Advertisements

Friday, June 2, 2017

DIWANI WA CHADEMA ARUSHA AJIUZULU

By Moses Mashalla,Mwananchi mmashalla@mwananchi.co.tz

Arusha. Diwani wa Chadema, kata ya Bangata wilayani Arumeru (Arusha) Emmanuel Mollel amejiuzulu nafasi yake ikiwa ni siku chache baada ya kutuhumiwa na uongozi wa chama hicho kwa utovu wa nidhamu.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, Christopher Kazeri amethibitisha taarifa za kujiuzulu kwa diwani huyo na kusema kwamba ofisi yake imepokea taarifa za kujiuzulu kwake.

Mollel alipotafutwa kwa njia ya simu leo, Juni Mosi, 2017, alikiri kuandika barua ya kujiuzulu huku akisema kwamba amefanya uamuzi huo kwa utashi wake binafsi lakini akakanusha kupewa barua yoyote ya onyo na uongozi wa chama hicho.

Katibu wa Chadema mkoani Arusha,Aman Gorugwa amethibitisha taarifa za kujiuzulu kwa kiongozi huyo na kusema kuanzia leo Mollel sio mwanachama wa Chadema tena.

Gorugwa amesema kwamba uongozi wa chama chao ulimwandikia barua hivi karibuni ya kumtaka ajieleze sababu za kutowajibishwa kutokana na tuhuma zinazomkabili.

Ametaja tuhuma hizo kuwa ni pamoja na utovu wa nidhamu,mwenendo usiofaa ,kwenda kinyume na maagizo ya chama na usaliti.

Amesema hata kabla ya kujibu tuhuma hizo walipokea barua ya kujiuzulu kwake.
Katibu huyo amesema kwamba jina la Mollel lilikuwa kwenye orodha ya kitabu cheusi (black book) na alikuwa kwenye hatua za mwisho za kutimuliwa.

No comments: