ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 3, 2017

WABUNGE WA CCM WAMTETEA HALIMA MDEE



Mbunge wa Kawe, Halima Mdee
By Reginald Miruko, Mwananchi; rmiruko@mwananchi.co.tz

Dodoma. Saa chache baada ya Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kunusurika adhabu ya kutohudhuria vikao vyote vilivyosalia vya Bunge la Bajeti, amejitokeza na kuelezea kuguswa kwake na jinsi wabunge wa pande zote walivyomtetea licha ya kutokuwapo bungeni.

Amesema endapo umoja huo utaendelezwa, chombo hicho cha kutunga sheria kitafanya mambo makubwa na kwa haki.

Jana, wabunge CCM na upinzani waliungana na kuamua kumsamehe Mdee baada ya Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kupendekeza asimamishwe vikao vilivyosalia vya Mkutano wa Bajeti.

Mdee pamoja na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe walifikishwa kwenye kamati hiyo kwa makosa yanayofanana ya kudharau kiti cha Spika na kutoa maneno ya kuudhi ndani na nje ya Bunge.

Kamati hiyo pia, iliwahoji Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti kwa kosa kama hilo la kulidharau Bunge.

Wakati taarifa ya kamati iliyowasilishwa na mjumbe wake, Almasi Maige (Tabora Kaskazini-CCM) ilikuwa imependekeza watuhumiwa hao wasamehewe, isipokuwa Bulaya aliyetakiwa kupewa karipio kali na Mdee aliyetakiwa kusimamishwa vikao vilivyosalia vya Mkutano wa Bajeti utakaomalizika Juni 30 mwaka huu.

Mdee, ambaye pia ni waziri kivuli wa fedha, alikosa Bunge la bajeti la mwaka jana baada ya kuadhibiwa.

Wakijadili hoja hiyo ya kamati, wabunge wote waliochangia waliafiki Mdee asamehewe kwa kuwa alishaonyesha amebadilika kwa kuomba radhi bungeni.

Walisema utolewe msamaha ili Bunge lifungue ukurasa mpya, na wabunge waanze kuheshimu kiti na Bunge lenyewe na hivyo kuwa na nguvu ya pamoja dhidi ya watu wa nje ya mhimili huo.

Baada ya mjadala ulioonekana kumtetea mbunge huyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama alitoa hoja ya kubadili azimio lililowasilishwa na kamati na kupendekeza asamehewe kwa masharti.

Katika azimio lake jipya ambalo liliridhiwa na Bunge, Mhagama alitaka mbunge huyo ambaye haikuwa mara yake ya kwanza kufanya kosa hilo na kuhukumiwa, ikitokea akatenda kosa jingine kama hilo adhabu hiyo itekelezwe bila kurudi tena kwenye kamati hiyo.

Kuhusu azimio hilo ambalo lilikubaliwa na Bunge, Mdee alisema sharti alilopewa ni changamoto kubwa kwake katika kipindi kilichosalia cha vikao hivyo vya Bunge.

No comments: