ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 9, 2017

MBUNGE MPYA WA CHDEMA AZUNGUMZIA MIKAKATI YAKE

DK CATHERINE RUGE NI NANI? Alizaliwa Juni 25, 1982. Alisoma Shule ya Sekondari Msalato mkoani Dodoma kuanzia mwaka 2001 hadi 2003. Baadaye alisoma Jangwani kuanzia Juni 2001 hadi Mei 2003 na kuhitimu elimu ya juu ya sekondari. Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 2004 hadi 2007 akisomea Shahada ya Biashara na Uhasibu. Mwaka 2011 – 2015 alisoma Shahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Biashara katika chuo cha ESAMI (Eastern and Southern Africa Management Institute). Kwa sasa anachukua masomo ya udaktari (PHD) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye masuala ya jinsia katika fani ya uhasibu.

By Herieth Makwetta, Mwananchi hmakweta@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mbunge mpya wa viti maalumu (Chadema), Dk Catherine Ruge ametaja vipaumbele vyake katika Bunge la Kumi na Moja kuwa ni kusimamia masuala ya jinsia, kupinga mila kandamizi na kutetea haki za watoto wa kike na wanawake.

Dk Ruge aliteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) katika kikao chake cha Mei 4 kuwa mbunge kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Dk Elly Macha aliyefariki Machi 31.

Akizungumza jana katika mahojiano maalumu, Dk Ruge alisema amekuwa akijishughulisha na masuala ya harakati za kijamii. Alisema kuingia kwake katika Bunge la Kumi na Moja kumempa jukwaa la kuzungumzia harakati hizo kwa kuwa awali alikuwa akitumia asasi kupaza sauti.

“Kabla sijawa mbunge, kuna mambo kadhaa ambayo nilikuwa nafanya. Mimi ni mwanaharakati wa kijamii ninayepinga mila kandamizi na kutetea haki za watoto wa kike na kina mama. Namshukuru Mungu kwa sasa nimepata jukwaa kubwa zaidi,” alisema Dk Ruge.Mbunge huyo ambaye ni mwanzilishi wa asasi ya Girls Education Support Initiatives (Gesi) akiwa mkurugenzi mtendaji, alisema alianzisha asasi hiyo mwaka 2014 kabla hajagombea ubunge wa viti maalumu.“Katika asasi hii nilikuwa nafanya kazi za kuwaunga mkono wasichana katika jamii za wafugaji, hasa Mkoa wa Mara ambako mimi natokea. Nikiwa na miaka 12, niliwahi kunusurika kukeketwa hivyo baada ya kusoma na kuelimika, nimefanikiwa kuelimisha jamii yangu kuhusu suala hilo,” alisema.

Akizungumzia harakati za kisiasa, Dk Ruge alisema alijiunga na Chadema mwaka 2010 na ilipofika mwaka 2013 mwishoni alianza rasmi harakati za siasa.Alianza kwa kugombea nafasi ya katibu wa rasilimali fedha Kanda ya Serengeti na kushinda.

“Nilipata nafasi hiyo na kuiwakilisha Kanda ya Serengeti yenye mikoa mitatu ya Mara, Shinyanga na Simiyu. Mwaka 2015 niligombea ubunge wa viti maalumu katika Jimbo la Serengeti kabla ya kugombea nafasi ya mweka hazina wa kanda mapema mwaka huu na sasa natumikia nafasi hiyo,” alisema.

No comments: