ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 24, 2017

Wanachama wa CUF ya Lipumba ‘wawabadilikia’ waandishi


Wanachana wa CUF wanaomuunga mkono mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba walijikuta wakizozana wao kwa wao muda mfupi baada ya mwenyekiti huyo kumaliza mkutano wake na waandishi wa habari.
Mwenyekiti huyo alikuwa akizungumza na waandishi wa habari leo (Jumamosi) kuhusu kamati mpya ya maadili ya nidhamu iliyozinduliwa katika ofisi za chama hicho Buguruni.
Baada ya kumaliza kutoa maelezo yake, mwenyekiti aliketi chini na kisha Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Abdul Kambaya amesimama na kuwataka waandishi kutoka nje.
Lakini waandishi hao walisita kutii agizo hilo wakitaka kupata ufafanuzi wa baadhi ya hoja.
“ Ndugu waandishi tunaomba mtoke nje tuendelee na kikao chetu maswali mtauliza baada ya kamati kumaliza majukumu yake,” amesikika akisema Kambaya.
Hata hivyo, waandishi wameendelea kusisitiza kutaka kupata fursa ya kuuliza maswali kwa mwenyekiti ghafla kulisikika sauti toka nyuma ya ukumbi zikiwashinikiza waandishi hao watoke.
Mmoja wa mwanachama aliyekuwa amevalia fulana na kofia zenye nembo ya chama ndiye aliyeamsha zogo pale alipodai; “waondoke hawa waandishi kila siku wanakuja hapa hawaandiki habari zetu.”
Matamshi yake hayo yalidakwa na wengine waliokoleza mjadala hatua iliyofanya baadhi ya wanachama kusimama na kupinga hali hiyo.
“ Wewe ebu jiheshimu...acheni mambo yenu haya..ahaa hatutaki,” wamezozana wanachama hao.
Mzozo huo uliodumu kwa dakika tano umemalizika baada ya waandishi kutoka nje. Wakati wote wa malumbano hayo waandishi hawakuchangia neno lolote.
Mzozo huo ulihamia nje kwa dakika kadhaa huku baadhi ya wanachama wakivitaja na kuvituhumu vyombo vya habari kwa kutoandika habari zao.

Chanzo: Mwananchi

No comments: