Advertisements

Friday, May 19, 2017

M/kiti mstaafu wa CCM wilayani Kibiti auawa

WATU wasiofahamika wamemuua kwa kumpiga risasi Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kijiji cha Muyui, wilaya ya Kibiti, mkoani Pwani, Iddi Kirungi (60).

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kwa vyombo vya habari, kamanda wa Polisi mkoani humo, Onesmo Lyanga alisema kuwa Kirungi alipigwa risasi akiwa anatoka bafuni kuoga. Lyanga alisema kuwa tukio hilo ni la Mei 17, saa 1:40 usiku huko Muyui kata ya Mtunda wilayani Kibiti ambapo walimpiga risasi ya bega la kulia.

“Mbali ya kumuua mwenyekiti huyo mstaafu wa CCM Kijiji cha Muyui pia walimjeruhi kwa risasi tumboni upande wa kulia mwanaye, Nurdin Kirungi (18) kisha kutoweka kusikojulikana,” alisema Lyanga.

Alisema kuwa majeruhi alikimbizwa kwenye Hospitali ya Misheni ya Mchukwi kwa matibabu zaidi huku taratibu za mazishi zikiandaliwa kwa ajili ya kumzika mwenyekiti huyo mstaafu.

“Hadi sasa chanzo cha mauji hayo bado hakijafahamika na hakuna mtu aliyekamatwa na jitihada za kuwatafuta wauaji hao zinaendelea ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema Lyanga.

Aidha alisema kuwa wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari za kiusalama na kuwafichua watu wanaojihusisha na matukio ya mauaji yanayojitokeza mara kwa mara. Hivi karibuni kumekuwepo na mauaji ya kutisha katika wilaya na Kibiti na nyingine za jirani, mengi yakilenga viongozi wa Serikali za Mitaa, maofisa wa polisi na wa chama tawala cha CCM.

HABARI LEO

No comments: