ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 14, 2017

NDUNGAI AWATAJA SUMAYE, LOWASSA SAKATA LA MCHANGA

By Julius Mnganga, Mwananchi jmathias@mwananchi.co.tz

Siku moja baada ya Rais John Magufuli kupokea ripoti ya pili ya kamati iliyochunguza masuala ya kiuchumi na kisheria kwenye mchanga wa madini (makinikia), wabunge wa upinzani wametaka maraiswastaafu washtakiwe, lakini, Spika Job Ndugai akawageuzia kibao na kuwatahadharisha kuwa wasisahau kwamba wanao mawaziri wakuu wawili wastaafu.

Ingawa hakuwataja kwa majina, lakini mawaziri wakuu wawili walio katika kambi ya upinzani ni Frederick Sumaye na Edward Lowassa aliyegombea urais kwa tiketi ya Chadema mwaka 2015.

Juzi, kamati ya kisheria na kiuchumi iliwasilisha ripoti na kubainisha kasoro nyingi kwenye taarifa za kodi, wizi wa madini na ukwepaji kodi na kutoa mapendekezo 21.

Miongoni mwa mapendekezo hayo, wadau wengi hasa wabunge walivutiwa na kuwapo kwa haja ya kupitia upya sheria, sera na mikataba ya wawekezaji wa sekta ya madini.

Maoni ya upinzani

Wakichangia mjadala wa Bajeti, wabunge wa upinzani wakiongozwa na wale wa Chadema walisema marekebisho ya sheria za madini ndizo zitakazotoa suluhisho la kudumu kwenye sekta hiyo, huku wakitaka marais wastaafu waondolewe kinga.

Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche aliitaka Serikali kuwaruhusu wananchi wanaozungukwa na migodi kusaidia kuwakamata wezi hao wa madini huku wao wakiachwa bila manufaa yoyote.

Alisema wapo wananchi ambao waliporwa ardhi na kuondolewa kwenye maeneo yao kwa nguvu kupisha wawekezaji hao ambao sasa wamethibitika kuwa ni wezi.

“Kwa hili, nashauri Rais (John)Magufuli alete mabadiliko ya Katiba ili watangulizi wake wachunguzwe.”

Alisema haiwezekani mawaziri wafanye dhambi hizo bila kushirikiana na Rais aliyepo madarakani.

Hakuwa pekee yake aliyekuwa na msimamo huo. Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali alipigilia msumari kile alichozungumza Heche kiasi cha kumfanya Spika Ndugai kutoa tahadhari kwa wapinzani kuwa wasisahau mabadiliko hayo ya Katiba yakifanywa, yatawahusisha hata mawaziri wakuu ambao wamehamia upinzani.

“Mkumbuke, hao viongozi mnaotaka wakamatwe, mnao wawili huko ndani, mawaziri wakuu wastaafu. Watakapobanwa msianze kupiga kelele hapa,” alisema Ndugai akihitimisha mchango wa Lijualikali.

Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa alitaka mabadiliko ya Katiba ili kuruhusu kushtakiwa kwa Rais atakayebainika kutenda kosa la jinai akiwa madarakani.

Wakati mbunge huyo akitoa mchango wake ambao kwa kiasi kikubwa alikuwa hakubaliani na suala la kuiita kampuni ya Acacia wezi, Spika aliingilia kati tena na kutoa ufafanuzi wa wizi unaofanywa na wawekezaji wa madini licha ya ubovu wa mikataba iliyopo.

Spika alifafanua kwamba makubaliano yaliyokuwapo yamekiukwa na watu hao ambao wamefanya wizi wa rasilimali za Taifa.

“Kama mmekubaliana mwekezaji atatoa mchanga wa tani 20, lakini yeye anajaza tani 26 huo ni wizi” alisema na kuongeza:

“Kama anakwambia anachukua makinikia kwenda kuchenjua kwa kuwa mtambo haupo nchini kumbe anayauza juu kwa juu mtu huyu hajawa mwizi? Hata kama mkataba ni mbovu, kwa mwenendo huu hawa ni wezi tu.”

Msigwa alijaribu kumteteta aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwamba aliingia madarakani wakati mikataba na sheria nyingi zikiwa zimepitishwa tayari.

Hata hivyo, Ndugai alimkumbusha kwa kusema, “Unayejaribu kumtetea unaweza ukawa humjui vizuri kuliko wengine. Ni bora ukachangia hoja yako tu.”

Msimamo wa Msigwa ulikuwa ni katika makosa yaliyopo kwenye mkataba uliowapa Acacia uwezo wa kuendesha shughuli zao.

Alisema sheria nyingi za madini zilizopo zilipitishwa kwa hati ya dharura hata aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, ambaye sasa ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alitolewa nje ya Bunge alipoeleza kuhusu upungufu uliopo kwenye sheria na mikataba.

Akieleza kuhusu anachokifanya Rais Magufuli sasa alisema: “Ni kama mgombea binafsi, sera ya CCM ameiweka pembeni. Kama kweli ana dhamira ya kweli ya kuleta mapinduzi, basi aruhusu mabadiliko ya Katiba ili marais wahojiwe.”

Hiyo ilimfanya Ndugai atoe ufafanuzi mwingine, “Hakuna bajeti ilikuwa inapita kwa ugumu kama ya nishati na madini. Mara zote wabunge walikuwa wanapinga ufisadi tangu siku nyingi.”

Lissu amtaja ‘Waziri’ Kikwete

Akichangia mjadala wa mchanga wa madini, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliipa changamoto Serikali kwa kuitaka kumuingiza Jakaya Kikwete katika orodha ya watuhumiwa wa sakata la makinikia.

Lissu alisema wakati wa kusaini mikataba ya madini, Kikwete alikuwa Waziri wa Maji, Nishati na Madini.

“Katika taarifa hii ya jana wamependekeza watu fulani fulani washtakiwe makamishna, mwanasheria mkuu (Andrew) Chenge, (aliyekuwa waziri wa nishati, William) Ngeleja, jamani naombeni niwaambie kitu ili wabunge muwe na maarifa,” alisema na kuongeza:

“Mtu wa kwanza kusaini mikataba na leseni za madini alikuwa ni Jakaya Kikwete, Agosti 5 mwaka 1994 alisaini leseni ya Bulyanhulu inayopingwa leo hii wakati akiwa Waziri wa Maji, Nishati na Madini wakati huo hakuwa na kinga ya urais.”

Alisema wakati aliposaini leseni na mikataba hiyo alikuwa hana kinga kwa masuala ambayo aliyafanya.

“Rais (Kikwete) alisaini si ya Bulyanhulu pekee, ya Nzega, ya Geita hizo leseni zina saini ya Kikwete anaponaje kwa mapendekezo haya? Anaponaje kama kweli mnataka kuwashughulikia watu walioshiriki kwenye mambo haya?” alihoji.

“Mbona mnachagua chagua hizi? Leseni na hizi sheria tangu mwaka 1999 tumesema tatizo kubwa ni sheria.”

Alimtaka Spika wa Bunge Ndugai kama anataka kukumbukwa wakati wa uongozi wake, basi asikubali kupitisha miswada ya sheria kwa hati ya dharura.

Akijibu hilo, Ndugai alisema atairuhusu miswada hiyo ya madini na gesi iingie bungeni kwa hati ya dharura.

“Kwanza wanaoamua si mimi tu ni Kamati ya Uongozi ya Bunge, lakini kama itakuja kwa hati ya dharura hii (madini) itaruhusiwa kwa sababu moja tu tunaibiwa sana,” alisema.

Mdee, Bulaya wapigwa mkwara

Wakati mjadala wa madini ukiendelea kutikisa, Spika Ndugai alihitimisha kipindi cha Bunge cha asubuhi kwa kuwataka wabunge waliopewa adhabu, kujiepusha na kauli dhidi ya Bunge vinginevyo hatua kali zitachukuliwa.

“Wapo wenzetu ambao walichukuliwa hatua za kinidhamu ila baadhi yao wamekuwa wakifanya malumbano na Bunge na kutoa kauli ambazo si nzuri,” alisema Ndugai.

Kuepuka matatizo zaidi, aliwataka kujiepusha na maneno yanayowakwaza wengine kwani kufanya hivyo ni kuanzisha mapambano ambayo yanaweza kuwaumiza zaidi.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya wamesimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge mpaka Bunge lijalo la bajeti mwakani.

No comments: