Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi
Hamad Masauni (aliyevaa Kaunda suti), akiongozwa na Afisa Tarafa ya Amani,
wilayani Muheza, Ayubu Mhina kumuonyesha eneo la Kihara ambalo ni chanzo cha
maji cha Mto Zigi ambalo linasambaza maji sehemu kubwa ya Jiji la Tanga ambalo
limeharibiwa na wahalifu kwa kuchimba mashimo wakidai kuwa wanatafuta madini ya
dhahabu. Hata hivyo, Jeshi la Polisi linafanya oparesheni katika eneo hilo mara
kwa mara na pia linatarajia kujenga Kituo cha Polisi katika eneo hilo ili kupambana
na wahalifu hao. Kushoto ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Muheza, Oscar Joshua, na
kulia ni Mshauri wa Wagambo wilayani humo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi
Hamad Masauni (kushoto), akimsikiliza Mhifadhi Msaidizi Hifadhi ya Asili Amani,
wilayani Muheza, Bob Matunda (wapili kushoto), alipokua anamuonyesha eneo la
Kihara ambalo ni chanzo cha maji cha Mto Zigi lililoharibiwa na wahalifu kwa
kuchimba mashimbo wakidai wanatafuta madini ya dhahabu katika eneo hilo. Masauni
aliongozana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya muda wa usiku kwenda
kuangalia waharibifu hao walivyoliharibu eneo hilo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi
Hamad Masauni, akimfafanulia jambo Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhandisi Mwanaasha
Tumbo (kulia), mara baada ya kuangalia eneo la chanzo cha maji katika hifadhi
ya Msitu wa Asili wa Amani ambalo liliharibiwa na wahalifu kwa kuchimba mashimo
katika eneo la Kihara ambalo ni chanzo cha maji, wakidai wanatafuta madini ya
dhahabu katika eneo hilo. Masauni
akiongozana na Mkuu wa Wilaya hiyo, walifika eneo hilo la tukio muda wa usiku. Katikati ni Afisa Tarafa ya Amani, wilayani
Muheza, Ayubu Mhina.
Mbunge wa Jimbo Muheza, Balozi Adadi
Rajabu akimuonyesha Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto), ameneo mbalimbali
yaliyoathiriwa na wachimbaji wa madini katika eneo hilo ambalo ni muhimu kutokana
kuwa na chanzo cha maji ambayo yanatumika katika eneo kubwa mkoani Tanga.
Wapili kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Mwanaasha Tumbo. Picha zote na Wizara ya Mambo ya
Masauni alifika katika eneo hilo la tukio saa mbili usiku na kujionea maeneo yaliyoharibiwa kwa kuchimbwa mashimo makubwa na wahalifu hao wakidai kuwa wanatafuta madini ya dhahabu. Hata hivyo, hakuna mhalifu aliekamatwa katika eneo hilo wakati wa oparesheni hiyo.
Akizungumza katika eneo hilo lililopo Tarafa
ya Amani, wilayani humo jana, Masauni ambaye pia aliambatana na Mbunge wa Jimbo
la Muheza, Balozi Adadi Rajabu, alisema Jeshi la Polisi litaendelea kufanya
oparesheni katika eneo hilo usiku na mchana kwa kushirikiana na walinzi wa msitu
ili kuwaondoa wahalifu hao haraka
iwezekanavyo.
Masauni alisema licha ya Polisi
kuendelea kufanya doria katika eneo hilo lakini wanatarajia kufungua kituo cha
polisi ili kuongeza ulinzi zaidi katika eneo hilo muhimu ambalo ndio chanzo cha
maji kwa sehemu kubwa ya wakazi wa Mji wa Tanga.
“Tumepanga kuimarisha ulinzi zaidi katika
eneo hili kwa kujenga kituo cha polisi ambapo askari wetu watashirikiana na
walinzi wa misitu kufanya doria ya kupambana na wahalifu,” alisema Masauni na
kuongeza;
“Kwa habari zisizo rasmi tulizozipata
katika vyanzo vyetu, hawa wahalifu wanamtandao mkubwa wakishirikiana na watu
mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara na hata baadhi ya watumishi wa umma,
tutaendelea kufanya uchunguzi huu kwa kina kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa
wilaya ili kuwabaini wahalifu wote haraka iwezekanavyo.”
Hata hivyo, Masauni alifafanua kuwa, watafanya
uchunguzi wa kina kuwachunguza wale wote waliohusika kuwaficha wahalifu iwe
askari polisi, iwe mamlaka yoyote nyingine, iwe hakimu au watu wa aina yoyote watachunguzwa.
Watanzania tunapaswa tulinde rasilimali za Taifa pamoja na kusimamia ipasavyo.
Masauni alitarajia kwenda mkoani
Kilimanjaro kuendelea na ziara yake lakini mara baada ya kupewa taarifa kuhusu
uharibifu mkubwa unaofanywa na wahalifu katika msitu huo wa asili, ndipo
akaelekeza safari ya kwenda eneo hilo kwanza kuangalia hali halisi pamoja na
kuwasaka wahalifu hao ambao inasemekana wana watu hao wanapoona msafara unakuja
katika eneo hilo, wanaambizana na utoweka haraka katika eneo hilo.
Katika ziara yake ya siku moja mkoani
humo, kwa kutembelea mjini Tanga, Wilaya ya Pangani na baadaye akamalizia
Wilaya ya Muheza, Masauni alitoa maelekezo mbalimbali kwa Taasisi zilizochini
ya Wizara yake hasa Jeshi la Polisi na
Uhamiaji kuakikisha wanaongeza nguvu kubwa ya kuchunguza na kuzidi kuwasaka wahamiaji
haramu mkoani humo, na pia aliamuru ujenzi wa Gereza la Muheza kuanza mara moja
ili kupunguza msongamano mkubwa uliopo katika Gereza Kuu la Tanga pamoja na
mengineyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya
Muheza, Mhandisi Mwanaasha Tumbo
alimshukuru Naibu Waziri huyo kwa kufanya ziara katika wilaya yake, na pia
alishukuru kwa kuamuru ujenzi wa Gereza Muheza kuanza mara moja na kuahidi
kuyafanyia kazi zaidi maelekezo mbalimbali aliyoyatoa wilayani humo.
Hata hivyo, Mhifadhi Msaidizi wa Hifadhi
hiyo ya Asili, Bob Matunda alisema mara kwa mara wanawakamata wahalifu hao na
kuwafikisha katika vyombo vya usalama, na akaahidi kuwa wataendelea
kushirikiana kikamilifu na Jeshi la Polisi katika oparesheni mbalimbali za
kuwaondoa wahalifu hao katika eneo hilo.
1 comment:
Mbona hawaendi kufanya msako Kibiti?
Post a Comment