ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 3, 2017

Bilionea IPTL kutibiwa Amana au Lugalo

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru mshtakiwa Harbinder Singh Sethi anayeumwa atibiwe hapahapa nchini.
Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amesema hajawahi kusema atibiwe nje ya nchi, bali atibiwe nchini na kwamba ndani ya siku 14 wanasubiri matokeo kama amefikishwa hospitali kutibiwa ama la.
Amesema hay oleo Alhamisi, Agosti 3 baada ya Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai kuomba atibiwe katika Hospitali ya Amana au Lugalo.
Akiwasilisha hoja hiyo leo kwa Hakimu Shaidi, Swai amekiri kuwepo kwa amri ya Mahakama ya mshtakiwa kupatiwa matibabu.
Hata hivyo, amedai hawana ushahidi kuwa siku mshtakiwa alipokamatwa alikuwa anakwenda Afrika Kusini kutibiwa.
Pia, amedai suala la mshtakiwa kupelekwa nje ya nchi kutibiwa si sahihi kwa sababu utaratibu wa mgonjwa kupelekwa nje unafahamika na kwamba haendi kwa sababu ya amri ya Mahakama.
Swai amepinga Sethi kutibiwa nje kwa kuwa madaktari wa hapa nchini hawajakiri kushindwa na hakuna uthibitisho wa madaktari kwamba wameshindwa kumtibu.
Pia, amedai hakuna utaratibu wa mgonjwa kupelekwa Muhimbili moja kwa moja anatakiwa kuanzia Hospitali ya Amana ama Lugalo wao ndiyo watafanya utaratibu wa kumuhamishia Hospitali ya Muhimbili.
Amedai Magereza ambapo Sethi anatibiwa ndiyo wametakiwa kuthibitisha na kufanya utaratibu apeleke Hospitali ya Amana.
Amebainisha kuwa Amana nao hawajasema wameshindwa kumtibu hivyo ameomba aendelee kutibiwa katika Hospitali ya Amana.
Kuhusu ombi la Wakili wa Sethi, Alex Balomi kuomba kesi itajwe ndani ya siku saba kwa ajili ya kuangalia kama amepelekwa hospitali.
Swai aliyeomba siku 14 alidai kutajwa ndani ya siku saba ni kumsumbua mgonjwa na kwamba muda huo autumie kwenda hospitali na siyo mahakamani.
Amebainisha kuwa ndani ya siku 14, atakuwa amefikishwa katika Hospitali ya Amana ama Lugalo kupatiwa matibabu kwa kuwa taratibu za Magereza zimekamilika na wao watasimamia.
Lakini Balomi amedai hadi sasa mteja wake hajapelekwa hospitali na akaomba mahakama isimamie amri yake ya mshtakiwa kupatiwa matibabu.
Hakimu Shaidi katika uamuzi wake amewapa siku 14 Takukuru kama walivyoomba awali, ili kuangalia kama atakuwa amefikishwa katika Hospitali ya Amana ama Lugalo kupatiwa matibabu.

Kesi imeahirishwa hadi Agosti17, 2017.
Awali, Julai 14, 2017, Wakili wa kujitegemea wa Sethi, Alexi Balomi aliifahamisha mahakama kuwa Sethi anaumwa na kwamba hali yake ilikuwa ikiendelea kubadilika kuwa mbaya na alikuwa hawezi kupata usingizi kwa wiki nne.
Wakili Balomi aliiambia mahakama hiyo kuwa Seth anasumbuliwa na uvumbe tumboni kama puto ambao unahitaji uangalizi wa karibu wa madaktari.
Katika kesi hiyo, Sethi na James Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kighushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababisha hasara ya Doa za Marekani 22, milioni na Sh309 bilioni.

No comments: