Advertisements

Thursday, July 13, 2017

Mfumo mpya kuwaondoa watumishi waliostaafu kila ifikapo saa 6 usiku

Waajiri nchini wametakiwa kufanya uhakiki wa kina wa vyeti vya elimu kwa ajira mpya zitakazotolewa ili kuwa na watumishi wenye sifa zinazostahili katika utumishi wa umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, amesema hayo leo Alhamisi, Julai 13 katika kikao kazi na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Amewataka wWaajiri kusafisha taarifa za watumishi wa umma mara kwa mara katika Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS).
“Kuna watumishi ambao muda wao wa kuwepo kazini umemalizika (wamestaafu) lakini bado wanaendelea kuwepo, mfumo wa HCMIS sasa kila ifikapo saa 06:01 usiku utakuwa unawaondoa wale wote ambao muda wao wa kuwepo kazini umefika, lakini bado wanaendelea kuwepo kwenye Mfumo,” amesema.
Kairuki amesema uhakiki wa kina utasaidia kuepuka kutojirudia tena kwa suala la watumishi wa umma wanaoghushi vyeti.
“Jana tumetoa vibali vya ajira 10,184 kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekretarieti za Mikoa, Wakala za Serikali, pamoja na Taasisi na Mashirika ya Umma ili kujaza nafasi zilizoachwa na watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti vya elimu, hivyo napenda niwasisitize sana waajiri wote kufanya uhakiki wa kina ili tusiwe tena na watumishi wa umma wasiostahili katika orodha ya malipo,” amesema.
Waziri Kairuki amesisitiza kuwa zoezi la uhakiki ni endelevu ambapo lazima lifanyika pale mtumishi wa umma atakaporudi katika kituo cha kazi kutoka masomoni na watakaorejea katika utumishi wa umma baada ya likizo bila malipo au sababu nyingine.
“Tunafanya hivi sio kwa nia mbaya, bali tunataka tuwe na watumishi wanaostahili kuwepo katika utumishi wa umma kwa sababu wanaoghushi wanaziba nafasi za wale wanaostahili kuwepo na wenye sifa katika utumishi wa umma,” Kairuki ameongeza.
Kairuki yupo katika ziara ya kikazi katika Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa leo ni siku yake ya nne aliyoitumia kukutana na watendaji na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, baada ya kuzungumza na watumishi wa umma wa Temeke na Mbagala.
Lengo la ziara ni kukutana na watumishi wa umma na kusikiliza malalamiko, ushauri na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi ili kuzifanyia kazi na kuleta mabadiliko katika Utumishi wa Umma nchini.

No comments: