ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, August 6, 2017

BAMBI BAMBI MY DEAR, MY DEAR, MY DEAR

BAMBI BAMBI MY DEAR MY DEAR MY DEAR...
ALIITWA Bambi! Ni jina lenye asili ya Italia, jina hili hupewa mabinti wazuri waliotosheka urembo. Kama lilivyo jina lake, Bambi alikuwa Bambi kweli. Bahati yake hakuzaliwa enzi za utumwa, angevushwa bahari kwa senti kiduchu!

Pendapenda alibahatika kumpata Bambi, wakapendana wangali bado vijana wenye nguvu. Mapenzi motomoto yaliwatawala wawili hawa, kuna waliozusha eti kuna wakati mapenzi yalikolea moto mpaka zikatoka cheche! Ulikuwa uzushi.

Pendapenda alimpenda vilivyo Bambi wake. Alimpa kila alichokuwa nacho. Kipi Bambi aliomba akanyimwa? Hakuna! Bambi akaendelea kutumbua katika vinono alivyopewa.

Kuna wakati mama yake Bambi aliugua, Pendapenda akatinga ukweni. Wakamweleza mkwe alihitaji figo. Pendapenda alitoa. Mwanaume mwenye upendo akabaki na figo moja. Upendo wa ajabu huu! Hakuishia hapo, akamjengea nyumba mama mkwe, na akaamua kuchukua majukumu yote, ya mjane yule. Alisikika akisema, “Mama we tulia… usifanye kazi nitakuhudumia!”

Alifanya mambo mengi yasiyoweza kuelezwa yote. Kwa bahati mbaya ule wakati wa dharura ukafika. Kumbe Pendapenda alikopa benki akashindwa kurejesha kutokana na biashara zake kuyumba. Kila kitu chake kikachukuliwa katika mnada, akabaki kapuku wa kutupwa.

Bambi msichana aliyezoeshwa starehe na aliyekuwa akiwindwa kutwa na vigogo wa jiji, akasahau fadhila zote alizofanyiwa na Pendapenda, huyoo akatokomea kwa mwanaume mwingine mwenye fedha! Pendapenda akaachwa!

Pendapenda alipenda kweli. Uchungu wa kupoteza mali na mwanamke aliyempenda, ukamtia wazimu. Akili yake ikayumba! Akafikiri tofauti.

Aliamua kujiua! Akatamani kunywa sumu ya panya, lakini hakuwa na pesa ya kununulia sumu. Akataka kujinyonga, akawaza akagundua hana pesa ya kununulia kamba imara!

Akagundua njia moja rahisi, haraka akaelekea katika jengo moja refu, akakwea mpaka juu, akasimama. akipiga ukunga wa uchungu, watu wakajaa chini wakimbembeleza asijirushe. Bambi hakuwepo, alikuwa Visiwa vya Shelisheli akiponda starehe na bwana mwenye fedha nyingi.

Pendapenda hakusikia ushauri wa mtu, moja.. mbili… tatu.. alijirusha. Jengo lilikuwa refu, niliuona mwili wake ukija chini kwa kasi, pia niliiona fulana kifuani pake yenye maandishi yaliyosomeka,
‘BAMBI BAMBI, MY DEAR MY DEAR MY DEAR…’

Sikutaka kumshuhudia akifika chini, niliamua kuondoka, hata kabla sijapiga hatua mbili, kikasikika kishindo kikubwa… ‘puuuuuuuh’… vikafuata vilio vya akinamama wastaarabu wa Pwani. 

GPL


No comments: