Advertisements

Friday, May 26, 2017

TETEMEKO LA ARDHI LAUA POLISI AKIHOJI MTUHUMIWA MWANZA

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi

TETEMEKO lingine limetokea katika baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na kusababisha kifo cha Polisi aliyekuwa akimhoji mtuhumiwa Mwanza. Tetemeko la jana limetokea takribani miezi tisa baada ya Septemba mwaka jana kusababisha vifo kadhaa na uharibifu wa mali pia mkoani Kagera.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo jana walithibitisha kuwapo kwa tetemeko hilo na kifo cha Polisi wa kike mkoani Mwanza. Kamanda Msangi alimtaja askari aliyekufa kwa mshituko kuwa ni mwenye namba za kijeshi, WP 4674, Koplo Joyce wa Kituo cha Polisi cha Misungwi.

“Tukio hili limetokea mchana majira ya saa saba; walikuwa ofisini wanahoji mtuhumiwa basi akapata mshituko… wakati wanatoka nje, akafariki maana huwa ana matatizo ya moyo,” alieleza Kamanda Msangi. Kamanda Mponjoli alisema tetemeko hilo lililodumu kwa dakika mbili hivi, limepita karibu wilaya zote za Mkoa wa Geita, Chato, Geita, Bukombe na Mbogwe.

“Hata hivyo katika ukanda wote, huu hatujapata taarifa za madhara ingawa bado tunafuatilia zaidi,” alisema Kamanda Mponjoli. “Hili tetemeko lilikuwa na kishindo kikubwa kama ngurumo za radi au kitu kinacholipuka na tulikuwa ofisini tukadhani ni mlipuko wa baruti za kwenye mgodi wa GGM ingawa haukuwa mlipuko wa kawaida tuliouzoea,” alisema.

Alisema kwa kuwa lilitokea mchana wakati wa kazi, watu walipata kihoro na kukimbia. “Inaonekana kuna hali kama hiyo maana hata usiku wa kuamkia leo (jana) yapata saa mbili hivi usiku, hali kama hiyo ilijitokeza ingawa licha ya kuwa na nguvu, watu hawakujali sana,” alisema Kamanda.

HABARI LEO


No comments: