Advertisements

Monday, July 10, 2017

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO ZANZIBAR AZUNGUMZA NA WAANDISHI KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA IDADI YA WATU DUNIANI

 Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar Dkt. Khalid Salum Mohamed akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na maadhimisho ya siku ya Idadi ya Watu duniani ambayo huadhimishwa kila ifikapo July,11. Kulia yake ni Katibu Mtendaji Tume ya Mipango Zanzibar Juma Hassan Reli.
 Baadhi ya wandishi wa habari wakifuatilia mkutano wao na Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dkt. Khalid Salum Mohamed hayupo pichani uliofanyika wizarani kwake Mjini Zanzibar.
 Mwandishi wa habari wa Idara ya Habari Maelezo Faki Mjaka akiuliza swali kwa Waziri wa Fedha na Mipango juu ya siku ya Idadi ya Watu duniani katika mkutano uliofanyika Wizarani kwake Vuga.
 Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar Dkt. Khalid Salum Mohamed akitoa ufafanuzi wa maswali alioulizwa na wandishi wa habari.
Picha na Makame Mshenga.

Na Maelezo Zanzibar 
Wakati dunia inaungana kuadhimisha siku ya Idadi ya Watu duniani bado uzazi wa Mpango unaonekana ni changamoto katika baadhi ya maeneo ya Zanzibar.
Hali hiyo hupelekea ongezeko la idadi ya watu lisiloendana na kasi ya ukuaji wa uchumi na upatikanaji wa huduma za jamii katika maeneo mbalimbali nchini.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Khalid Salum wakati akitoa taarifa yake kwa Vyombo vya habari kuelekea maadhimisho hayo hapo kesho.
Amesema ni vyema jamii kujenga mwamko juu ya umuhimu wa suala la uzazi wa Mpango ili kujenga jamii bora, iliyoimara na chachu katika kuongeza kasi ya maendeleo.
Dkt. Khalid amesisitiza jamii kuendelea kutumia njia za asili za uzazi wa mpango ambazo ni salama kwa afya ya mama na kuhudhuria katika Vituo vya afya kupata taaluma ya matumizi ya njia za kisasa pale inapohitajika.
Ameongeza kuwa suala la uzazi wa Mpango limesisitizwa hata katika Vitabu vya Dini ili kumpa nafasi Mama mzazi kurudisha afya na nguvu anazozitumia wakati wa kubeba mimba na kujifungua.

Kila ifikapo July 11, Zanzibar huungana na nchi zingine duniani kuadhimisha Siku ya Idadi ya Watu duniani ambapo kwa mwaka huu Kauli mbiu ni “Uzazi wa Mpango:Kuwawezesha Watu,kuendeleza Mataifa”

No comments: