Dar es Salaam. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo, ambaye aliwahi kumtaka Rais John Magufuli kuacha kuondoa wasomi na kuwapa madaraka, ameteuliwa kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, uteuzi aliouelezea kuwa ni heshima lakini wa “mshtuko, mshtuko, mshtuko”.
Wakati Profesa Kitila akikabiliana na msimamo wake, Rais Magufuli amebadili ahadi yake aliyoitoa Zanzibar aliposema kuwa kiongozi wa upinzani hatatia mguu ndani ya Serikali yake.
Mambo hayo mawili yametokea baada ya Rais kufanya mabadiliko madogo katika safu ya makatibu wakuu.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais imeeleza kuwa Profesa Kitila anaenda kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Mhandisi Mbogo Futakamba ambaye amestaafu.
“Ni shock, shock, shock (mshtuko), sikutegemea na nashindwa hata kukuelezea Matandiko (mwandishi). Ni heshima kubwa sana aliyonipa Rais,” alisema Profesa Kitila, ambaye ni muasisi na mshauri wa ACT Wazalendo, nafasi ambayo alijiuzulu jana jioni.
Profesa Kitila hakuwa na taarifa ya uteuzi wake hadi alipopigiwa simu na Mwananchi.
“Nimerudi jana kutokea Dodoma kwenye uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki pamoja na masuala ya Wizara ya Elimu. Hivi tunavyozungumza niko hapa na mabegi yangu nimetoka nyumbani asubuhi hii nilikuwa najiandaa kuingia katika kipindi hapa chuoni kufundisha,” alisema.
“Haya mambo ni mazito sana nakosa hata namna ya kuelezea.”
Mhadhiri huyo amesema hakutegemea na amepatwa na mshtuko baada ya kupata taarifa ya uteuzi huo.
Profesa Kitila amesema ni heshima kubwa na asiyoweza kuielezea kwa sasa kutokana na imani kubwa aliyoionyesha Rais Magufuli kumuingiza katika safu ya makatibu wake wakuu.
Profesa Kitila aliwahi kunukuliwa akisema kuwa Rais amekuwa akiondoa wahadhiri vyuoni na kuwapa madaraka ya kisiasa na kuviacha vyuo vikipukutisha wasomi.
Alisema vyuo vilivyoathirika sana na uteuzi wa Rais Magufuli ni UDSM na Chuo Kikuu cha Dodoma na kumtaka Rais awaache wasomi waendelee kufanya kazi zao, hasa za utafiti ili wasaidie wanafunzi.
Akizungumzia uteuzi huo, kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamepokea kwa mikono miwili taarifa ya uteuzi huo, akisema umeonyesha Rais amebaini kuwa vyama vya upinzani vina uwezo, weledi na uzalendo wa kutumikia nchi.
Alisema ameridhia uteuzi huo baada ya kushauriana na viongozi wakuu wenzake wa chama hicho.
Alisema wamejiuliza mambo mengi, lakini wameamua kumruhusu kwenda kutumikia nafasi hiyo kwa sababu Profesa Kitila alikuwa mtumishi wa umma na kuteuliwa kwake kushika nafasi hiyo ni sawa na kupandishwa cheo kwenye utumishi wa umma
“Wengine waliona kama jambo hili lingetunyong’onyesha kama chama ama ni kufutwa kwa machozi baada ya kukataliwa na kanuni za Bunge kushiriki (uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mashariki), lakini tukaona hatuwezi kuwanyima Watanzania mtu mwenye weledi kuwatumikia,” alisema Zitto.
Kwa upande mwingine, Rais amebadili kauli yake kuwa hatateua wapinzani kuingia kwenye Serikali yake.
Akiwa kisiwani Unguja, Magufuli alimshangaa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwa kuteua wanasiasa wa vyama vya upinzani kwenye Serikali yake wakati alipata ushindi mkubwa.
“Sijawahi kuona, makamu mwenyekiti wa Tadea amezungumza hapa, rais uchaguliwe, upate asilimia 92, bado unachukua watu wa vyama vingine unawaingiza kwenye Serikali yako,” alisema Rais Magufuli kwenye mkutano wa hadhara.
“Mimi nilipata asilimia 58, hakuna wa chama kingine mle ndani yangu. Na wala hataingia.
“Mimi nimepata asilimia 58 hakuna atakayekanyaga mguu kwenye Serikali yangu.”
Profesa Kitila ni mtu wa pili kutoka vyama vya upinzani kuteuliwa na Rais baada ya mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Parole.
Kada mwingine wa ACT Wazalendo, Hidaya Usanga aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa mkurugenzi wa Wilaya ya Tarime. Lakini wakati akisubiri kula kiapo Ikulu, Usanga, ambaye katika uchaguzi uliopita aligombea ubunge wa Jimbo la Malinyi kwa tiketi ya ACT Wazalendo, aliitwa pembeni na kutakiwa aondoke.
Uteuzi wa Profesa Kitila umeibua mjadala katika mitandao ya kijamii, huku wasomi wakitoa maoni tofauti.
Wasomi waelezea uteuzi wake
Akizungumza na gazeti hili, Richard Mbunda kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora ya UDSM, alisema Profesa Kitila alijipambanua kushiriki katika siasa na uwezo wake ndiyo imekuwa kigezo klichomshawishi Rais kumchukua.
“Kitila amekuwa na hali ya kuleta mabadiliko kwa muda mrefu akiwa nje ya mfumo. Sasa amepata nafasi ya kuinga ndani ya mfumo. Kwa uteuzi huu ninampa credit Rais Magufuli,” alisema Mbunda.
“Hajaangalia tofauti ya kiitikadi ila ameangalia uwezo wake. Wapo wana-CCM wengi angeweza kuwateua ila ameona Kitila anamfaa zaidi.”
Msomi mwingine, Profesa Abdallah Safari, ambaye ni makamu mwenyekiti wa Chadema, alisema baada ya kupata taarifa za uteuzi alishtuka kwa sababu si kawaida kwa siasa za Afrika. Alisema tukio hilo limeingia katika historia ya Tanzania na Afrika.
“Nimeshtuka, nimeshtuka sana kwa sababu nchi za Kiafrika hazifanyi kazi na upinzani. Mimi nilifukuzwa serikalini nikiwa mkurugenzi wa Mipango na Mafunzo wa Chuo cha Diplomasia mwaka 2000 baada ya kuonekana nimempa lifti (mwenyekiti wa CUF) Profesa Lipumba katika gari langu la kazini. Sasa uteuzi wa aina hii lazima ushtuke,” alisema.
Alisema uteuzi kama huo umezoeleka katika nchi za Ulaya na Amerika na si barani Afrika hivyo haamini kilichotokea.
“Aliyewahi kuwa rais wa Marekani Bill Clinton alimteua mpinzani kutoka chama cha Republican kuwa Waziri wa Ulinzi, ni kawaida kwao. Sasa tunajiuliza kweli Kitila alikuwa mpinzani, what is a motive behind (kuna nini nyuma yake). Kama kuna nia njema basi fine (safi),” alisema.
Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti wa taasisi ya Repoa, Dk Abel Kinyondo alisema athari kwa upande wa Rais Magufuli inaweza kujitokeza katika utendaji.
Alisema kuna tofauti ya uwezo wa kufundisha darasani na uwezo wa kufanya kazi ofisini, hivyo ipo hatari ya wateule wake wapya kutumia muda mwingi kupata uzoefu wa kazi.
Mtafiti huyo alisema tatizo jingine linaloweza kujitokeza ni kuibuka kwa migomo baridi kutoka kwa wafanyakazi wa ndani ya taasisi kwa kuwa mteule ametoka nje ya mfumo.
“Hii ina athari. Kuna watendaji wengine ndani mfumo wana uwezo, uzoefu na elimu lakini inawakatisha tama kwa kuwa hawapandishwi vyeo badala yake anateuliwa mtu mwingine wa nje, ni muhimu kulitazama hilo,”alisema.
Profesa Kitila alikuwa mwanachama wa Chadema, lakini alivuliwa uanachama na Kamati Kuu kwa kudaiwa alikuwa akipanga njama za kukihujumu chama hicho.
Mwaka 2015, Profesa Kitila aliteuliwa na ACT Wazalendo kugombea urais, lakini alikataa. Hata hivyo Profesa Kitila alishiriki kufanya kampeni ya kumtangaza Anna Mghwira aliyeteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho.
No comments:
Post a Comment