ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 28, 2017

Mkuu wa Mkoa Dodoma apiga marufuku shisha

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana amepiga marufuku uvutaji wa kilevi aina ya shisha unaoendelea kwenye mahoteli yote mkoani hapa akisema ni sehemu ya matumizi ya dawa ya kulevya.
Rugimbana ametoa kauli hiyo leo (Jumatano) mjini hapa kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani yanayofanyika leo mjini Dodoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Amesema kuwa Mkoa wa Dodoma ni mojawapo ya mikoa iliyoathirika zaidi na madawa ya kulevya kwa kuwa ina vijana wengi ambao wapo vyuoni hivyo ni walengwa wakubwa wa madawa hayo.
Amesema hoteli nyingi zimekuwa na mtindo wa kuweka kilevi aina ya shisha kwa ajili ya kuwavutia wateja wao na hivyo kukipiga marufuku kilevi hicho mkoani hapa.
"Shisha ni madawa ya kulevya ina athari kubwa kwa maisha ya binadamu hivyo basi kuanzia leo ni marufuku uvutaji shisha mkoani hapa hasa kwenye mahoteli ambapo huwa wanapenda kuweka kilevi hicho," amesema Rugimbana.
Mbali na hilo, amepongeza juhudi zinazofanywa na Jeshi la Polisi katika mapambano dhidi ya madawa ya kulevya kwa kung'oa miche ya bhangi na kuwafikisha wahusika mahakamani.
Kwa upande wake mwakilishi wa Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Kinga, Tiba na Utafiti Dk, Cassian Nyandindi, alisema kuwa kuna njia kuu tatu za kupambana na dawa za kulevya ambazo hutumika duniani kote ambazo ni kuwakamata na kuwadhibiti wasambazaji na wauzaji wa dawa za kulevya.
Nyingine amesema ni kutoa elimu ya madhara ya dawa za kulevya kwa watu ambao bado hawajaingia kwenye matumizi na kutoa fursa ya tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya ili kupunguza madhara yaliyotokana na madawa ya kulevya.
Maadhimisho hayo ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani yatafanyika leo kitaifa mkoani Dodoma ambapo kauli mbiu inasema tuwasikilize na kuwashauri vijana na watoto ili kuwaepusha na dawa za kulevya.

No comments: