Advertisements

Tuesday, June 6, 2017

Majeruhi wa Lucky Vincent atembea kwa mara ya kwanza

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Mmoja wa majeruhi wa ajali ya basila Shule ya Lucky Vincent, Sadia Ismael ametembea kwa mara ya kwanza tangu alipopata ajali hiyo Mei 11, mwaka huu.

Ajali hiyo iliyotokea katika eneo Rhotia, Karatu mkoani Arusha, iligharimu maisha ya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja na kujeruhi wanafunzi watatu ambao walisafirishwa Marekani kwa ajili ya matibabu.

Wanafunzi hao ni Sadia, Wilson Tarimo na Doreen Mshana ambao wanaendelea na mazoezi ya viungo katika makazi yao mapya mjini Sioux IA baada ya kuruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Mercy, Marekani.

Sadia ambaye hakuwahi hata kunyanyua mguu leo ameweza kufanya hivyo kwa mara ya kwanza wakati akiendelea na mazoezi ya viungo.

Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ambaye ana mchango mkubwa kwa safari ya wanafunzi hao Marekani, amebainisha hilo katika ukurasa wake wa Facebook.

“Mtoto Sadia Atembea kwa kupanda ngazi kwa mara ya kwanza. Praise the Lord...aanza rasmi mazoezi ya kutembea,”ameandika Nyalandu.

Jana Nyalandu ambaye amekuwa akitoa taarifa za maendeleo ya wanafunzi hao kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii hasa Facebook na Twitter, jana aliandika kuwa pamoja na mazoezi ya viungo, watoto hao wanaanza kufundishwa kwa saa moja kila siku saa 9 alasiri.

Alisema wazazi wao walioambatana nao kwenye safari hiyo wanaanza darasa la lugha kwa saa moja kila siku saa 3.00 asubuhi.

“Tunawashukuru walimu wote waliojitolea kwa kazi hii. Tuendelee kuwaombea watoto wetu,”aliandika Nyalandu.

1 comment:

Anonymous said...

Amen!!!