Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa akiongea katika mkutano na waandishi wa habari kuelezea Tanzania itakavyokuwa wenyeji wa kuandaa Kongamano la ‘Global Logistics Summit 2017’ linalotarajia kufanyika Agost 23-26, 2017 jijini Dar es Salaam. Picha zote na Kajunason Blog/Cathbert Kajuna.
Kongamano hili la kiulimwengu litakaribisha zaidi ya wageni 350 wakiwa mawakala wa kusafirisha mizigo, wajumbe wa kibiashara, washiriki wa kibiashara, maafisa wa serikali, mabalozi kutoka ukanda wa Afrika na Mashariki ya Kati, n.k. Zaidi ya nchi 32 toka ulimwengu mzima zinategemewa kuhudhuria na kushiriki mkutano huu toka dunia nzima.
Mhe. Prof. Makame Mbarawa ameipongeza TAFFA kwa jitihada zake za kutengeneza ufahamu ambao ulihitajika kwa muda mrefu katika sekta ya uchukuzi ambayo ni muhimu katika taifa lolote sababu inawezesha usafirishaji wa watu na mizigo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (katikati) akiongea katika mkutano na waandishi wa habari kuelezea Tanzania itakavyokuwa wenyeji wa kuandaa Kongamano la ‘Global Logistics Summit 2017’ linalotarajia kufanyika Agost 23-26, 2017 jijini Dar es Salaam. Kulia ni Rais wa Chama cha Wakala wa Forodha Tanzania (Taffa), Stephen Ngatunga na kushono ni makamu wa Rais wa Chama cha Wakala wa Forodha Tanzania (Taffa), Edward Urio.
Waandishi wa habari wakifuatilia mkutano huo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa akitilia msisitizo jambo.
Rais wa Chama cha Wakala wa Forodha Tanzania (Taffa), Stephen Ngatunga (kulia) alisema kuwa Kongamano hili pia litaiwezesha Tanzania kupata fursa ya kukuza uchumi wake kupitia sekta ya usafirishaji na usambazaji na baadhi ya maswala kama uboreshaji wa bandari na kuifanya iwe ya kisasa, kuongeza vyanzo vya mapato na changamoto zingine zitapewa kipaumbele kwenye majadiliano.
Kongamano hili linafanyika wakati ambao wafanyabiashara wa Kitanzania wanahitaji uelewa zaidi pamoja na maarifa kuhusu njia bora za utendaji kazi zinazotumika katika dunia hii ya kidijitali ambapo teknolojia inatawala. Kwa hakika kuna fursa nyingi za ukuzaji wa biashara Tanzania kwa maana ya usafirisaji na uhifadhi wa mizigo hasa katika nchi zisizo na bahari kama Burundi, DRC, Rwanda, Zambia, Malawi na Uganda zinaweza kutumia bandari ya Dar es Salaam kama njia ya usafirishaji mizigo.
“Sisi kama TAFFA tunapiga hatua kuhakikisha tunaziwezesha biashara kupitia kongamano hili la GLS ambapo wadau mashuhuri na waliobobea katika fani hizi watatoa maarifa bora kwa wasafirishaji wa kimataifa. Hii ni mara ya kwanza kwa sisi kuwa wenyeji wa mkutano huu wa kiulimwengu. Tunafurahia sana kupata fursa hii ambayo itaitangaza Tanzania kama kituo kizuri cha usafirishaji.” Alielezea Ngatunga.
“Hii ni fursa muhimu kwa taasisi yoyote yenye maslahi na sekta ya usafirishaji iwe kama, wakala, kampuni ya bima, mtoa huduma, mwanasheria, mtoa bidhaa ama afisa biashara kutengeneza wigo na mahusiano ya kibiashara. Tunataka kuionyesha dunia kupitia mkutano huu kwamba Tanzania ni sehemu sahihi kwa biashara za ukanda huu.
No comments:
Post a Comment