ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 25, 2017

WATUMISHI WA UMMA ZANZIBAR WAPIGWA MSASA


Katibu Mtendaji wa Mpango wa Afrika wa Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) Tanzania, Bi. Rehema Twalib akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Kubingwa Mashaka Simba (hayupo pichani) kwenye ufunguzi wa Warsha ya kuunganisha mipango ya APRM na Mipango ya Serikali inayofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, mjini Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu, Bw. Kubingwa Mashaka Simba akitoa hotuba kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika ufunguzi wa Warsha ya ya kuunganisha mipango ya APRM na Mipango ya Serikali

Sehemu ya viongozi waliohudhuria kwenye Warsha hiyo wakimsikiliza kwa makini Mhe. Simba.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar, Bw. HAji Kombo (katikati), wa kwanza kushoto ni Mratibu wa Utawala APRM, na kulia ni Amani A.M. Shein nao wakifuatilia kwa makini ufunguzi wa Warsha hiyo.

Mjumbe wa Jopo la Watu Mashuhuri na Kiongozi wa Mchakato wa Tanzania toka APRM, Mhe. Bridget Mabandla naye akizungumza kwenye ufunguzi huo.

Sehemu ya washiriki wa ufunguzi huo wakisikiliza kwa makini.

Sehemu ya watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wa kwanza kulia ni Halima Salim Abdallah, na katikati ni Hamida Makame Juma.

Watumishi wa APRM Tanzania, Bi. Stella William (kushoto`) na Bi. Elizabeth Ngereza nao wasikiliza hotuba iliyokuwa ikiendelea kutolewa na mgeni rasmi (hayupo pichani).

Bw. Max Ochai kutoka (UNECA), akitoa mada ya kwanza mara baada ya kumalizika kwa zoezi la ufunguzi

Sehemu ya washiriki wakifuatilia kwa kumsikiliza Bw. Ochani (hayupo pichani) alipokuwa akiwasilisha mada ya kwanza.

Bw. Ochani akiendelea kutoa mada yake kwa washiriki

Picha ya pamoja mara baada ya kumaliza ufunguzi wa Warsha hiyo.



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Watumishi wa umma Zanzibar wapigwa msasa kutekeleza Mipango ya Serikali

Taasisi za Umma zimeshauriwa kujikita zaidi katika utekelezaji wa mipango iliyojiwekea badala ya kutumia muda mwingi kupanga mipango isiyotekelezwa. 

Ushauri huo umetolewa leo kwenye warsha ya kuwajengea uwezo watendaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuingiza Mpango kazi wa utelezaji wa APRM kwenye mipango ya maendeleo ya nchi kama vile Dira ya Zanzibar 2020, MKUZA III na Mipango ya Matumizi ya Muda wa Kati. 

Warsha hiyo ya siku mbili imeandaliwa na APRM Tanzania na inafanyika katika Hoteli ya Golden Tulip mjini Zanzibar tarehe 24 na 25 Agosti 2017.

Mgeni Rasmi kwenye warsha hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Kubingwa Mashaka Simba ambaye alimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Haroun Ali Suleiman aliwahakikishia washiriki kuwa Serikali ya Zanzibar imejipanga vema kutekeleza changamoto zote zilizobainishwa kwenye ripoti ya APRM iliyowasilishwa rasmi kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan mwanzoni mwa mwezi Agosti 2017.

Bw. Simba alieleza kuwa tayari Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilishachukua hatua za kuimarisha Utawala Bora ikiwemo kuunda taasisi za kusimamia suala hilo ambazo baadhi yao ni Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Tume ya Kupambana na Rushwa pamoja na ugatuzi wa madaraka. 

Wadau wanaoshiriki warsha hiyo walibainisha kuwa changamoto kubwa katika taasisi za umma ni utekelezaji wa mipango iliyowekwa, Hivyo kuna umuhimu wa APRM kuangalia namna ya kujenga uwezo wa watumishi katika kutekeleza mipango ya Serikali kwa kuzingatia namna ya kupata rasilimali zinazohitajika na zenye uwezo wa kutekekeza mipango iliyopo pamoja na muda wa kutekeleza mipango hiyo.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa APRM, Tanzania, Bi. Rehema Twalibu alisema warsha hiyo ni muhimu kwa watumishi wa Serikali ya Zanzibar kwa kuwa itawapa uwezo wa kuandaa taarifa ya utekelezaji wa changamoto zilizoainishwa kwenye ripoti ya APRM iliyowasilishwa miaka mitano iliyopita kwa Wakuu wa Nchi zilizoridhia Mpango wa APRM. 

Taarifa ya utekelezaji itakayoandaliwa na Serikali ya Zanzibar itajumuishwa na taarifa ya Tanzania Bara ili kupata ripoti moja ambayo inatarajiwa kuwasilishwa na Mhe. Rais kwa Marais wenzake wanaounda APRM baadaye mwaka huu.

-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Zanzibar, 24 Agosti 2017

No comments: