ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 12, 2017

BWAWA LA MAJI KUNUFAISHA WANANCHI ZAIDI YA 24,000 SIKONGE

Bwawa la maji Igumila lililoko wilayani Sikonge Mkoani Tabora litakalohudumia wananchi zaidi ya 26,000 wa kata za Kiloli na Kitunda wilayani humo kwa maji ya kunywa, kunyweshea mifugo na uvunaji samaki
(Picha na Allan Kitwe)

Na Mussa mbeho, Sikonge

WAKAZI zaidi ya 24,000 wa vijiji 6 vilivyoko katika kata za Kiloli na Kitunda wilayani Sikonge Mkoani Tabora wanatarajia kunufaika na mradi wa maji wa Bwawa la Igumila unaoendelea kujengwa katika maeneo hayo.

Wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea mradi huo hivi karibuni, wakazi wa kata hizo walielezea kufurahishwa kwao na ujio wa mradi huo unaotekelezwa kupitia Mpango wa Serikali wa Maendeleo ya maji vijijini (WSDP) kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.

Stanley Stefano mkazi wa kijiji cha Mwenge alisema ujio wa mradi huo ni faraja kwao kwani utasaidia kukuza uchumi wao hasa ikizingatiwa kuwa maji ya bwawa hilo yatatumika kwa ajili ya kunywa, kunyweshea mifugo na ufugaji samaki.

Alisema kupitia mradi huo mifugo yao haitakufa tena kwani wamejengewa birika kubwa la kunyweshea mifugo kwa kutumia bwawa hilo na samaki wapatao 380 aina ya sato tayari wamepandikizwa katika bwawa hilo kwa ajili ya uvunaji.

Mjumbe wa serikali ya kijiji cha Mgambo Jackson Ernest alisema mradi huo ni neema kubwa sana kwao kwa sababu hawatakuwa na shida ya maji ya kunywa kama zamani kwani walikuwa wakichota maji ya visima yasiyo salama.

Alifafanua kuwa bwawa hilo litawawezesha kuongeza kipato chao kupitia mifugo na uvuvi wa samaki, aidha aliomba maji hayo yasambazwe karibu zaidi na wananchi na katika taasisi za umma ikiwemo Kituo cha Afya Kitunda, misheni na msikitini ili kuwaondolea usumbufu.

Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Kapumpa Mtelya Mgwagu alisema bwawa hilo ni mkombozi kwa wananchi wake kwani maisha yao yalikuwa hatarini kutokana na kutumia maji ya visima yasiyokuwa safi na salama, aidha samaki waliopandikizwa katika bwawa hilo alisema ni kichocheo
kikubwa kwa uchumi.

Alimpongeza Mhandisi wa Maji wilaya ya Sikonge Pascal Ngunda kwa kusimamia vizuri mradi huo na kuomba mkandarasi aliyepewa kazi hiyo aongeze kasi na amalize kwa wakati ili waanze kuyatumia.

Mhandisi Pascal Ngunda alisema bwawa hilo lenye ukubwa wa mita za ujazo milioni 1.1 na kina cha mita 5, kwa awamu ya kwanza liligharimu zaidi ya sh milioni 700 na kwa awamu hii limegharimu zaidi ya sh mil.650 zilizotolewa na Benki ya Dunia.

Msimamizi wa Mradi huo Mhandisi Mkata Temsi kutoka Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Magharibi alisema mradi huo umefikia hatua nzuri kwani ujenzi wa tuta na njia za kutolea maji vimeshakamilika na sasa wanatengeneza tanki la kupozea na mfereji wa kuongezea maji.

Alisema baada ya zoezi hilo kitakachofuata ni zoezi la usambazaji maji kwa wananchi ambalo linatarajiwa kuanza mwezi wa Agosti mwaka huu au kabla ya hapo.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Simon Ngatunga aliwataka wananchi walioko karibu na mradi huo kujiepusha na vitendo vya uharibifu mazingira ili kutoathiri bwawa hilo huku akionya kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa watakaokaidi agizo hilo.

Diwani wa kata ya Kiloli Winston Hamsin alitaja vijiji vitakavyonufaika na mradi huo kuwa ni Kapumpa, Mgambo, Mwenge na Mkola katika kata ya Kitunda na vijiji vya Majojoro na Mwitikio vilivyoko katika kata yake ya Kiloli.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Mwalimu Peter Nzalalila alisema serikali imewaletea mradi huo ili uwainue kiuchumi hivyo akaonya mtu yeyote atakayejaribu kuharaibu miundombinu ya mradi huo.

No comments: