Msafara wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi” kulia mtu wa nne aliyafaa sare za CCM fulana na kofia za kijani huko shehia ya Koani Wilaya ya Kati Unguja.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi” akizungumza na mmoja kati ya wananchi waliopata maafa ya mvua zinazoendelea kunyesha, Bw. Kassim Vuai huko Shehia ya Kizimbani Wilaya ya Magharib “ A” Unguja.
Mwananchi wa shehia ya Miwani iliyopata athari ya kuharibika kwa miundombinu ya barabara Bw. Mohamed Sheweji Mohamed ambaye pia ni miongoni mwa waasisi wa ASP akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi” katika ziara hiyo ya kuwafariji wananchi.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar , akiingia ndani ya nyumba ya mkaazi wa shehia ya miwani Bi. Christina John kumfariji juu ya maafa hayo.
Bw. Edward Maziku mmoja kati ya wananchi waliopata maafa hayo ambaye nyumba yake imepotomoka kutokana na mvua hizo kama inavyoonekana pichani na Dr. Mabodi alimpa msaada wa sh.200,000 ili aweze kujikimu huku CCM na SMZ zikitafuta wa changamoto hizo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi” akiangalia ukuta uliobomoka kwa mvua wa vyoo vya Skuli ya msingi na sekondari Bwejuu na kuchangia sh.200,000 na gari moja la mawe ili ukuta huo ujengwe haraka ili shule ikifunguliwa wanafunzi wapate huduma ya vyoo.
Ni baadhi ya nyumba za shehia ya Chwaka zilizojaa maji kutokana na mvua hizo.
PICHA NA AFISI KUU CCM ZANZIBAR.
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema kinaendekea na juhudi za kuishauri serikali iharakishe utaratibu wa kutoa misaada kwa wananchi walioathiriwa na maafa ya mvua ili waweze kupata huduma za msingi kama walivyo wananchi wengine waliosalimika na tatizo hilo.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Mkuu wa Chama hicho Zanzibar, Dkt.Abdalla Juma Saadala '' Mabodi" katika mwendelezo wa ziara yake ya kukagua maeneo mbali mbali nchini yaliyopata maafa ya mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Dkt.Mabodi aliwambia wananchi hao kwamba serikali ya Mapinduzi ya zanzibar inayotokana na chama hicho ni sikivu na inathamini maisha na utu wa wananchi wote bila ya kujali itikadi za kisiasa, hivyo itaendelea kutoa mapendekezo kwa Idara ya Maafa nchini ifike kila pembe ya visiwa vya zanzibar kuhakikisha wananchi wote waliopata maafa wanaratibiwa na kupatiwa misaada.
Alieleza kwamba pamoja na taasisi hiyo kufanya kazi za kisiasa bado ina jukumu la kuwalinda na kuwasaidia wananchi wakati panapotokea majanga mbali mbali ya kitaifa ili waweze kubaki salama na kuendelea na shughuli za kimaendeo.
" Wananchi tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu atuvushe salama katika hii neema ya mvua iliyochanganyika na mitihani, ili turudi katika maisha ya kawaida na kuondokana na hofu.
Jukumu letu kama chama cha kisiasa wakati wa maafa ni kuhakikisha kila mwananchi ana kuwa salama na kupata huduma za msingi sambamba na kuwafariji huku serikali ikiendelea kukamilisha taratibu za kutafuta ufumbuzi wa kumaliza changamoto zinazotokana na maafa hayo." alieleza Dkt. Mabodi wakati akitoa msaada wa fedha sh.200,000 kwa mwananchi wa Shehia ya Miwani Unguja, Bw.Endward Maziku ambaye nyumba yake imebomoa na kukosa makaazi ya kuishi.
Akitoa ufafanuzi kwa wananchi wa maeneo ya shehia ya Miwani kuwa changamoto ya miundo mbinu ya barabara inayowakabili , alisema SMZ ina mpango wa kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa awamu pamoja na Vijiji vya Koani, Jendele, Unguja Ukuu na Jumbi.
Alifafanua kuwa baadhi ya barabara hizo tayari zilikuwa zimeanza kutengenezwa lakini baadae serikali ikabaini kuwa Mkandarasi aliyepewa tenda hiyo hana sifa na ikaamua kumfuta.
Sambamba na hayo Naibu Katibu Mkuu huyo, aliendelea kuwasisitiza waakazi wa maeneo mbali mbali kutibu maji kabla ya kuyatumia pamoja na kuwa karibu na watoto wadogo wasicheze karibu na mabwawa ya maji ya mvua kwa lengo la kuepuka athari za maafa.
" Nakiri kwamba mvua hizi ni kubwa sana hazijawahi kutokea kwa miaka ya hivi karibu, kwani mvua kama hizi nakumbuka zilitokea miaka ya 1972-1973 na kuacha maafa makubwa.
Pia nawaomba wanasiasa nchini tusitumie maafa haya kama ajenda ya kisiasa bali tuwafariji na kutoa nasaha za kuwashauri mambo mema na kuwaeleza hali halisi kwani SMZ na CCM hazipendi wananchi wapate majanga na migogoro, hivyo mitihani hiyo ni majaaliwa ya Mwenyezi Mungu".alifafanua Naibu Katibu Mkuu huyo.
Mapema wananchi hao kwa nyakati tofauti walisifu kasi ya usimamizi wa Ilani ya CCM inayotekelezwa na Serikali kwa kuimarisha huduma za msingi katika sekta mbali mbali za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza Mkaazi wa Chwaka Wilaya ya Kati alisema licha ya kuwepo kwa changamoto za maafa zilizoharibu miundombinu ya maji, barabara na umeme lakini bado wana matumaini kwa serikali itafanya marekebisho ya haraka kwa baadhi ya huduma ili zilidi katika hali ya kawaida.
Naye Mkaazi wa Jambiani Kikadini, Ramadhan Kassim, aliwaomba wananchi wa maeneo mbali mbali nchini kuwa na utamaduni wa kuwa na tahadhari ya kujipanga mapema kwa kufuata ujenzi unaozingatia ushauri wa kitaalamu ili kuepuka maafa wakati wa mvua zijazo.
No comments:
Post a Comment