ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, April 8, 2017

Mdee: Niliwahi Dodoma kuepuka kukomolewa

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi ebahemu@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee amesema aliamua kuwahi Dodoma kuepuka kukomolewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai aliyeagiza afike mbele ya Kamati ya Maadili jana asubuhi na kuagiza polisi wamsake popote alipo, ikiwezekana apelekwe akiwa amefungwa pingu.

Mdee, ambaye alikuwa Dar es Salaam wakati amri hiyo ikitolewa juzi saa 5:00 asubuhi, aliwasili Dodoma jana, lakini suala lake litajadiliwa leo.

“Spika ana mamlaka ya kisheria ya kuomba vyombo vingine vya dola kumsaidia kumkamata mtu,” alisema Mdee alipoongea na Mwananchi jana.

“Kwa sababu hiyo, ana uwezo wa kutumia mamlaka hayo kumkomoa mtu. Ndiyo maana nikaja mwenyewe Dodoma. Niliacha majukumu mazito niliyokuwa nayo ili lengo lake la kunikomesha lisifanikiwe,” alisema.

Spika Ndugai, aliyezungumza kwa ukali, alisema anajua kuwa Mdee alikuwa nje ya Dodoma, lakini akataka awe amefika mbele ya kamati hiyo jana muda sawa na ule aliokuwa akitoa maagizo hayo juzi.

Mdee anatuhumiwa kutoa lugha mbaya kwa Spika, Rais na wabunge wakati wa mjadala uliokuwa mkali wa nafasi za wagombea wa Chadema na CUF katika Bunge la Afrika Mashariki.

Mdee pamoja na Kiongozi wa Kambi Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kufika watahojiwa na kamati hiyo leo.

Mdee alisema alipofika nyumbani kwake Dodoma jana asubuhi alikuta barua ya Spika inayomtaka kufika mbele ya kamati leo na si jana kama alivyotangaza kiongozi huyo wa Bunge.

“Nadhani siku imebadilishwa kwa sababu ya sikukuu ya Karume maana nilipofika nyumbani kwangu Dodoma asubuhi ya leo (jana) niliambiwa kuna barua ililetwa na maaskari wa Bunge na nilipoifungua ilikuwa inaeleza kuwa natakiwa kuhojiwa na Kamati ya Maadili kesho (leo) bila kueleza sababu ya kutohojiwa leo (jana),” alisema Mdee.

Alisema wakati anapata taarifa za kuitwa, alikuwa Dar es Salaam kwa ajili ya kesi ya uchaguzi wa Meya wa Ilala ya mwaka jana. Pia, alitaka kumjulia hali Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Aida Khenani aliyepata ajali ya pikipiki juzi mjini Dodoma, na kupokea mwili wa mbunge mwingine wa viti maalumu wa chama hicho, Dk Elly Macha ambao unatarajiwa kuwasili leo.

Kuhusu hali ya Aida

Kuhusu hali ya Aida, Mdee alisema aliruhusiwa kutoka hospitali baada ya madaktari kujiridhisha kuwa hakupata madhara makubwa katika ajali hiyo.

“Kwa sababu alikuwa amevimba katika baadhi ya sehemu ya kichwa, madaktari walimfanyia uchunguzi na kusema kuwa ni uvimbe wa kawaida. Pia tulihisi amepata madhara katika taya lake, lakini madaktari wamesema meno hayajalegea sana,” alisema Mdee.

“Alipewa dawa za kumsaidia kurejea katika hali yake ya kawaida na kutakiwa kuripoti tena baada ya wiki mbili kwa ajili ya uchunguzi na kuona maendeleo yake.”

No comments: