Advertisements

Tuesday, May 9, 2017

TAIFA LAZIZIMA

Waombolezaji wakiwa katika ibada maalumu ya kuwaaga wanafunzi na wafanyakazi wa shule ya Lucky Vicent katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha jana. (Picha na Mroki Mroki).
JIJI la Arusha na vitongoji vyake jana lilisimama kwa simanzi, majonzi na vilio kwa zaidi ya saa tano wakati wa ibada maalumu ya maziko ya kitaifa ya wanafunzi 33 wa darasa la saba, walimu wawili na dereva mmoja wa Shule ya Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya Lucky Vincent ya jijini Arusha waliokufa kwa ajali ya gari Jumamosi asubuhi.

Hali ilikuwa mbaya pale miili 35 iliyokuwa ikitolewa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kupelekwa kwenye Uwanja wa Michezo wa Shehe Amri Abeid Kaluta ambako ibada hiyo ilifanyika ikiongozwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan. Maiti hizo zilikuwa katika magari maalumu matatu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yenye namba za usajili 5611JWTZ08 aina ya IVIECO, gari lingine la jeshi hilo aina ya Ashok Leyland lenye namba za usajili 9123JWTZ na gari la tatu ni la aina hiyo hiyo lenye namba za usajili 9121JWTZ.

Msafara wa magari hayo ulianza saa 2.10 asubuhi kutoka Hospitali ya Mount Meru, lakini uliingia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid saa 5.15 asubuhi, saa tatu zaidi kutokana na umati wa watu kuangua vilio barabarani pindi maiti hizo zilipokuwa zikipita na wengine kuzuia magari hayo kupita bila ya kujitambua kuwa wanafanya makosa. Askari wa JWTZ kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani Arusha ilibidi wafanye kazi ya ziada kuwaondoa watu hao barabarani waliokuwa wakigalagala kwa vilio na kuwasogeza ili maiti hizo zipite na kuelekea uwanjani ambako uwanja huo unaochukua watu zaidi ya 15,000, lakini ulijaa pengine maradufu ya uwezo wake.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ilibidi kufanya kazi ya ziada kuwaasa wananchi wa Arusha kuruhusu magari hayo ya jeshi kupitia na kusiweze kutokea majanga mengine yasiyokuwa na msingi. Hali ya vilio na majonzi ilizidi zaidi pale miili hiyo ilipoingia kwenye uwanja huo wa michezo saa 11.15 asubuhi na kufanya watu zaidi ya 155 wakubwa kwa wadogo wakiwemo wanafunzi, kuanguka kwa kuzirai baada ya kupatwa na mshituko walipoona maiti zikiwa katika majeneza zikiingia uwanjani hapo.

Kwa mujibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu Mkoa wa Arusha, watu zaidi ya 200 walizirai katika ibada hiyo ya jana. Magari ya kubeba wagonjwa yalilazimika kufanya kazi ya ziada kubeba wagonjwa waliokuwa wakianguka uwanjani na kuwakimbiza MountMeru kupata matibabu ya awali. Maiti hizo zilipofikishwa uwanjani, ziliteremshwa kwa ustadi mkubwa na askari wa JWTZ kwa kushirikiana na vijana wa Skauti na kupelekwa uwanjani sehemu ilipotengwa kwa ajili ya ibada ya kuaga wanafunzi, walimu na dereva huyo waliokufa katika ajali ya barabarani eneo la Rhotia Marera wilayani Karatu wakati basi lao aina ya Mitsubishi Rosa lilipotumbukia korongoni wakiwa safarini kwenda wilayani humo kwa mitihani ya ujirani mwema.

Hali ilizidi kuwa mbaya zaidi kwa wazazi wa wanafunzi waliokufa katika ajali hiyo kwani hawakuweza kujizuia na kila mmoja aliangua kilio pale alipoona jeneza la mtoto wake likiwa na msalaba na kuandikwa jina kamili. Hali hiyo ya kilio kwa kila mzazi ilisababisha hata viongozi mbalimbali wa serikali na vyama wakiongozwa na Makamu wa Rais, Samia waliokuwepo katika ibada hiyo maalumu, kuinamisha vichwa vyao kwa simanzi na wengine kujikaza kwa kufuta machozi kwa vitambaa vyao vya mikononi.

MAKAMU WA RAIS Akizungumza katika ibada hiyo maalumu, Makamu wa Rais, Samia amewataka madereva kote nchini kuwa waangalifu na makini wanapofanya kazi zao za kila siku kwani wajue kuwa wanabeba roho za watu. Alisema serikali kila siku imekuwa ikiwakumbusha madereva kuacha kutumia vilevi pindi wanapoendesha vyombo vya moto kwani kwa kufanya hivyo ni kutenda kosa kubwa sana, na aliwakumbusha madereva kuwa iwapo watakuwa makini na waangalifu katika kuendesha magari, ajali nyingi zinaweza kuepukika.

Mbali ya hilo, amewataka wamiliki wa magari na madereva kubeba abiria wanaostahili katika vyombo vyao vya usafiri kwa kufanya hivyo kunaweza kuepuka ajali. Alisema vifo vya wanafunzi, walimu na dereva wa shule hiyo ya awali na msingi yenye makao yake Kwamrombo jijini hapa, vimeleta huzuni kubwa sana kwa nchi na Rais John Magufuli ametoa salamu za kuwapa pole sana wafiwa na wakazi wote wa Jiji la Arusha kutokana na msiba huo mkubwa. Aliwashukuru watalii ambao ni madaktari bingwa kutoka Marekani kwa msaada mkubwa waliotoa ajali ilipotokea na kuwataka kuendeleza ukarimu huo sehemu yoyote bila ya kificho.

Alisema madaktari hao baada ya ajali ndio waliokuwa wa kwanza kufika katika eneo la tukio na kutoa huduma ya kwanza na hatimaye kufuatilia hadi hospitalini walikopelekwa, hiyo ni kiasi gani walitimiza wajibu wao wa upendo kwa nchi kwa kuwashughulikia majeruhi na wengine kupoteza masiha. Makamu wa Rais alimshukuru Rais Uhuru Kenyatta na wananchi wake wa Kenya kwa kushiriki kikamilifu katika msiba huo na pia kumtuma Waziri wa Elimu kushiriki ibada hiyo inatia moyo ni jinsi gani Kenya ilivyo karibu na Tanzania.

MBOWE Naye Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema jana ilikuwa siku muhimu sana kila Mtanzania kutafakari amani ya kitaifa. Mbowe alisema Chadema na vyama vyote vya upinzani vitakuwa mstari wa mbele na Serikali Kuu na Mkoa katika kuhakikisha kila jambo la msingi linakwenda sawa na kuwapa pole wale wote waliofikwa na msiba huo.

Alisema msiba huu ni mkubwa na Watanzania wote. KINANA Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kwa niaba ya wanachama wa chama hicho kote nchini na wabunge wake, alitoa pole nyingi sana kwa msiba huo na kuwataka wafiwa kuwa na uvumilivu katika kipindi hicho kigumu kwao. Kinana aliyeingia uwanjani hapo na Makamu wa Rais saa 3.40 asubuhi, alisema kila mtu aliyekuja uwanjani hapo ana dini na kifo ndicho huunganisha watu na kuacha tofauti zao na kuangalia kilicho mbele.

Alitumia muda mfupi sana kuongea na kuwataka wakazi wa Jiji la Arusha, wazazi na walimu kuwa wapole katika wakati huu. WAZIRI WA ELIMU KENYA Kabla ya kuingia kwa miili hiyo uwanjani, kulikuwa na salamu za viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Elimu wa Kenya, Fred Matiang’i, ambaye alisema ametumwa na Rais Uhuru, kuwa nchi yake imeguswa na msiba huo mkubwa. Matiang’i alisema wananchi wa Kenya wakiongozwa na Rais wao, wako bega kwa bega na Serikali ya Tanzania katika kuomboleza msiba huo na kuwapa pole wazazi, walezi na ndugu wa wanafunzi, walimu na dereva waliokufa katika ajali hiyo.

“Nimekuja hapa siku ya leo nimetumwa na Rais Uhuru kutoa pole na rambirambi za vifo hivyo na Kenya nzima imehuzunishwa sana, na Serikali ya Kenya imetoa pole sana kwa wale wote waliofiwa. Mungu aendelee kuwafariji na kuwapa pole katika kipindi hiki kigumu kwani sisi sote ni wamoja na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na ni lazima tushirikiane kwa hali na mali katika kila jambo,” alieleza waziri huyo wa Elimu Kenya.

SALAMU ZA SMZ Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed, alisema kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na Serikali ya Baraza la Mapinduzi wamesikitishwa na tukio hilo na wako katika majonzi na huzuni kubwa kwa msiba huo. Aboud alisema SMZ iko mstari wa mbele katika jambo hilo na kuwataka wazazi, walezi na ndugu kuwapa pole katika kipindi hiki kigumu na wao watatoa rambirambi ikiwa ni njia ya kuwafariji wafiwa.

MAWAZIRI WATOA NENO Vingozi wengine waliopata fursa ya kuzungumza ni baadhi ya mawaziri, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.

Pia walikuwapo viongozi wa dini, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa. Dk Mpango alisema alikuwa Arusha kushiriki kikao cha bajeti na mawaziri wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), lakini alipopata taarifa hiyo ilimsikitisha na hakutaka kuondoka na kusubiri ibada jana. Alisema watoto na wengine waliofariki katika ajali hiyo wanapaswa kupongezwa kwani wamefariki wakiwa kazini wakisaka elimu. Kwa upande wake, Profesa Ndalichako alisema wanafunzi na walimu wamekufa wakiwa katika harakati za kusaka elimu hivyo kazi ya Mungu haina makosa.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera, alisema kwa niaba ya wakuu wa mikoa yote na yeye kama jirani anawapa pole sana wazazi na wananchi wote wa Arusha. Bendera alisema msiba hauzoeleki na kila mtu ameguswa na msiba huo na kila mmoja wetu anawapenda sana wanafunzi na walimu wao, lakini Mungu amewapenda sana na ndio maana amewachukua ghafla.

KAIMU JAJII MKUU Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, aliwapa pole wale wote waliofiwa na kusema hiyo ilikuwa mipango ya Mungu. Jaji Juma alisema binadamu hupanga mipango yake, lakini Mungu naye hupanga mipango na kutekeleza na kuwataka wafiwa kuwa wapole katika kipindi hiki kigumu kwao. Alisema watoto hao walikuwa wakisaka mwanga wa elimu hivyo wanapaswa kuombewa kule waendako wapate mwanga zaidi.

MAENEO WANAKOZIKWA Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Gambo, wanafunzi waliopata ajali ya kufa wanasafirishwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwamo ya Nyanda za Juu Kusini katika Mkoa wa Iringa, Kyela mkoani Mbeya na Mkoa wa Tanga. Gambo alitaja maeneo mengine ya mbali ambayo yamegharamiwa na serikali ni mkoani Singida, Kondoa mkoani Dodoma, Rombo Mkoani Kilimanjaro na wanafunzi wengine wanazikwa jijini Arusha katika maeneo ambayo wafiwa watakuwa tayari kusema .

Pia baadhi ya miili ya watoto kadhaa imerudishwa hospitali walimokuwa wamepumzishwa wakisubiri siku ya kuzikwa jijini hapa; wengine wanazikwa leo, wengine kesho hadi Ijumaa katika maeneo tofauti. Gambo alisema gharama za majeneza, usafiri na nyingine zote zinagharamiwa na Serikali ya Mkoa wa Arusha na kuwataka wafiwa kushirikiana na kamati kwa kila jambo. SHULE YAFUNGWA Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ya Lucky Vincent, Ephraim Jackson, shule hiyo imefungwa kwa wiki moja kwa sababu ya maombolezo ya msiba huo.

HABARI LEO

No comments: