ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 30, 2017

KIINI CHA MAUAJI KIBITI KUJULIKANA LEO

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana alipotembelea Bohari Kuu ya Jeshi la Polisi iliyopo jijini.(Picha na Fadhili Akida).

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, leo anatarajia kukutana na maofisa wa ngazi ya juu wa Jeshi la Polisi nchini, kujadili na kuweka mikakati ya kudhibiti matukio ya uhalifu ikiwemo mauaji ya Kibiti.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na waziri huyo wakati akizungumza na waandishi wa habari, kabla ya kufanya ukaguzi kwenye bohari ya jeshi la Polisi iliyopo eneo la Kurasini jijini humo. Baadhi ya maofisa hao wa ngazi za juu wa jeshi hilo ni pamoja na wakuu wote wa operesheni maalumu, makamanda wa polisi (RPC) na wapelelezi kutoka mikoa yote.

“Kabla ya kufanya ukaguzi huu (bohari), kuna mambo mengi mazito nimeyagundua, hivyo naomba mnipe nafasi ya kuyazungumzia mambo haya pamoja na yale tutakayokubaliana katika kikao kitakachofanyika kesho (leo) cha maofisa wa ngazi za juu wa polisi,” alisema Masauni. Alisema katika kikao hicho, pia watajadili suala la mauaji yanayoendelea katika eneo la Kibiti mkoani Pwani, na kuwataarifu wananchi kupitia vyombo vya habari juu ya kilichojadiliwa katika kikao hicho na mikakati iliyopitishwa.

Pamoja na suala hilo la mauaji ya Kibiti, pia Masauni alisema kikao hicho kizito kitajadili masuala mengine ya uhalifu katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo suala la mauaji ya watu watatu yaliyofanyika kwa nyakati tofauti lakini yakitumia mtindo mmoja wa mauaji. “Naomba mnivumilie hadi kesho (leo) nitakapokutana na maofisa hawa na kati ya mambo tutakayoyajadili ni pamoja na suala hili la mauaji ya Kibiti,” alisema.

Aidha, waziri huyo ambaye aliita waandishi wa habari kwa ajili ya kukagua bohari hiyo ya polisi, aliwataarifu waandishi hao kuwa katika kikao chake cha ndani kabla ya kufanya ukaguzi, alibaini mambo makubwa na mazito yanayohusu bohari hiyo. Hata hivyo, alisema hawezi kuyazungumzia masuala hayo aliyoyabaini kwa sababu ya muda kwani alikuwa hajakagua maeneo yote ya bohari hiyo.

Aliahidi kuanika mambo yote aliyoyabaini leo baada ya kukutana na maofisa hao wa polisi, katika mkutano wa waandishi wa habari atakaouandaa. Tangu kuanza kwa mfululizo wa mauaji ya polisi na raia katika maeneo hayo ndani ya mwaka huu, zaidi ya watu 35, wakiwemo polisi 13, wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana. Tukio la mwisho lilitokea siku mbili zilizopita wilayani Kibiti, baada ya viongozi wawili wa Kijiji cha Mangwi, Kata ya Mchukwi kuuawa kwa kupigwa kwa risasi

HABARI LEO



No comments: