Advertisements

Sunday, July 23, 2017

Wanasheria watoa tamko kukamatwa kwa Lissu

Vyama vitatu vya wanasheria Afrika vimetoa tamko la pamoja kulaani kukamatwa kwa Rais wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS), Tundu Lissu alipokuwa akielekea Kigali, Rwanda kwenye mkutano wa wanasheria wa Afrika Mashariki.
Tamko hilo limetolewa kwa pamoja na Chama cha wanasheria cha Afrika Mashariki (EALS), Chama cha Wanasheria cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-LA) na Muungano wa Wanasheria Afrika (PALU).
Tamko hilo lililosainiwa na Rais wa PALU, Elijah Banda, Rais wa Sadc LA, James Banda na Rais wa EALS, Richard Mugisha limeeleza kwamba Lissu alikamatwa kabla ya kukamilika kwa uchunguzi wa tuhuma dhidi yake , jambo ambalo ni kinyume na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria nyingine za kimataifa.
Muungano wa vyama hivyo umebainisha wazi kwamba mfululizo wa matukio hayo ni mwanzo wa kuzorota kwa uhusiano kati ya TLS na serikali ya Tanzania.
"Kwa kuwa suala hili liko mahakamani, hatutasema mengi kwa sasa, isipokuwa tunazikumbusha pande zote kutambua uwepo wa sheria hasa zile zinazotambua haki za binadamu. Tutaweka utaratibu wa kufuatilia mashitaka dhidi ya Lissu," inasomeka sehemu ya tamko hilo.

Chanzo: Mwananchi

No comments: