Mbunge huyo alitoa ombi hilo bungeni alipopewa nafasi na Spika Job Ndugai kuuuliza swali la nyongeza.
Katika maelezo ya utangulizi ya swali lake, Nape alisema utaratibu wa kuweka alama ya X kwenye nyumba umezagaa nchi nzima na unaathiri maendeleo ya wananchi.
Alisema utaratibu huo unazuia wananchi kuendeleza maeneo yao na inachukua muda mrefu kwa serikali kuanza kutekeleza mipango yao.
“Je, serikali haioni sasa umefika wakati wa kubadilisha utaratibu huu... wawe wanapanga mipango yao, wakikamilisha ndiyo waende kuzungumza na wananchi kwenye maeneo husika na kuweka alama hizo. “Mfano mzuri ni kwenye maeneo ya Jimbo langu la Mtama ambapo inasemekana kuwa utapita mradi wa reli na nyumba zimewekwa alama ya X kwa muda mrefu.
Kama serikali itakubaliana na mpango huu itoe tamko hapa ili niwaambie wananchi wangu wapake chokaa zile alama za X ili waendelee na shughuli nyingine,” alisema.
Katika majibu yake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani alisema serikali itaendelea kuziwekea alama za X nyumba zote ambazo zimejengwa ndani ya hifadhi za barabara.
Katika swali la msingi la Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (CCM) alitaka kujua ni wananchi wangapi wa Wilaya ya Kakonko kati ya hao wenye alama ya X wanaokidhi vigezo vya kulipwa na sababu ni zipi kwa wasiolipwa.
Ngonyani alisema alama ya X ziliwekwa ili kubainisha wananchi waliojenga ndani ya hifadhi ya barabara ambayo ina upana wa mita 30 kutoka katikati ya barabara kila upande.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment