Msaada iliyotolewa katika hospiali ya Butimba jijini Mwanza kutoka kwa wanawake wa Dini ya Kiislamu wa Msikiti wa Khoja Shia Ithna Asheri Mwanza.
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
WANAWAKE wa Dini ya Kiislamu wa Msikiti wa Khoja Shia Ithna Asheri jijini Mwanza wametoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 2 kwa Hospitali ya Butimba ya Wilaya ya Nyamagana ili kusaidia kupunguza changamoto zinazoikabili.
Mwenyekiti wa kina mama hao Radhida Ahmed akimkabidhi msaada huo Kaimu Mganga Mkuu wa Jiji la Mwanza, Dk. Kajiru Mhando alisema utasaidia kupunguza kero kwa wagonjwa na kuzitaka taasisi zingine zijitokeze kutatua changamoto za hospitali hiyo hasa ujenzi wa wodi ya wazazi.
Alisema msaada huo umelenga kuonyesha mshikamano wao kwenye jamii katika kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa mjukuu wa Mtume, Imam Mahdi (A.T.F.S) ambayo hudhimishwa Mei 7, kila mwaka.
“ Tuliguswa na changamoto zinazoikabili hospitali yetu hii ya wilaya lakini pia kuonyesha mshikamano wetu na jamii tukaona tuje kutoa msaada huu kwa ajili ya kuwapunguzia wagonjwa kero na changamoto,Wapo wenye utajiri waone na kuguswa na matatizo ya wenzao na kuwasaidia hasa wagonjwa” alisema Rashida.
Aliutaja msaada huo walioukabidhi kuwa ni magodoro 10, mashuka pea 25 na foronya zake, mablanketi 50 na vyandarua 50, vifaa vya usafi (mifagio 10, brashi 10 na Squizers 10) pamoja na sabuni ya maji (Detol) lita 10 na ya unga kg 15.
Vingine ni vifaa tiba ambavyo ni mashine mbili za kupima mapigo ya moyo,Stethescope mbili na, Heavy duty Gloves(pea 5),Sterile Gloves (boksi 4) makasha ya kuhifadhia uchafu makubwa na madogo (12) na zawadi kwa watoto.
Awali Mwenyekiti mstaafu wa Msikiti huo Alhaji Sibtain Meghjee alisema jamii ya Waasia na Waislamu shughuli wanazozifanya kwenye jamii hazipewi fursa ya kutangazwa kwenye vyombo vya habari.
“Kwetu sisi Waislamu, hasa Asian Community ( jamii ya Waasia) shughuli nyingi za kijamii tunazofanya hazipewi nafasi kwenye vyombo vingi vya habari.Vyombo vingi viko mstari wa mbele kutangaza zaidi migogoro kuliko misaada inayolenga kusaidia jamii, kujenga umoja na mshikamano kwenye jamii,” alisema Meghjee.
Akipokea msaada huo Dk. Mhando aliwapongeza akina mama hao kwa moyo wao wa huruma na kujitoa kuisaidia hospitali hiyo na kwamba utawasaidia kupunguza changamoto lukuki zilizopo .
“Ingawa bado tuna changamoto ya ukosefu wa wodi ya wanaume lakini vifaa hivi vimetusaidia sana na vitaanza kutumika leo hii hasa katika wodi ya wazazi ya akina mama wanaojifungua ambao wengi ndio waathirika,”alisema.
Dk. Mhando alieleza kuwa hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa madawa, vifaa tiba na vitendanishi pamoja na miundombinu ya majengo pia haina kitanda cha kutolea damu, mashine ya kupima mapigo ya moyo ya mtoto akiwa tumboni ili kutambua kama yu hai ama la.
“Wodi zilizopo kwenye hospitali yetu ya wilaya hazitoshi na hatuna wodi ya wanaume na wanaokuja kutibiwa hapa na kutakiwa kulazwa, tunalazimika kuwapa rufaa ya kwenda Hospotali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure,”alisema Dk. Mhando.
Wanawake wa Dini ya Kiislamu wa Msikiti wa Khoja Shia Ithna Asheri Mwanza wakabidhi Blanketi
Dk Kajiru akipokea moja ya godoro kati ya 10 yalitolewa msaada wa akinamama wa Msikiti wa Khoja Shia Ithna Asheri Mwanza
Mwenyekiti wa Wanawake wa msikiti wa Khoja Shia Ithan Ashaeri Rashida Ahmed pamoja na Mrs karimu wakimfurahia mtoto Hajida walipotelea wodi ya wazazi kwenye hospitali ya Butimba.
No comments:
Post a Comment