ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 25, 2017

DIASPORA NI RASILIMALI MUHIMU KATIKA KUIMARISHA UCHUMI AFRIKA, MAKAMBA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Issa Haji Ussi Gavu, akimkaribisha Mgeni Rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. January Makamba (Mb.) kuzungumza na Watanzania waishio ughaibuni.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. January Makamba (Mb.) ambaye alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akitoa hotuba ya Ufunguzi wa Kongamano la Nne la Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora), linalofanyika katika Hoteli ya Sea Cliff Mjini Zanznibar. 
Baadhi ya Watanzania waishio Ughaibuni wakisikiliza Hotuba ya ufunguzi. 
Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nao wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mgeni Rasmi 
Sehemu nyingine ya wageni waliohudhuria mkutano wa nne wa Diaspora unaoendelea mjini Zanzibar 
Mhe. Makamba akiendelea kuzungumza na Watanzania waishio ughaibuni. 
Watanzania waishio ughaibuni wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi 
Watanzania waishio ughaibuni wakiingia kwenye meli ya MV Mapinduzi 2 tayari kuzunguka na kujionea mandhari ya visiwa vya Tumbatu na Nugwi kwa madhumuni ya kutambua fursa za uwekezaji.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bi. Severa Kazaura (wa kwanza kulia), akiwa katika chumba cha manahodha ambapo alimshuhudia Nahodha wakike akiiongoza meli MV Mapinduzi. 
Mkurugenzi wa Mamlaka ya uendelezaji Biashara Tanzania(TanTrade) Bw Edwin Rutageruka (kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF), Mh William Erio na Mkuu wa Kitengo na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Bi. Mindi Kasiga wakiwa katika safari ya Kuzunguka na meli ya MV Mapinduzi pamoja na Watanzania waishio Ughaibuni. 
Watanzania waishio Ughaibuni wakipata burdani kwenye meli ya MV Mapinduzi waliyoitumia kuzunguka nayo kujionea Mandhari ya Visiwa vya Tumbatu na Nungwi..

Taarifa kwa Vyombo vya Habari 

Serikali imeahidi itaendelea kuboresha mazingira wezeshi ili wanadiaspora wengi zaidi waweze kuwekeza nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Januari Makamba (Mb) ambaye alimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa Nne wa Diaspora unaofanyika katika Hoteli ya Sea Cliff mjini Zanzibar.

Mhe. Makamba alibainisha kuwa mwaka jana pekee, Bara la Afrika lilipokea kiasi cha Dola za Marekani bilioni 33 kutoka kwa Diaspora, kiasi ambacho ni kikubwa kuliko misaada ambayo bara hilo inapokea kutoka nchi wahisani.

Alisema hiyo inadhihirisha kuwa endapo nchi zitaweka mazingira mazuri ya kuvutia wanadiaspora watakuwa na mchango mkubwa wa kuinua uchumi wa nchi zao.

"Nchi nyingi duniani zinatumia diaspora yao kuendeleza mipango ya maendeleo na kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi zinazojitokeza kama vile uhaba fedha za kigeni" Waziri Makamba alisema

Alitolea mfano wa Zimbabwe ambayo mwaka jana ilipokea kiasi cha Dola milioni 750 kutoka Diaspora ya nchi tatu ambazo ni Afrika Kusini, Marekani na Uingereza na kufanikiwa kupunguza tatizo la uhaba wa fedha za kigeni.

Akionesha zaidi umuhimu wa diaspora katika uchumi wa nchi, Mhe. Makamba alisema nchi ya Kenya kwa mwaka jana pekee, iliingiza Dola bilioni 1.7 kupitia diaspora, kiasi ambacho ni kikubwa kuliko ilichopata kupitia sekta ya utalii na kilimo cha maua ambazo ndio sekta zinazoingiza fedha nyingi kwa nchi hiyo.

Alieleza namna baadhi ya nchi zinavyotumia mbinu mbalimbali kuwawezesha diaspora wao kuwekeza. Baadhi ya mbinu hizo ambazo zinaweza zikatumiwa hata na nchi yetu ni pamoja na kutoa hati fungani maalum kwa ajili ya diaspora. Alisema mbinu hiyo inatumiwa na nchi nyingi duniani kama India na Nigeria kukusanya fedha kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ikiwemo ya miundombinu.

Mhe. Makamba aliwahimiza wanadiaspora kuwekeza nchini na kwamba Serikali itatoa ushirikiano unaohitajika kwa yeyote mwenye dhamira ya dhati ya kuwekeza. Aidha, alieleza kuwa yeyote anayetaka kuwekeza nchini na akakumbana na vikwazo atoe taarifa mapema kwenye mamlaka husika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Baadhi ya watoa mada ambao ni pamoja na Geofrey Simbeye wa TPSPF; Joseph Simbakalia wa EPZA; Geofrey Mwambe wa TIC na Edwin Rutagerura wa TANTRADE waliwashauri wanadiaspora kuunda kampuni ya uwekezaji katika maeneo yao wanayoishi. Kampuni hiyo itakuwa ni fursa kwa kila mwanadiaspora kuchangia mtaji angalau wa Dola 200 kila mwezi ili fedha hizo zitumike kuwekeza katika miradi mbalimbali nchini.

Wabobezi hao wa masuala ya uchumi na biashara walishauri pia wanadiaspora wawekeze katika miradi isiyohitaji mitaji mikubwa kama vile miradi ya kuzalisha bidhaa zinazotumia ngozi kama viatu, mabegi na mipira.

Mwisho wanadiaspora wanaoshiriki mkutano huo wenye kaulimbiu isemayo "Mtu kwao ndio Ngao" walielezwa kuwa hali ya kisiasa nchini ni tulivu, hivyo wasiwe na shaka yeyote wawekeze kwa wingi miradi yao itakuwa salama.

-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Zanzibar, 23 Agosti 2017




No comments: