili ya kuokoa mfumo wa ikolojia katika bonde la mto Ruaha Mkuu kimehudhuriwa na Mawaziri Watano ambao ni Waziri Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge, Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe.

Mawaziri wengine ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dakta Charles Tizeba, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba ambaye ameunda kikosi kazi hicho.

BOFYA HAPA KWA PICHA ZAIDI

No comments: