Advertisements

Wednesday, April 26, 2017

SII MARA YA KWANZA KWA MGONJWA KUJIRUSHA GHOROFANI MUHIMBILI

By Herieth Makwetta, Mwananchi hmakweta@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katika hali isiyokuwa ya kawaida mgonjwa mmoja aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alijirusha kutoka ghorofani jana asubuhi na kujeruhiwa kichwani.

Tukio kama hilo liliwahi kutokea mwaka 2012, katika wodi hiyo hiyo na dirisha hilo hilo.

Mgonjwa huyo (jina linahifadhiwa) alikuwa amelazwa wodi 6 katika jengo la Mwaisela.

Shuhuda wa tukio hilo Juma Omary alisema mgonjwa huyo alikuwa akiweweseka, kabla ya kuamka kitandani na kuanza kukimbia.

“Kilichoonekana ni kama alikuwa anaota na baadaye aliamka na kuanza kukimbia kama anafukuzwa, kabla ya kulifikia dirisha na kisha kutoka nje nafikiri alidhani ni mlango," alisema Omary.

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano kwa Umma wa MNH, Aminiel Aligaesha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba hali ya mgonjwa ni nzuri na kwamba anaendelea na matibabu.

Aligaesha hakutaka kutoa taarifa za kina za mgonjwa huyo zaidi ya kueleza kuwa ni mwanaume, mwenye miaka 25 na kuwa alifikishwa Muhimbili juzi kwa rufaa akitokea katika Hospitali ya Amana.

"Mgonjwa wetu alikuwa akiendelea na matibabu chini ya jopo na madaktari, lakini leo asubuhi wakati wagonjwa wamelala na muda wa madaktari kupita wodini, mgonjwa aliamka ghafla na kuanza kukimbia," alisema.

Aligaesha alifafanua kuwa mgonjwa huyo aliparamia dirisha akidhani mlango na kuanguka chini na kitendo hicho kilimsababishia kupata jeraha upande wa kulia wa kichwa chake.

Alisema mgonjwa aliwahishwa katika kitengo cha huduma za dharura na baada ya kuangaliwa na madaktari na kuonekana na jeraha lililosafisha na kuwekwa dawa.

"Jeraha alilolipata si kubwa na halikuwa la kushona, jopo la madaktari linamwangalia mgonjwa huyu kwa ukaribu zaidi na tayari limeshamwandikia kipimo cha CT Scan,” alisema na kuongeza:

“Kwa sasa anasubiri kipimo hicho ili kujua amedhurika kwa kiasi gani dhidi ya ajali hiyo sababu alidondokea kichwa.”

Alipoulizwa kuhusu tatizo lililokuwa likimsumbua mgonjwa, historia ya ugonjwa wake na kutaka mazungumzo naye, Mkuu huyo wa kitengo alisema hiyo ni siri ya mgonjwa na haipaswi kuweka hadharani.

"Ieleweke kwamba hii ni ajali kama zilivyo nyingine na wala si kwamba mgonjwa huyo ana matatizo ya akili kwa maana wagonjwa wa akili wana wodi zao na miundombinu yao ipo tofauti sana, suala hili halihusiani kabisa na matatizo hayo," alisema.

Hata hivyo Aligaesha alisema katika uchunguzi wa awali uliofanywa na madaktari kuhusu mgonjwa huyo imebanika kuwa alihisi alikuwa akifukuzwa na watu.

“Inavyooenakana ni kama alikuwa anataka kujiokoa na alijikuta akilivamia dirisha hilo akidhani ni mlango,” alisema Mwaka 2012 ajali inayofanana na hiyo iliwahi kutokea katika wodi hiyohiyo jengo la Mwaisela ghorofa ya kwanza.

Ajali hiyo ilitokea katika wodi hiyo hiyo, dirisha hilo hilo na katika jengo la Mwaisela ghorofa ya kwanza.

Kisa cha Chameleone

Tukio kama hilo liliwahi kumtokea Mwanamziki nyota wa Uganda Jose Chameleone ambaye alijikuta ameanguka kutoka ghorofani hadi chini ilhali alikuwa amelala katika hoteli ya Impala jijini Arusha Oktoba 2008.

Mwanamuziki huyo amabaye alikuwa nchini kikazi alidondoka kwa kupitia dirishani asubuhi, muda mchache baada ya kumaliza kutoa burudani katika onyesho mjini humo.

Mwenyewe alisema alikuwa anaota na si kwamba alijirusha akiwa timamu.

Mmoja wa wataalamu waliokuwa waliokuwa wakimtibu mwimbaji huyo alisema tukio hilo lilisababishwa na Chameleone kutembea akiwa usingizini.(Sleep walking)

“Chameleone aliinuka akiwa kwenye ndoto usingizini na kutoka kupitia dirishani la kioo na alikuwa pekee yake kwenye chumba ambacho kimefungwa. Ugonjwa wa kutembea ukiwa usingizini mara nyingi unatokana na wasiwasi, kuchanganyikiwa akili, matokeo ya matumizi ya dawa, ulevi au kutokana na matibabu,” alisema.

Mwanasaikolojia.

Mwalimu wa Saikolojia katika chuo cha Ualimu cha Patandi Tanga, Modesta Kimonga alisema sauala hili ni la kawaida kwa binadamu na sio kama watu wanavyoamini kuwa linasababishwa na nguvu za giza.

“Kwa hali ya kawaida binadamu anakuwa na vitu anavyovifikiria muda wote na anapopata usingizi vinaweza vikamjia ndotoni hivyo anaweza akaviwaza akiwa usingizini, akavizungumza na wakati mwingine akatenda, hivyo huenda ndivyo ilivyokuwa kwa mtu huyo,”alisema Kimonga.

Hata hivyo wanasaikolojia wameeleza sababu za watu wanaojirusha ghorofani kwa kutaka kujiua kuwa ni kukosa suluhisho na kukosa thamani ya maisha yake.

Mwanasaikolojia kutoka Taasisi ya Christom Solution, Charles Nduku alisema:

“Ukibahatika kumuokoa ukimuuliza vizuri sababu ya kujiua, utagundua kuwa alikosa mapenzi (watu wa kumwambia kuwa wanampenda.”

No comments: