Advertisements

Sunday, May 21, 2017

Mdee awatibua wabunge wa CCM

Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee jana aliwatibua wabunge wa CCM baada ya kuwaambia wasaidie wananchi ambao ni asilimia 65 wanaotegemea kilimo badala ya kumpongeza waziri kwa kufuta tozo za mazao.
Tangu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba awasilishe bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/18, wabunge wa CCM wamekuwa wakipongeza kwa hatua hiyo.
Kwa mujibu wa Dk Tizeba katika mwaka wa fedha 2017/18 kodi, tozo na ada 80 kati 139 ambazo zimekuwa kero kwa wakulima zitafutwa.
Akichangia bajeti hiyo, Mdee aliwataka wabunge wapya kuwasaidia wakulima ambao ni asilimia 65 badala ya kutoa pongezi kwa kufutwa kwa tozo.
“Mnasema kuwa mmefuta tozo mbalimbali badala ya kutuambia mna mkakati gani wa kuwasaidia wananchi. Tungewekeza katika kilimo ajenda isingekuwa ni kuondoa tozo,” alisema Mdee.
Hata hivyo, Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi alimpa taarifa mbunge huyo kuwa wabunge wote waliopo bungeni ni wapya na walichaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kabla ya kuapa.
Akiendelea kuchangia, Mdee alisema kuwa yeye ni mbunge wa jimbo la mjini, lakini analazimika kuyasema hayo kwa sababu wapigakura wake wanaathirika na mfumuko wa bei.
Alisema Serikali imewaahidi Watanzania kuwa kilimo kitakua kwa asilimia 10, lakini ukuaji wa sekta hiyo umekuwa ukipungua mwaka hadi mwaka.
Mbunge huyo alisema Serikali katika mwaka wa fedha 2016/17 imetoa Sh3.3 bilioni sawa na asilimia 3.3 ya bajeti ya maendeleo.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Stella Manyanya alisema malalamiko ya mbunge huyo hayana mashiko.
“Kama alivyosema yeye ni mbunge wa mjini na wabunge wa vijijini wanatambua kero za wananchi wao asiingilie uchangiaji wao,” alisema.
Mdee ambaye alikuwa akikatishwa kwa taarifa na miongozo, alisema anachokisema ni kwa nia njema ya kutaka kuishauri Serikali kwa ajili ya manufaa ya Taifa.
“Nimesoma bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji fedha iliyotolewa ni Sh8 bilioni tu kwa ajili ya kujenga miundombinu ya umwagiliaji, lakini Tume ya Umwagiliaji ina wajibu wa kueneza miundombinu ya umwagiliaji nchini,” alisema.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe alisimama na kumpa taarifa kuwa pamoja na Serikali kutoa kiasi hicho kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji lakini wafadhili wametoa Sh43 bilioni kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji.
Alisema kuwa ujenzi wa miradi hiyo unaendelea katika maeneo tofauti. Baada ya taarifa hiyo, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe aliomba mwongozo wa Spika akitaka wabunge wawe wavumilivu wakati wenzao wenye mawazo tofauti wanapochangia.
Akijibu mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge taarifa zinaruhusiwa. Hata hivyo, alionyesha kukerwa na tabia iliyoanza kujengwa na baadhi ya wabunge ya kukataa taarifa hata kama ndio hali halisi ilivyo.
Mbunge wa Newala (CCM), George Mkuchika alisimama na kutoa taarifa kuwa anachofahamu katika Bunge hilo hakuna mbunge wa mjini wala wa shamba bali wote ni sawa.
“Kila mtu ana uhuru wa kusema anachokiamini, awaachee anayepongeza aendelee kupongeza,” alisema Mkuchika.
Hata hivyo, yaliibuka maneno kutoka kwa baadhi ya wabunge wakisema bila kuruhusiwa na kiti, “mwenyekiti wa nidhamu lakini hana nidhamu.”
Akiendelea kuchangia, Mdee alisema anawashauri wabunge wapya na wa zamani wakasome Ilani ya CCM ambayo hata yeye anaisoma (akaionyesha).
“Mkasome Ilani yenu, haya nayoshauri ni kwa mafanikio yenu na Taifa mimi naisoma Ilani yenu pia,” alisema mhunge huyo.
Alisema katika bajeti Serikali imekuwa ikitenga asilimia moja kwa ajili ya utafiti, lakini fedha hizo hazitoki na kiasi kinachotolewa kwa ajili ya suala hilo ni aibu.
Mdee alisema Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema kuwa jumla ya viwanda 234 vimejengwa lakini karibu robo tatu ya viwanda hivyo viko jijini Dar es Salaam.
“Tunasema kuwa hakuna viwanda bila malighafi lakini robo tatu viko Dar es Salaam. Ukienda kuangalia unaweza kucheka ufe mbavu, havina hadhi ,” alisema .
Mbunge huyo alihoji Serikali ni moja lakini iweje leo ukisoma bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwezeshaji na ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi hazioani.
“Ukisoma hotuba zote mbili hizi ni mbingu na kingine dunia havikutani,” alisema.
Alisema inauma kuona hoja binafsi ambayo iliungwa mkono na wabunge wengi mwaka 2011 iliyoitaka Serikali kufanya ukaguzi wa ardhi na kupeleka majibu bungeni haijatekelezwa ili waweze kupanga mipango ya kutatua matatizo yaliyopo.
Aliongeza kuwa hadi leo Serikali haijaleta majibu hayo bungeni ili waweze kutatua matatizo ya migogoro ya wakulima na wafugaji nchini.
Hali hiyo iliwafanya wabunge wengi wa CCM waliofuatia kuchangia kujikita kumjibu Mdee kwamba kuondolewa kwa tuzo hizo kuna manufaa makubwa kwa wakulima.

No comments: