Advertisements

Monday, May 22, 2017

Mizani 94 kati ya 150 yatakiwa kufanyiwa marekebisho wilayani Ruangwa, mkoa wa Lindi.

Afisa Vipimo akikagua mawe ya Mizani kabla ya kuanza kuipima
Afisa Vipimo akiandaa mawe ya mizani iliyopitishwa kwa ajili ya kugonga muhuri wa Wakala wa Vipimo
Jiwe la Mizani likiwa limegongwa muhuri wenye nembo ya Bibi na Bwana pamoja na tarakimu mbili za mwaka husika (17)
Stika maalum ikiwa imebandikwa katika mizani baada ya kuhakikiwa na kupasishwa
.
Afisa Vipimo akikagua rula ya Mizani kabla ya kuanza kupima
Jiwe la Mizani likiwa limegongwa muhuri wenye nembo ya Bibi na Bwana pamoja na tarakimu mbili za mwaka husika (17)

Wakala wa Vipimo nchini imezuia matumizi ya mizani 94 kati 150 ya vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) katika Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi, isitumike hadi pale itakapo fanyiwa marekebisho na kuonekana inafaa kwa matumizi.
Wakala wa Vipimo Mkoani humo imesema, kuzuiliwa huko kutakwenda hadi msimu ujao wa ununuzi wa ufuta na korosho, na ili iweze kutumika ni mpaka pale itakapo fanyiwa marekebisho na Mafundi Mizani na kisha kugongwa mhuri tena kwa ajili ya matumizi.

Wakala wa vipimo imesema katika zoezi hilo la ukaguzi wa Mizani Wilayani Ruangwa imehakiki jumla ya vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) 23 na kukagua jumla ya mizani 150 ambapo kati ya mizani hiyo iliyopimwa na kuhakikiwa kuwa sahihi ni mizani 56 na iliyozuiliwa kutumika mpaka itakapofanyiwa marekebisho ni mizani 94.

Kwa mujibu wa wakala wa vipimo Mizani mingi imeonekana kuwa na mapungufu kama vile kutokuwa na vipimo sahihi, “Ni kwamba mizani hii tuliyo ipitia tumeabaini ina mapungufu kuanzia 200g hadi 1kg ambayo kwa kawaida mzani unatakiwa kuwa na Upungufu unaokubalika wa kiasi cha 80g tu” alisema mmoja ya maafisa wa wakala wa vipimo.

Ameongeza kuwa, Vilevile baadhi ya mizani imechakaa na kusababisha kupoteza usahihi katika Upimaji wake kutokana na namna mizani hiyo inavyo hifadhiwa mara baada ya msimu wa ununuzi kukamilika, “Mizani mingi huifadhiwa katika maeneo machafu yenye vumbi ambayo husababisha mizani kupata kutu, lakini pia njia inayotumika kusafirishia mizani hiyo si salama kwani mizani mingi husafirishwa kwa Usafiri wa pikipiki mara baada ya msimu mauzo kukamilika, ambapo husababisha mizani kuangusha baadhi ya vifaa vyake muhimu wakati wakusafiri”. Imesema taarifa hiyo ya wakala wa vipimo.

Kwa upande wake Meneja wa mkoani Lindi Bw. Stephen Masawe ameeleza kuwa wameamua kuendesha zoezi hilo la ukaguzi wa mizani ili kubaini mizani iliyo sahihi na isiyo sahihi ili kuipitisha kwa ajili ya msimu ujao wa ununuzi wa mazao.”tunaelekea katika msimu wa ununuzi wa mazao, hivyo kama mkoa lazima tujiridhishe na mizani iliyopo, kabla msimu haujaanza”, alisema Masawe.

Aidha amesema kwamba, kwa mizani itakayo hitaji marekebisho mafundi watapita kuifanyia ukarabati kisha tutaihakiki upya na kama itakuwa sawa basi itapasishwa kwa ajili ya msimu huu wa ununuzi wa ufuta na korosho.

“Zoezi hili litapunguza sana gharama za uendeshaji wa vyama vya ushirika vya msingi kwani awali mafundi mizani walikuwa wanapita na kurekebisha mizani zote, hii ilikuwa inapelekea nyama vya ushirika vya msingi kutumia gharama kubwa ya matengenezo hadi Tsh. 400,000= kwa mzani Mmoja lakini kwa sasa mafundi watapita kurekebisha mizani iliyobainika kuwa na mapungufu ambayo yameainishwa na Wakaguzi wa mizani tu” alisema Masawe.

Zoezi la uhakiki wa mizani lilianzia katika Wilaya ya Ruangwa na sasa zoezi hilo limehamishiwa katika Wilaya ya Nachingwea mkoani humo, zoezi hilo la ukaguzi wa Mizani ni zoezi endelevu ambalo humsaidia mnunuzi na muuzaji kutopunjana wakati wa mauzo ya mazao.

Wilaya ambazo hadi hivi sasa hazijafanyiwa ni Liwale, Kilwa, Lindi Mjini na Lindi Vijijini hata hivyo wakala wa vipimo amesema zoezi hilo litandelea katika wilaya hizo.

Nao wananchi kwa upande wao wameipongeza Wakala wa Vipimo kwa kuwapa elimu ya matumizi sahihi ya Vipimo pamoja na kufanya ukaguzi wa Mizani kabla ya mafundi kupewa tenda ya kuitengeneza,

Akizungumza kwa niaba ya wnanchi wenzake ndugu Laurent Adrian Muya, ambae ni mwanakijiji wa Michenga A amesema, kuhakikiwa kwa mizani kunawapa faraja na inatoa picha kuwa Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuhakikisha mkulima hapunjwi wala mnunuzi hapunjiki, “Uhakiki huu wa mizani ni ishara kwamba, Serikali yetu imedhamiria kumkomboa mwananchi, tunampongeza sana Rais wetu John Pombe Magufuli, Mungu ambariki”, alisema Laurent.

Kila mwaka Wakala wa Vipimo huendesha zoezi la Uhakiki kwa nchi nzima inapofikia msimu wa ununuzi wa mazao ya Biashara na Chakula na katika msimu wa 2017/2018, zoezi hilo limeanzia katika mikoa ya kusini ya Lindi, Mtwara na pamoja.

No comments: