Advertisements

Friday, June 30, 2017

Rais Magufuli amlilia Mkurugenzi wa AfDB aliyefariki ghafla

Dk Tonia Kandiero enzi za uhai wake

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kutokana na kifo cha ghafla cha Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kanda ya Afrika Kusini, Dk Tonia Kandiero.

Dk Kandiero amefariki dunia ghafla jana usiku Juni 28 akiwa ofisini kwake Pretoria, Afrika Kusini.

“Kwa mshituko na masikitiko makubwa nimepokea taarifa za kifo cha Mkurugenzi Mkuu wa AfDB Kandiero aliyefariki dunia ghafla jana usiku akiwa ofisini kwake huko Pretoria,” amesema Rais.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, imeeleza kuwa kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa AfDB katika Ofisi za Kanda ya Afrika Kusini mwishoni mwa mwaka 2016, Dk Kandiero alikuwa Mwakilishi wa AfDB Tanzania.

“Nitamkumbuka Dk Tonia Kandiero kama mchapakazi hodari aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yetu, nikiwa Waziri wa Ujenzi nimeshirikiana nae kwa karibu kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kwa nchi yetu ambayo imefadhiliwa na AfDB, ametoa mchango mkubwa kufanikisha ujenzi wa madaraja na barabara za Dodoma – Iringa, Dodoma – Babati, Namtumbo – Tunduru – Mtambaswala, Arusha – Taveta – Voi na pia alitoa mchango mkubwa katika kufanikisha miradi mingine ambayo ipo mbioni kutekelezwa ikiwemo ujenzi wa barabara ya Bagamoyo – Tanga – Mombasa, Mbinga – Mbambabay na Tabora - Katavi” amesema Rais.

Rais ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa AfDB Dk Akinwumi Adesina, familia ya Dk Kandiero, wafanyakazi wote wa AfDB, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huu.

No comments: