ANGALIA LIVE NEWS
Tuesday, August 1, 2017
HOSPITALI ZOTE ZA MIKOA ZIJENGE VITUO VYA METHADONE-MAJALIWA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amegiza hospitali zote za mikoa nchini kujenga vituo vya kutolea huduma ya Methadone kwa ajili ya kuwahudumia waathirika wa dawa za kulevya.
Alitoa agizo hilo jana (Jumatatu, Julai 31, 2017) alipozindua kituo cha kuhudumia waathirika wa dawa za kulevya katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, ambapo alisema Serikali inaendelea na mpango wake wa kudhibiti uingizwaji wa dawa hizo.
Kituo hicho kinatarajiwa kuhudumia watumiaji wa dawa za kulevya katika mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini, ambayo ni Iringa, Njombe, Ruvuma, Katavi, Rukwa, Songwe na Mbeya.
Waziri Mkuu alisema vituo vya kuhudumia waathirika wa dawa za kulevya ni msaada mkubwa kwa vijana kwa kuwa mbali na kupewa dawa pia watafundishwa stadi za maisha ili wanapomaliza matibabu waweze kushiri katika shughuli za maendeleo ikiwemo kujiajiri.
Hata hivyo aliwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwafichua wazalishaji, watumiaji na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kwa sababu ni watu wanaoishi nao katika jamii.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya, Rodgers Sianga alisema licha ya matumizi ya dawa za kulevya kuathiri mfumo wa fahamu pia watumiaji wako katika hatari ya kuugua homa ya ini.
Alisema vituo hivyo licha ya kutoa dawa ya methadone pia waathirika wa dawa za kulevya ambao watagundulika kuwa na maradhi mengine kama ukimwi, kifua kikuu, matatizo ya kisaikolojia pamoja na homa ya ini pia watatibiwa katika vituo hivyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dkt.Godlove Mbwanji alisema matumizi ya dawa za kulevya yamechangia ongezeko la wagonjwa wa akili mkoani Mbeya, ambapo mwaka jana pekee walibainika wagonjwa 486.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment