Advertisements

Sunday, July 9, 2017

Polisi wawatoa hofu wakazi Mwanza, msako waendelea

Wakati wakazi wa mtaa wa Fumagila Mashariki Kata ya Igoma, Mwanza wakiwa na hofu baada ya watu wawili wanaodhaniwa kuwa majambazi kukimbia juzi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, limesema linaendesha msako mkali kuwasaka watu hao.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi ameendelea kuwatoa hofu wakazi hao kuwa hakuna jambo baya litakalotokea kwani polisi wamejipanga vya kutosha na wapo kwenye msako kila kona kuhakikisha kundi lote la uhalifu linatiwa nguvuni.
“Wakazi hao wasiwe na wasiwasi tumejipanga vya kutosha, hakuna kibaya kitakachotokea hilo kundi tumeshapata taarifa zao hivyo tutawasambaratisha wote, kikubwa wananchi waendelee kutoa taarifa na kushirikiana na polisi kwa watu wanaowatilia mashaka.” Amesema.
Katika tukio hilo polisi waliua watu sita, kukamata silaha ya SMG AK47, magazine mbili kila moja ikiwa na risasi 30, risasi 36 za AK 47 ambazo zikuwa nje ya magazine, risasi moja aina ya rafal, risasi nane za shortgun.
Silaha nyingine zilizokamatwa ni bastola nne za kienyeji, sare za jeshi za nchi jirani, kofia sita za kuziba uso, kitambaa cha kichwani, nusu kanzu, nguo mbalimbali za kiume, mabegi matatu yaliyokuwa yakihifadhi silaha hizo, baiskeli mbili, pikipiki moja, unga na dagaa.

No comments: