Enzi za mababu zetu, masuala kama hayo, yalikuwa hayana haja, kwani kulikuwa na utamaduni wa watu kuchaguliwa wenza wao wa maisha ambao baadaye hujikuta wakipendana na kuanzisha familia kutokana na mazoea.
Hata hivyo, hali kwa sasa ni tofauti sana na zamani, kwani wengi wetu hujichagulia wenza wetu wa kuwa na uhusiano nao ikiwa ni pamoja na kuanzisha nao familia. Hivyo basi, ili kuepuka lindi la kuvunjika kwa uhusiano ambao katika miaka ya sasa hali hiyo imekuwa ni kawaida, ni vyema kwanza kabla ya kuingia kwenye uhusiano ukajihadhari na mambo yafuato.
Epuka kujiingiza kwenye uhusiano kama bado hauko tayari. Wapo watu wanajikuta wanapata tabu ya kuendelea kudumisha uhusiano walionao kutokana na kujiingiza kwenye uhusiano walipo wakiwa hawako tayari kuwa kwenye uhusiano.
Unakuta mtu mwingine ametoka kwenye uhusiano mbaya au hata hajajiandaa wala kujiwekea malengo ya kuwa na uhusiano wa namna gani au vitu anavyovitaka kwa mwenza wake, lakini anajikuta anapapukia kwenye uhusiano tu ghafla matokeo yake uhusiano husika huvunjika kutokana na wawili hao kutofautiana.
Na katika eneo hilo, pia jiepushe na mwenza asiye na malengo ya maisha au kuwa na uhusiano wa kudumu. Tukiri tu kuwa wapo wanawake na wanaume wanaotaka kuwa kwenye uhusiano wa muda mfupi kwa maana ya kwamba hawana mpango wa kuwa na uhusiano wa kudumu na kuwa na familia.
Watu wa aina hiyo, ni hatari sana kuanzisha nao uhusiano kwani pindi wanapotimiza malengo yao, bila kujali hisia zako watakuacha wewe ukiendelea na maumivu ya moyo. Japokuwa hili si lazima sana, lakini ni vyema kabla hujaingia kwenye uhusiano, uhakikishe angalau mwenza utakayekuwa naye uwe na vitu kadhaa mnavyoendana tofauti na hapo uhusiano huo utakuwa na wakati mgumu.
Ni kweli kuwa watu wanaweza kuvumiliana na kuishi pamoja hata kama wana tabia tofauti, ila kama tofauti ni kubwa sana, kuna hatari ya kuburuzana na kama hakuna mvumilivu uhusiano huo unaweza kuwa njia panda.
Hizi sifa zilizotajwa hapo juu sio za kina sana, lakini ni mojawapo ya mambo ya kuzingatia katika kuchagua mwenza wako wa maisha kabla ya kujizamisha katika mapenzi. Je wewe unaona ni mambo gani ya kuzingatia katika mahusiano na ni mambo gani yanasababisha ndoa kuvunjika? \ Usisite kuandika maoni yako kupitia h.luhindi@dailynews-tsn.tz.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment