ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, June 25, 2017

TADB: “TENDEENI HAKI MAFUNZO YA UKOPESHAJI KATIKA KILIMO”

Na mwandishi wetu,

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imewataka wahitimu wa mafunzo ya Kanuni za Ukopeshaji katika Kilimo kuyatendea haki mafunzo hayo kwa kutumia utaalamu walioupata katika kuwahudumia wakulima wanaomba mikopo kwenye taasisi zao.

Akizungumza na wahitimu hao wakati wa ufungaji wa awamu ya pili ya mafunzo hayo, Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Albert Ngusaru amesema kuwa wahitimu hao wanapaswa kutumia weledi katika utendaji kazi wao ili waweze kuyatendea haki mafunzo hayo.

Bw. Ngusaru ameongeza kuwa mafunzo hayo yaliyokuwa na lengo la kuwajengea uwezo watoa huduma hasa kutoka mabenki na taasisi za kifedha nchini kuweza kutoa huduma kwa wakulima kwa wakati na kuzingatia tija wakulima nchini ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.

“Nawaomba mukayafanyie kazi kwa vitendo mafunzo haya ili kuchagiza malengo ya Serikali katika kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini,” alisema Bw. Ngusaru.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Bw. Augustino Matutu Chacha amesema kuwa TADB ipo tayari kushirikiana na Mabenki na Taasisi za fedha nchini katika kuwakopesha wakulima nchini ili kuharakisha mapinduzi na maendeleo katika Sekta ya Kilimo, ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 75 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi nchini na pia kutoa kiasi cha zaidi ya asilimia 65 cha mali ghafi kwa ajili ya viwanda.

“Tupo tayari kushirikiana na mabenki yote nchini katika kukopesha mnyonyororo mzima wa sekta ya kilimo na mifugo hili kuunga mkono juhudi za Serikali za kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini,” alisema.

Akizungumzia faida aliyoipata baada ya kuhudhuria mafunzo hayo, mmoja wa wahitimu hao, Bi. Vivian Sakoe kutoka Benki ya NMB amesema kuwa mafunzo hayo yamewajenga katika kutoa huduma bora kwa wakulima ambao ndio walengwa wakuu wa mikopo ya kilimo nchini.

“Tumepata utaalamu wa hali ya juu sana kwa kujifunza na kufahamu kwa undani vigezo vya kuzingatia wakati wa utoaji wa mikopo kwa wakulima ambavyo hapo awali hatukuwa nao, hakika tunaishukuru TADB kwa mafunzo haya,” alisema.

Mafunzo haya yaliendeshwa kwa ushirikiano wa pamoja kati ya TADB, Benki ya Taifa ya Kilimo na Maendeleo Vijijini India (NABAD) na Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani Mazao na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) na kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 50 kutoka taasisi zinazojishughulisha na utoaji wa mikopo kwa wakulima nchini

Viongozi waandamizi kutoka TADB, Bw. Augustino Chacha (kushoto) na Bw. Albert Ngusaru (wapili kushoto) wakizungumza na Wakufunzi kutoka NABARD, Dkt. R.S. Reddy (kulia) na Bw. M.R. Gopal (wapili kulia) wakati wa ufungaji wa mafunzo ya awamu ya pili yanayohusiana na Kanuni za Ukopeshaji katika Kilimo yaliyokuwa yanafanyika katika Hoteli ya Beachcomber Dar es Salaam.Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Bw. Augustino Matutu Chacha akizungumza na washiriki wa mafunzo ya awamu ya pili yanayohusiana na Kanuni za Ukopeshaji katika Kilimo wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo.


Mshauri wa Kiufundi wa MIVARF, Bw. Ravi Malik akizungumza wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo.


Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Bi. Vivian Sakoe kutoka Benki ya NMB akizungumzia faida aliyoipata baada ya kuhudhuria mafunzo hayo.

Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Albert Ngusaru (watatu kushoto) akifunga rasmi mafunzo ya awamu ya pili yanayohusiana na Kanuni za Ukopeshaji katika Kilimo yaliyokuwa yanafanyika katika Hoteli ya Beachcomber Dar es Salaam. Wengine pichani ni wakufunzi na maafisa kutoka TADB na MIVARF.
Mshiriki kutoka TADB, Bibi Rosemary Gordon akipongezwa na Mkufunzi wa mafunzo hayo, Dkt. R.S. Reddy mara baada ya kukabidhiwa cheti cha kufuzu Mafunzo ya Awali ya Kanuni za Ukopeshaji katika Kilimo.

Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Albert Ngusaru (kulia) akiwakabidhi zawadi ya shukrani Wakufunzi kutoka NABARD, Dkt. R.S. Reddy (kushoto) na Bw. M.R. Gopal (wapili kushoto) baada ya kufunga rasmi mafunzo ya awamu ya pili yanayohusiana na Kanuni za Ukopeshaji katika Kilimo.

No comments: