Advertisements

Monday, July 3, 2017

Rugemalira, Sethi waongezewa mashtaka sita

Mfanyabiashara Harbinder Singh Sethi na James Rugemalira wamepandishwa kizimbani kwa mara nyingine katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 12, badala ya mashtaka sita waliyosomewa awali.
Miongoni mwa mashtaka hayo 12 ya uhujumu uchumi yamo mashtaka matano ya kutakatisha fedha na kuisababisha hasara ya USD 22, 198, 544.60 na Sh 309,461,300,158. 27.
Akiwasomea hati mpya ya mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shedrack Kimaro kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alidai wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kighushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kuisababishia Serikali hasara na kutakatisha fedha.
Washtakiwa hao katika shtaka la kwanza wanadaiwa, Rugemarila ambaye ni Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL, Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa PAP wanadaiwa kuwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jiji Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Kimaro alidai katika shtaka la pili la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao kati ya Oktoba 18, 2011na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam wakiwa siyo watumishi wa umma na watumishi wa umma walitekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.
Kwa upande shtaka la tatu, Sethi anadaiwa kuwa Oktoba 10, 2011 katika mtaa wa Ohio Ilala Dar es Salaam akiwa na nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14 ya usajili wa makampuni na kuonyesha yeye ni mtanzania anayeishi Kitalu namba 887 Mtaa wa Mrikau Masaki wakati akijua ni uongo.
Seth katika shtaka la nne anadaiwa kutoa nyaraka ya kughushi ambayo ni fomu namba 14a ya usajili wa kampuni kwa ofisa msajili wa kampuni, Seka Kasera kwa njia ya kuonyesha kwamba yeye ni mtanzania na Mkazi wa Mtaa wa Mrikau.
Katika shtaka la tano, washtakiwa wote, wanadaiwa kuwa kati ya Novemba 28/29, 2011 na Januari 23, 2014 makao makuu Benki ya Stanbic Kinondoni na Benki ya Mkombozi Tawi St Joseph kwa ulaghai washtakiwa hao walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), walijipatia USD 22,198,544.60 na Sh 309, 461,300,158.27.
Katika shtaka sita la kusababisha hasara, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la kati Kinondoni kwa vitendo vyao waliisababishia Serikali hasara ya USD 22, 198, 544.60 na Sh 309,461,300,158.27.
Kimaro alidai katika la saba, kuwa kati ya Novemba 29, 2013 na Januari 23, 2014 maeneo tofauti Dar es Salaam kwa pamoja walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT USD 22,198,544.60 na Tsh 309,461,300, 158.27 wakati wakijua fedha hizo zao la kujihusisha na genge la uhalifu.
Shtaka la nane, Kimaro alidai kuwa Novemba 29, 2013 katika tawi la kati la Benji ya Stanbic Tanzania Wilaya ya Kinondoni Sethi alitakatisha fedha kwa kuchukua BoT USD 22,198,544.60 wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.
Kwa upande wa shtaka la tisa, Sethi anadaiwa kuwa kati ya Novemba 29, 2013 na Machi 14,2014 katika tawi la kati la Benji ya Stanbic Kinondoni Dar es Salaam alitakatisha fedha, Sh 309,461,300,158.27 kutoka BoT wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.
Shtaka ya kumi, inadaiwa Januari 23, 2014 katika Benki ya Mkombozi tawi la St Joseph Cathedral, Rugemalila alitakatisha fedha, Sh 73, 573, 500,000 kutoka kwa Seth wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.
Kwa upande wa shtaka la 11, Kimaro alidai kuwa Januari 23,2014 katika Benki ya Mkombozi tawi la St Joseph Cathedral, Rugemarila alitakatisha fedha USD 22,000,000 kutoka kwa Seth wakati akijua fedha hizo ni zao la uhalifu.
Shtaka la 12, Seth anadaiwa kuwa Januari 28, 2014 katika tawi la kati la Benki ya Stanbic Wilaya ya Kinondoni alihamisha Rand (zar 1,305,800 kwenda kwenye akaunti namba 022655123 katika Standard bank Land Rover Sandton Johannesburg wakati akijua katika kipindi anahamisha fedha hizo zimetokana na zao la kujihusha na genge la uhalifu.
Washtakiwa hawakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hao.
Upande wa mashtaka ulidai upelelezi bado haujakamilika na washtakiwa wamepelekwa rumande hadi Julai 14, 2017.
Hata hivyo mashtaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili washtakiwa hao hayana dhamana.

No comments: