ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 28, 2017

TAMCO KUENDELEZA HARAKATI ZA KIDINI, KIJAMII TANZANIA

Na Swahilivilla, Washington
Jumuiya ya Waislamu wa Tanzania waishio katika jiji la Washington na vitongoji vyake (TAMCO), imejidhatiti kuendeleza harakati za kijamii nchini Tanzania.
Mweka Hazina  wa Jumuiya ya Waislamu wa Tanzania  (TAMCO), Bi Asha Hariz 
Hayo yalielezwa na Mweka Hazina wa Jumuiya hiyo Bi Asha Hariz katika mazungumzo maalum na Swahilivilla pembezoni mwa Sherehe za Idd Al-Fitri zilizoandaliwa na jumuiya hiyo kuadhimisha kumalizika kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani katika Mji huo Mkuu wa Marekani.
Katika Sherehe hizo zilizohudhuriwa na Balozi Mstaafu Bwana Mustafa Nyang'anyi, Bi Asha alisema kuwa, kwa kupitia Kamati yake ya Uhamasishaji, TAMCO imekuwa ikifanya juhudi za kusaidia katika shughuli kama za ujenzi wa Misikiti na vituo vya mayatima nchini Tanzania.
Alitoa mfano wa ujenzi wa Msikiti katika Mkoa wa Simiyu uliofadhiliwa na jumuiya hiyo akisema: " Kule Simiyu, Waislamu wenzetu walikuwa wana ardhi tu, lakini walikuwa hawajui jinsi ya kuiendeleza. Alhamudu Lillah, Mwenyezi Mungu ametuunganisha nao, na wanachama wetu wakajitolea kwa michango, na kuwasaidia kusimamisha Msikiti"
Wanafunzi waanza masomo ya Darsa, ndani ya  Msikiti wa Simiyu.
TAMCO haikusitisha juhudi zake baada ya kusimama kwa kuta za Msikiti huo tu, bali iliendeleza juhudi ili kuhakikisha kuwa Msikiti huo unakuwa na huduma zote muhimu ikiwemo nishati ya umeme.
"Baada ya Msikiti kusimama, bado kulikuwa na haja ya Msikiti huo kuwa na huduma ya umeme, nasi tukafanya juhudi za michango tukawatumia, na sasa Msikiti huo una umeme", alisema Mweka Hazina wa TAMCO.
Mbali na huduma kama hizo za majengo ya ibada, Bi Asha Hariz aliendelea kufafanua kuwa Jumuiya yake inaendesha vituo vya Mayatima nchini Tanzania.
"Sasa hivi tuna mradi mwengine wa kuwasaidia watoto mayatima. Tuna kituo pale Tandale, Dar es Salaam, na chengine Kibaha, kwa hivyo wale watoto nao pia tunawasidia." Alifafanua.
Image may contain: one or more people
TAMCO Zakatul Fitri kwaajili ya kusaidia Tanzania Aliongeza kusema: "Na katika kipato chengine tunachokusanya ni Zakatul Fitri, ambazo kwa mwaka huu tumepeleka Zanzibar - Unguja na Pemba ili kuwasaidia wanawake wenye uwezo mdogo wa kiuchumi. Na sehemu nyengine ya Zaka hiyo tumeipeleka kwenye vituo vyetu vya mayatima na Simiyu".
Hatua hizo za uhamasishaji wa huduma za kijamii, inatokana na imani yakinifu ya TAMCO kuwa kutoa Zakka ni wajibu kwa Waislamu. Hayo yanasisitizwa na Bi Asha kwa kusema: "Tunajua kuwa kadri Mwenyezi Mungu anavyokubariki inabidi umsaidie mwenzio.
Alifafanua kuwa, fedha zinazopatikana katika mapato ya kawaida kama vile ada za Wanachama, hutumika katika kuendeshea ghughuli za kawaida za jumuiya hiyo zikiwemo mkusanyiko wa kila mwaka ujulikanao kama TAMCO Day (Siku ya TAMCO), michezo ya watoto, futari za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Sherehe za Iddi.
Member wa  TAMCO Habiba Jatha Brown, akikusanya michango
Ama fedha zinazohudumia mipango ya Kidini na Kijamii nchini Tanzania, hizo huchangishwa maalum kupitia kikosi-kazi cha Uhamasishaji kikiongozwa Na Bwana Yussuf Mohamed. Michango hiyo huendeshwa pale panapotokea dharura, na kuzitumia fursa za mikusanyiko mbali mbali na kutangaza harambee.
"Inapotokea kuwa tunataka kutuma msaada Tanzania huomba michango kwa wanachama wetu, siyo Waislamu tu, bali hutafuta misaada hata kwa marifiki zetu wengine wasiokuwa Waislamu", alinena Bi Asha na kuelezea shukrani zake kwa marafiki hao kwa kuitikia wito wao huo wa misaada, huku akiwahakikishia kuwa fedha zote zinazokusanywa kwenye michango hiyo zinaelekea Tanzania.
"Na zile hela hazibaki Marekani, zinakwenda Tanzania kusaidia ndugu zetu ambao wanatuhitaji zaidi, na rekodi zote tunazo", alisisitiza.
Haya yakiendelea, TAMCO haijasahau swala la kuimarisha safu yake ya ndani ili kuweza kufanikisha shughuli zake khususan kwa upande wa wanawake ambao wana mchango mkubwa katika jamii. Uimarishaji wa safu hiyo unalenga zadi kwenye swala la elimu ya Kidini, ikifahamika kuwa jamii iliyoelimika ndiyo yenye uzalishaji bora.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake ya TAMCO Bi Jasmine 
Siri hiyo ilitobolewa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake ya TAMCO Bi Jasmine Rubama aliyeiambia Swahlivilla: "Tuna kamati ambayo bado iko kwenye maandalizi, lakini imefikia mbali, na lengo lake ni kuwaelimisha wanawake ambao mambo mengi yanawapa taabu, na hufika kwetu kutuuliza maswali mbali mbali na kuwapatia majibu"
Ili kurahisisha mawasiliano miongoni mwa wanachama wake, Kamati hiyo imeanzisha kundi maalum katika mtandao wa kijamii wa Whatsap likiwa na jina la "TAMCO WOMEN DMV", ambapo wajumbe hweza kutuma maswali yao na kujibiwa papo kwa papo. Inaposhindikana, basi swali hupelekwa kwa Wanazuoni ili kupatiwa jibu lake.
"Kwa vile elimu ni bahari pana, inapotokea kuwa kuna swali limetushinda tunawatafuta Wanazuoni kuwauliza na kutupaita Fatwa, kwa hivyo tunaelimishana kwa njia hiyo", alisema Bi Jasmine.
Hiyo ni hatua ya awali tu, lakini mipango ya baadaye ni kuweza kujenga Madrasa makhsusi kwa ajili ya wanawake wa jumuiya hiyo ili kuweza kutoa elimu kwa ufanisi zaidi, kama anavyoelezea Bi Jasmine: "Jambo jengine ambalo tumeazimia kulifanya ni kuweza kukutana na akina mama kwa njia ya madrsa, hilo tutalianzisha karibuni, na matayarisho yake yako njiani"

No comments: