Advertisements

Friday, May 19, 2017

Mwanamuziki Linah apata ‘dili’ kama la Diamond

By Herieth Makwetta, Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati watoto wa mwanamuziki Diamond Platnumz wakiwa mabalozi wa maduka ya nguo za watoto, mwanamuziki Linah Sanga anayetarajia kujifungua hivi karibuni amepata ubalozi wa duka la nguo za watoto.

Linah ambaye ni mwanamziki wa nyimbo za kizazi kipya amepata dili hilo la kuwa balozi wa duka la nguo za watoto la Kids City Shopping (KCS), zikiwa zimebaki wiki chache kabla ya kujifungua mtoto wake wa kwanza.

Linah ambaye mapema wiki hii alitambulisha herufi ya mwanzo ya jina la mtoto anayemtarajia baada ya kuweka picha ya ujauzito kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuandika ‘Baby T on the way’,anakuwa miongoni mwa mastaa ambao watoto wao wamepata bahati ya kuwa mabalozi.

“Kwa mara ya kwanza nitazungumza na mashabiki wangu mwishoni mwa wiki hii kwa niaba ya KCS ambao ni wauzaji wa bidhaa mbalimbali za watoto na akinamama wajawazito,” amesema Linah.

Hivi karibuni Linah alizindua wimbo wake mpya ‘Upweke’ na kupita katika vituo mbalimbali vya redio, televisheni na magazeti kwa ajili ya kuutangaza wimbo wake huo mpya.

Mwanadada huyo ambaye hivi karibuni alimtangaza mpenzi wake anayetarajia kuwa baba wa mtoto wake aitwaye Shabani ambaye pia ni bosi wake, Linah amedai kuwa anafuraha kuwa mjamzito kwa kuwa ni kitu ambacho alikuwa akitamani kwa muda mrefu.

“Ninafuraha kubwa kwa sababu ni kitu ambacho kama mwanamke nilikuwa nakitamani siku zote kwamba na mimi nije niitwe mama, nafuraha nimepata mtu sahihi wa kuwa mzazi mwenzangu ambaye nitalea naye watoto,”amesema.

Mzazi mwenzake ambaye pia ni mkurugenzi wa Kampuni Drops Up Entertainment ambayo inamsimamia Linah, amesema wamejipanga kuhakikisha Linah anafika mbali zaidi kimziki.

No comments: